MKURUGENZI wa Mashitaka (DPP), Eliezer Feleshi, amesema haoni mantiki yoyote au uhalali wa Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), kumshitaki Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
Alisema hayo janai wakati akijibu maswali ya waandishi
wa habari, baada ya kufungwa kwa mkutano wa siku tatu wa mawakili wa Serikali
wafawidhi, wakuu wa upelelezi wa mikoa na vikosi vingine vya Polisi Alisema
kauli aliyotoa Pinda bungeni, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kilwa
Kaskazini, Murtaza Mangungu kuhusu Polisi kutumia nguvu kwa wananchi, ililenga
wanaokaidi kukamatwa na kufikishwa mbele ya sheria na si kupiga na kuua kama
ilivyotafsiriwa na wengi.
“Sijapata taarifa kwa
maandishi juu ya azma ya kumshitaki Waziri Mkuu, lakini Pinda hajavunja sheria
kwa kauli yake aliyotoa,” alisema.
Alisema kwa jinsi alivyosikia maelezo ya Waziri Mkuu
bungeni, kama LHRC wanamshitaki kwa jinai Waziri Mkuu, haoni uhalali wa
mashitaka hayo.
Usahihi wa Pinda Alisema Waziri Mkuu alieleza hatua
zinazochukuliwa dhidi ya mvunja sheria, na kufafanua kuwa Mtanzania yeyote ana
haki kwa mujibu wa sheria, lakini pia ana wajibu, ndiyo maana vipo vyombo na
kila chombo kimepewa mamlaka na wajibu wa kutekeleza.
Alifafanua, kwamba kilichoongelewa ni dhana ya
mkusanyiko ambayo ni haki kwa mujibu wa Katiba, ikiwemo uhuru wa kukutana, kutoa
mawazo na kufanya mawasiliano.
Hata hivyo, alikumbusha kuwa Sheria ya Jeshi la Polisi,
inasema ili mkusanyiko ufanyike, lazima taarifa itolewe kwa kiongozi wa Polisi
wa eneo husika.
Sheria hiyo inasema, kama mkusanyiko una nia ya kutenda
kosa na ikafanyika hivyo, kuna chombo kilichopewa dhamana ya kuhakikisha
mkusanyiko haramu unatawanyika na sheria hiyo inaruhusu Polisi kutawanya
mkusanyiko haramu.
“Unatarajia nini kama kuna
watu wanafanya fujo na polisi wana mamlaka ya kuwakamata waliofanya
fujo?” Alihoji Feleshi na kuongeza kuwa dhana ya matumizi ya nguvu ni
ya kisheria pia.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema,
akizungumza kwa simu na gazeti hili, alisema utaratibu wa Polisi kulazimika
kutumia nguvu upo. Aliutaja utaratibu huo kwamba unatumika hasa katika
mikusanyiko isiyotakiwa, ambapo Polisi hulazimika kutoa tangazo la angalizo mara
kadhaa kutaka watu watawanyike.
“Tangazo linapotolewa, Polisi kwa kutumia kipaza sauti
husema, tawanyikeni, tawanyikeni na kusisitiza hivyo mara kadhaa, hapo
wanaopaswa kutawanyika wakikaidi, nguvu hutumika ingawa inaweza isiwe ya kupiga
risasi, pengine virungu, yote hiyo si
kupiga?
“Risasi ni kitu cha
mwisho, labda uwe unashambuliwa wewe (polisi), hata ikiwa hivyo, ukipiga risasi
kuna maeneo ya kupiga, si kichwani, polisi wana mafunzo ya kupiga maeneo ya
miguuni, hivyo kutumia nguvu kwa polisi kupo,” alisema Jaji
Werema.
Post a Comment