
WATUHUMIWA
wanaodaiwa kumuua Sista Cresencia Kapuli na kumpora Sh milioni 20, jana
wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es
Salaam na kusomewa mashitaka ya wizi wa zaidi ya Sh milioni 479 katika
benki ya Barclays.
Washitakiwa
hao ni Hamis Shabani (34) maarufu kwa jina la Caros na Manasi Genyeka
(35) maarufu kama Mjeshi, walifikishwa mahakamani hapo jana na
kuunganishwa na wenzao wanaokabiliwa na kesi hiyo ya wizi.
Awali
Wakili wa Serikali Mwanaisha Kombakono aliomba mbele ya Hakimu Mkazi
Nyigulila Mwaseba kubadilisha hati ya mashitaka ili aweze kuwaunganisha
washitakiwa hao.(Martha Magessa)
Alidai
kuwa washitakiwa hao na wenzao ambao walikuwa mameneja katika benki hiyo
Alune Kasililika na Neema Batchu, wengine ni Kakamie Julius, Iddy
Khamis, Sezary Massawe, Boniphance Muumba, Ruth Macha, Sajenti Iddy na
Koplo Bundala walikula njama za kutenda kosa.
Aliendelea
kudai kuwa Aprili 15 mwaka huu, washitakiwa hao wakiwa katika benki
hiyo tawi la Kinondoni, Dar es Salaam waliiba fedha hizo.
Ilidaiwa
kuwa kabla ya kufanya wizi huo walitumia silaha kuwatishia Anifa Ahmad
na Anna Tegete ambao ni wafanyakazi wa benki hiyo ili wajipatie fedha
hizo bila pingamizi.
Katika
mashitaka yanayowakabili askari wa Jeshi la Polisi Sajenti Iddy na Koplo
Bundala wanadaiwa Aprili 16 mwaka huu katika eneo la Kijitonyama
waliwasaidia washitakiwa wa wizi wa fedha hizo hizo, baada ya kitendo
kutendeka.
Washitakiwa wote wanadaiwa kuiba Sh milioni 390.22 dola 55, 000 za Kimarekani na Euro 2150 mali ya Barclays.
Baada ya
washitakiwa kusomewa mashitaka yao walikana kutenda kosa hilo na upande
wa Jamhuri ulidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika. Askari hao wako
nje kwa dhamana ya wadhamini wawili waliosaini hati ya Sh milioni 10.
Washitakiwa wengine wapo rumande kwa kuwa mashitaka yanayowakabili hayana dhamana. Kesi itatajwa tena Julai 22 mwaka huu.
CHANZO:HABARILEO
Post a Comment