Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

SOMA TAMKO RASMI LA UMOJA WA VIJANA WAZALENDO WA VYUO VYA ELIMU YA JUU DAR ES SALAAM LA KULAANI KAULI ZA MWENYEKITI WA CHADEMA TAIFA ZA KUHAMASISHA UASI KWA NJIA YA MAANDAMANO



  Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Wazalendo wa Vyuo vya Elimu ya Juu Mkoa wa Dar es Salaam, Mussa Omary (katikati), akizungumza na waandishi wa habari wakati akisoma tamko hilo. Kulia ni Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Theodora Malata na Mwanachuo Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Rehema Akukweti.
 Mwanachuo wa UDSM, Gulatone Masiga akijibu maswali ya waandishi wa habari. Kushoto ni Mwanachuo Mwita Nyarukururu na Mwenyekiti wa umoja huo, Mussa Omary.
  Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Theodora Malata, akichangia jambo wakati wa kujibu maswali ya wanahabari.
 Mwanachuo Mussa Mashamba kutoka Chuo cha Ustawi wa Jamii, akisisitiza jambo wakati akijibu maswali ya wanahabari. Kulia Massoro Kivuga na William Haule.

 Wawakilishi wa wanafunzi wa vyuo vikuu 12 vya Mkoa wa Dar es Salaam wakiwa kwenye mkutano na waandishi wa habari.
 
 Wanahabari wakiwa kwenye mkutano huo.Picha na habari za jamii.com-simu namba 0712-727062
 
*********

 TAMKO RASMI LA UMOJA WA VIJANA WAZALENDO WA VYUO VYA ELIMU YA JUU DAR ES SALAAM LA KULAANI KAULI ZA MWENYEKITI WA CHADEMA TAIFA ZA KUHAMASISHA UASI KWA NJIA YA MAANDAMANO

Sisi ni vijana wasomi wazalendo kutoka vyuo vikuu mbalimbali vilivyoko Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM); Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU); Dar es Salaam University College of Education (DUCE); USTAWI WA JAMII; Chuo Kikuu cha Mtakatifu John (St. John); Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM); Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT); Kampala International University (KIU); Dar es Salaam Institute of Technology (DIT); Institute of Adult Education (IAE); Tanzania School of Journalism (TSJ); College of Business Education (CBE), Chuo cha Uhasibu (TIA) na Chuo cha kumbukumbu ya Mwl JK Nyerere.

Tunachukua fursa hii kulaani vikali kauli zilizotolewa na Mh. Freeman Mbowe ambae ni Mwenyekiti wa CHADEMA ya kutaka kuitisha maandamano ya nchi nzima bila kikomo pamoja na kuhamasisha asasi nyingine za kiraia kufanya na kuratibu maandamano kama hayo ya CHADEMA kwa ajili tu ya kupinga kuendelea kwa Bunge Maalumu la Katiba.

Tunawaambia watanzania wenzetu kuwa tumekerwa na kusononeshwa sana na kauli ya kibabe ya kiongozi huyu wa CHADEMA ya kuhamasisha vurugu ambazo tumezishuhudia zikisambaratisha umoja wa nchi nyingi na kuwa chanzo cha vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo huwa haviishi na hatimaye kuendelea kulipakazia Bara la Afrika kuwa halijastaarabika na siasa za kidemokrasia.

Tulimsikia akiahidi maandamano bila kikomo kwa kibali cha polisi au bila kibali cha polisi mbele ya wajumbe ambao wengine sio watanzania. Ndugu watanzania wenzetu, kauli kama hii haiwezi kusemwa hata na Rais yeyote ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu anaeongoza kwa kufuata misingi ya sheria na utawala bora, je Mh. Mbowe anapata wapi uhalali na ujasiri huo? Maana Rais na Amiri Jeshi Mkuu ambae ni dikteta anaweza kusema lakini yule anaetawala kwa misingi ya sheria, katiba na utawala bora kamwe hawezi kusema kauli kama hizo. Maneno aliyoyasema Mh. Mbowe amejivalisha madaraka zaidi hata ya yale ya Rais wetu ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama. Lakini kwa mtazamo wetu ni kuwa Mh. Mbowe amejivalisha UDIKTETA ambao unatakiwa kulaaniwa na kila mtanzania aliyeko ndani na nje ya nchi hii. Uzito wa kauli zake haubebeki na mtu yeyote kwenye taifa hili. Hatuna shaka kuwa ametoa kauli mbaya sana kuliko zote za kisiasa ambazo zimewahi kusemwa majukwaani. 
Watanzania kwa ujumla wetu na makundi yetu tukikaa kimya bila ya kuzilaani na kuzikemea vikali kauli zake, tutakuwa hatujitendei haki sisi wenyewe na pia hatutavitendea haki vizazi vijavyo vya nchi yetu.

