Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe.
Mabehewa
hayo ni kati ya 25 aina ya Ballist Hopper Bogie (BHB) yaliyoingizwa
nchini Julai 24 yakiwa yamegharimu kiasi cha Sh4 bilioni na 20
yalibainika kuwa ni mabovu na kulazimika kuanza kutengenezwa kwa
kificho.
Mkataba
wa kununua mabehewa hayo ulisainiwa Machi 21, 2013 kati ya TRL na
Kampuni ya Hindusthan Engineering and Industries ya India.
Jana,
Dk Mwakyembe aliiagiza Bodi ya Wakurugenzi ya TRL kuwasimamisha kazi
mara moja kupisha uchunguzi, wahandisi wote waliokwenda India kwa ajili
ya kufanya uhakiki wa ubora wa mabehewa hayo.
Alitoa
maagizo hayo mbele ya Menejimenti ya TRL na wafanyakazi wa kampuni
hiyo, katika kikao cha kuhitimisha mchakato wa kushughulikia malalamiko
ya watumishi ambao wamekuwa wakidai malipo ya kima cha chini cha
mshahara cha Sh300,000.
“Natoa
siku 10 Bodi ya Wakurugenzi iwe imenipa majibu ya mchakato mzima wa
ununuzi wa mabehewa 25 ya kokoto ulivyofanywa. Nataka uchunguzi ufanyike
lakini wale wote waliokwenda India mara mbili kwa ajili ya kuthibitisha
ubora wa mabehewa hayo wasimamishwe kazi mpaka taarifa za wasio na
hatia zitakapobainika,” alisema.
Aliagiza
kusimamishwa kazi kwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TRL na kuondolewa katika
nafasi yake, mkuu wa idara ya fedha pamoja na kuvunjwa kwa bodi ya
zabuni ya kampuni hiyo na kusitishwa kwa mikataba yote iliyopo kati
kampuni hiyo na wazabuni.
Mikataba
aliyoagiza kusitishwa ni pamoja na ule wa TRL na Kampuni ya Transroads
inayoshughulikia upakiaji wa mizigo na kampuni ya R&A inayotekeleza
ukarabati wa reli pamoja na urekebishaji wa mfumo wa mawasiliano huku
akitaka kuondolewa kwa mzabuni anayehudumu katika Shule ya Msingi Itigi.
“Nataka
bodi iende Itigi na iniambie imemchukulia hatua gani msimamizi wa mradi
huu ambao mkataba wake unaonyesha kuwa chakula kinatolewa shuleni hapo
lakini si kweli. Huwa naongea nikiwa natabasamu lakini ikibidi
nitaiondoa bodi hii. Kuna Watanzania wengi wanaweza kufanya kazi hii,
kama kuna mtu anaona hawezi basi aache mara moja.”
Alisema
ripoti aliyonayo inaonyesha kuwa kati ya vitanda 320 vinavyoelezwa
kuwapo katika shule hiyo, 260 ni vibovu huku magodoro yakiwa hayafai kwa
matumizi ya binadamu.
Mgomo
Wafanyakazi
wa TRL chini ya chama chao (Trawu) walianza mgomo wa kutaka majibu juu
ya ongezeko la mishahara yao pamoja na malipo ya malimbikizo ya kati ya
Julai na Oktoba mwaka huu na baada ya kutoelewana na uongozi,
walilifikisha suala hilo wizarani.
Waziri Mwakyembe aliunda kamati ya uchunguzi iliyofanya kazi kwa wiki tatu ambayo ilikabidhiwa kwake Jumatatu iliyopita.
Taarifa
za awali zilionyesha kuwa ili kufanikisha madai ya mishahara hiyo
zilikuwa zinahitajika Sh400 milioni lakini baada ya uchambuzi imebainika
kuwa kiasi cha fedha kinachotakiwa ni Sh120 milioni.
“Nimesikia
mkuu wa idara ya fedha (Jasper Kisiraga) hajawaingizia mishahara yenu
kwa madai kwamba ana hasira baada ya ninyi kufikisha malalamiko yenu
kwangu. Naiagiza bodi kumwondoa mara moja katika nafasi hiyo,” alisema
Dk Mwakyembe na kuongeza:
“Nafasi
yake ichukuliwe na kijana aliyekuwemo katika kamati ya uchunguzi
(Mbaraka Mchopa). Nadhani bodi haitaniangusha kumthibitisha kijana huyu
ambaye ameonyesha nia ya dhati ya kushughulikia matatizo ya kampuni.”
Alimwagiza
Mchopa kuhakikisha kuwa madereva wote wanalipwa posho wanazostahili kwa
wakati na yeyote atakayeonyesha jitihada kwa kufanya kazi ya ziada
yenye mchango kwa maendeleo ya kampuni.
Pia
Dk Mwakyembe alitangaza kusitisha mikataba yote kati ya TRL na kampuni
tatu za ulinzi akisema hazina uwezo wala nyenzo... “Zinalinda mali ya
mabilioni ya shilingi kwa manati, hazina silaha yoyote kukabiliana na
chochote kinachoweza kutokea. Mikataba yote ivunjwe mara moja na
uanzishwe utaratibu wa kuajiri askari wetu kwa kushirikiana na Jeshi la
Polisi.”
Alimtambulisha
kamanda mpya wa polisi (kikosi cha reli), Simon Chillery, akimtaka
kuhakikisha magenge ya wahalifu katika baadhi ya maeneo kama Nguruka,
Kigoma na Mabamba, Tabora yanaondolewa mara moja.
“Huyu
jamaa ni msomi. Ni mhandisi kwa taaluma, nataka ukisuke kikosi chako
kwa namna itakayoonyesha tofauti kati ya kamanda msomi na ambaye
hajaenda shule, ukishindwa mimi mwenyewe nitakushtaki kwa IGP,” alisema.
Mwakyembe
alisema Serikali imegundua uwepo udanganyifu unaofanywa na baadhi ya
wafanyakazi. “Nitakuja tena wiki ijayo kuwafukuza kazi baadhi yenu
kutokana na wizi wa mafuta pamoja na udanganyifu wa upakiaji wa mizigo
walioufanya. Nasikia kati yao wengine wanaendesha biashara ya daladala,
nitazifuatilia na zikikamatwa zitataifishwa.”
Mabehewa mapya
Mapema
jana asubuhi, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alitembelea Bandari ya Dar es
Salaam na kukagua mabehewa 72 yakiwamo 22 ya abiria na 50 ya mizigo
ambayo yameingizwa nchini kwa ajili ya kuimarisha usafirishaji katika
reli ya kati.
“Hii
ni moja juhudi za Serikali kuboresha miundombinu ya usafiri nchini na
changamoto iliyopo ni kufikia viwango vya kimataifa. Kama nchi nyingine
wana treni za umeme sisi kinatushinda nini kufika huko? Nikutie moyo
waziri na tuendelee kushirikiana katika hili… nitajitahidi kushughulikia
masuala yote yahusuyo fedha,” alisema Pinda.
chanzo: gazeti la mwananchi
chanzo: gazeti la mwananchi
Post a Comment