Mwamuzi Anthony Ogwayo mwenye beji ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kutoka Kenya ndiye atakayechezesha mechi kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Burundi (Intamba Mu Rugamba) itakayochezwa keshokutwa (Aprili 26 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ogwayo katika mechi hiyo ya
maadhimisho ya miaka 50 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar,
atasaidiwa na Gilbert Cheruiyot na Oliver Odhiambo wote pia kutoka
Kenya. Mwamuzi wa mezani atakuwa Israel Mujuni wa Tanzania.
Nayo Taifa Stars
inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ipo kambini jijini Dar es
Salaam kujiandaa kwa mechi hiyo ambayo itakuwa ya kwanza tangu kuanza
kwa mpango wa maboresho wa timu hiyo.
Makocha wa timu zote mbili
pamoja na manahodha wao kesho (Aprili 25 mwaka huu) saa 5 asubuhi kwenye
ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) watakuwa na
mkutano na waandishi wa habari kuzungumzia mechi hiyo.
*KOCHA MPYA STARS KUTUA JUMAMOSI
Kocha Mkuu mpya wa Taifa
Stars, Martinus Ignatius Maria maarufu kama Mart Nooij anatarajiwa
kuwasili nchini Jumamosi alfajiri (Aprili 26 mwaka huu) tayari kwa ajili
ya kuanza kazi ya kuinoa timu hiyo.
Nooij (59) atawasili saa 7.20
usiku kwa ndege ya Ethiopia Airlines ambapo anatarajia kukutana na
waandishi wa habari Jumamosi mchana, saa chache kabla ya kuanza mechi ya
kirafiki kati ya Taifa Stars na Burundi itakayochezwa kwenye Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam.
Post a Comment