Ndugu zetu watanzania, kama ambavyo yeye mwenyewe alisema kabla ya kutoa amri kwa watu kuandamana kuwa anaamini watanzania wapo tayari kufanya mageuzi ili chama chake kingie IKULU ya Magogoni. Hayo yatafanikiwa endapo tu vijana wataacha uoga, maneno ambayo yanaashiria kutaka kuchukua uongozi kwa nguvu bila kufuata misingi ya kidemokrasia inayosimamiwa na serikali iliyo madarakani.

Sisi umoja wa vijana wazalendo wa vyuo vya elimu ya juu Dar es Salaam tunasema kuwa uzito na ubaya wa kauli hizi unaonesha wazi kuwa Mh. Freeman Mbowe hafai kupewa dhamana ya kuwa Rais wa nchi na Amiri Jeshi Mkuu wa vikosi vya ulinzi na usalama na pia amedhihirisha kuwa CHADEMA haina sifa ya kuiongoza nchi hii kwa sasa kwa kufuata misingi ya demokrasia na kudumisha amani, utulivu na mshikamano wa watanzania kwa lengo la kudumisha umoja, na muungano wetu.

Tunaomba watanzania mkumbuke na mtilie maanani kuwa, Mh. Freeman Mbowe katoa kauli hizi akiwa raia tu wa kawaida. Je itakuwaje akiwa Rais wa nchi na Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vyetu vya Ulinzi na Usalama wa nchi hii? Kwa maoni yetu ni kuwa kwa upeo na mtazamo wa akili yake hakuna atakaebaki salama ndani ya nchi hii kwa kuwa atatuingiza kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe na pia atatuingiza kwenye vita na nchi majirani. Hafai, hafai, hafai hata mara moja kuwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu. Ndugu watanzaia, hivi ni mtu gani anaeweza kuishi kwa amani na viongozi kama Mbowe na wenzake wanaotumia ubabe kwenye maisha ya kawaida ya kila siku? Na hapa ndipo wanatuthibitishia kuwa Mh. Freeman Mbowe na Kikundi cha viongozi wa chama chake wote karibu wameshindwa kuzichunga na kuziweka pamoja familia zao na hatimaye zimesambaratika kwa ubabe huo huo, hivyo hawataweza kutuongoza na kutuweka pamoja watanzania ili tuishi kwa amani.

Ndugu watanzania wenzetu tumebaini kuwa Mh. Freeman Mbowe na viongozi wenzake wa CHADEMA wanatumia maandamano na damu za watanzania kutafuta fedha kwa wafadhili wao ambao hawaitakii mema nchi yetu. Wakiaandaa maandamano, wanapiga picha na kuwapelekea wafadhili wao, wanapata fedha, wanajenga majumba na kununua magari ya kifahari na kusafiri ulaya, marekani na familia zisizo rasmi kwa kujificha kwenye pazia la DEMOKRASIA huku watanzania wakiendelea kuathirika na maandamano. Hapo ndugu watanzania hakuna DEMOKRASIA bali tunaona DOMO-KRASIA na BONGO-KRASIA, yaani wanatumia ulimi na akili ndogo za kitoto kujinufaisha na familia zisizo rasmi kwa siasa za ulaghai, ghilba, fitina, majungu, choyo, chuki, usanii wa kisiasa na uhaini alioutangaza Mh. Mbowe.

Ndugu zetu watanzania, fahamuni kuwa Mh. Freeman Mbowe, Dk. Wilbroad Slaa, Tundu Lissu, Godless Lema, Mchungaji Peter Msigwa, Hezekiah Wenje na wengine wana familia. Swali je mmeshawahi kuwaona wake, watoto, na ndugu zao wa karibu kwenye maandamano yoyote yale waliyowahi kuyaandaa? Siku zote huwaambia watu wao hao bakini majumbani mtadhurika. Pale damu za watanzania zinapomwagika kwenye maandamano baadae huwa wanajifungia na kushangilia ushindi mkubwa wa kuvuna mabilioni ya fedha za kigeni, kwa kuwa huwa wanapiga picha matukio hayo na kwenda kuonesha wafadhili wao kwa taswira kwamba demokrasia inanyanyaswa. Wanakinga mabilioni ya fedha za kigeni wanatia kwenye akaunti zao, wanagawana, na mambo yao yanaenda sawasawa, huku watanzania wengine wakiwa wana vilio vya kupoteza ndugu na baba zao, waume, wake, wapenzi/wachumba, na watoto wao na kadhalika. Swali kwa nini hawaoni umuhimu wa kujali utu, ubinadamu na uhai wa watanzania wengine? 

