WAHITIMU 39 wa kidato cha nne mwaka jana katika Shule ya Sekondari
Karobe jijini hapa wakiwa na wazazi wao, jana waliandamana hadi ofisi
za Mkuu wa Mkoa ili kujua hatma yao baada Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi kushindwa kuwapangia nafasi za kujiunga kidato cha tano licha
ya kufanya vizuri katika mitihani yao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti,
wanafunzi hao pamoja na wazazi wao, walisema kuwa waliamua kufika ofisi
za Mkuu wa Mkoa ili kujua hatima yake, baada ya kuona hawapewi majibu
ya kuridhisha kutoka kwa viongozi wa chini yake.
Walisema tangu wizara itangaze majina kwa ajili ya kujiunga kidato
cha tano wiki mbili zilizopita, wameshangazwa kuona wanafunzi kutoka
shule hiyo hawajapangiwa kwa ajili ya kuendelea na masomo katika ngazi
hiyo, licha ya kuwa na ufaulu mzuri.
Wanafunzi hao ambao wamepata alama za daraja la kwanza hadi tatu,
hawajui hatima yao kutokana na wizara husika kushindwa kuwapangia shule
kwa ajili ya kuendelea na masomo ya kidato cha tano.
Nao wazazi ambao waliambatana na watoto wao hadi ofisi ya Mkuu wa
Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi
‘Sugu’ (CHADEMA) kwa nia ya kutafuta suluhu ya suala hilo, walisema
kuwa tangu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kutangaza majina ya
wanafunzi waliofaulu kwa ajili ya kidato cha tano na shule
walizopangiwa, hakuna majina ya watoto wao.
Mmoja wa wazazi hao, Lawrance Shimo, alisema baada ya kufuatilia kwa
kina ikiwemo kuuliza uongozi wa shule, walibaini kuwa katika shule hiyo
hakuna mwanafunzi hata mmoja aliyepangiwa shule kwa ajili ya kuendelea
na kidato cha tano, licha ya kuwa na ufaulu wa alama mzuri.
Na Keneth Ngelesi
Post a Comment