Sisi umoja wa vijana wazalendo wa vyuo vya elimu ya juu Dar es Salaam tunapenda kuwahakikishia kuwa thamani ya maisha ya watanzania wote au hata kwa mtanzania mmoja ni kubwa sana kuliko hiyo katiba mpya wanayoidai.

Tunawaomba watanzania wenzetu msikubali kufanywa kama mbuzi wa kafara na watu wenye tamaa, pupa, ulevi, na uroho wa madaraka kama hawa akina Mbowe na kundi lake. Tusijiendee tu kama kuku aliekatwa kichwa halafu akaachiwa atembee, na tusishikiwe akili zetu kama za mbayuwayu kwani “Akili za Kushikiwa, ongeza na zako”. Tuwakataeni wanasiasa uchwara waliofilisika kihoja na kutaka kuwatumia ili kujinufaisha. Wanataka kutupeleka wapi? Ni dhambi isiyosameheka kulitumbukiza taifa hili katika machafuko yenye majuto makubwa kama ya Misri, Syria, Afrika ya kati, Libya, Sudan ya Kusini na kwingineko. Tusikubali watupeleke huko, waacheni waende wenyewe kama wanaweza. kwani nchi yetu ina mgogoro wa kisiasa?!!!!! Waulizeni wanataka nini?

Ndugu watanzania wenzetu, tunaomba mjue kwenye nchi hizo hizo zenye demokrasia pevu watu wa aina ya Mh. Freeman Mbowe (hasa kwa kauli zake alizozitoa juzi tarehe 14.09.2014) wanaotaka kuvuruga na kuvunja misingi mikuu ya utaifa wao (core values) kama vile amani, usalama na umoja huwa hawavumiliwi hata kidogo.

Sisi umoja wa vijana wazalendo wa vyuo vya elimu ya juu Dar es Salaam tunaviomba vyombo vyetu vya dola visizivumilie kauli kama hizi zilizotolewa na Mh. Freeman Mbowe hata mara moja. Kwani vyombo vya dola vina dhamana ya kulinda, kutunza na kuendeleza amani na utulivu wa nchi yetu. Umoja wetu, kwa heshima na taadhima kubwa, tunaviomba vyombo hivi kumchukulia hatua kali za kisheria Mh. Mbowe kwa kauli hii ya kutishia uvunjifu wa amani kabla hajaiingiza nchi yetu kwenye machafuko ya kisiasa.

Sisi umoja wa vijana wazalendo wa vyuo vya elimu ya juu Dar es Salaam hatutaki kuona vijana wenzetu na watanzania wote kwa ujumla wakiathirika kwa ujinga huo wa maandamano yanayofanywa mradi wa kutafuta fedha. Kwani maandamano hayo yatawaathiri wana vyuo wa Dar es Salaam pamoja na kuathiri shughuli nyingine za kiuchumi, na kijamii za wananchi wa kawaida. Kwa nini shughuli zetu na za wananchi zisimame kwa sababu tu ya machafuko ili Mh. Mbowe apate picha za kwenda kuuza huko kwa wafadhili wao? Sisi umoja wa vijana wazalendo wa vyuo vya elimu ya juu Dar es Salaam tulisikiliza na kutazama hotuba ile kwa umakini wa hali ya juu, tunapenda kuwathibitishia kuwa hotuba ile haikuwa ya kisomi, ilikuwa haijengi chama chake wala ilikuwa haijengi nchi yetu isipokuwa ilikuwa ya kibabe, ilikuwa ya kejeli, ilikuwa ya kichochezi iliyolenga kuvunja misingi ya amani na utulivu wa nchi yetu. Ni matumaini yetu kuwa hata kwa mwanafunzi wa shule ya msingi hawezi kujifunza kitu chochote cha maana kutoka kwenye hotuba ile. Hotuba ya Mh. Mbowe haiwezi kutusaidia kujenga taifa lenye dira kwa vizazi vijavyo.

Mwisho, Sisi kama umoja wa vijana wazalendo wa vyuo vya elimu ya juu Dar es Salaam, tunawataka watanzania wenzetu mzipime na kuzitafakari kwa makini kauli za Mh. Mbowe, na kujiuliza je anafaa kuwa kiongozi wa nchi hii?

Asanteni kwa kutusikiliza,

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika
Imesomwa na Mussa Omari, 

Mwanafunzi OUT, 
kwa niaba ya umoja wa vijana wazalendo wa Vyuo vya elimu ya juu

Dar es Salaam
Tarehe 17.09.2014 

Sahihi
……………………….

Simu 0715632681
 
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top