Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Maendeleo na Mageuzi ya Ukaguzi na Kazi za Kamati ya Hesabu Za Serikali (PAC)


  Zitto Kabwe, Mb-Mwenyekiti wa PAC, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
---
  KAMATI YA HESABU ZA SERIKALI (PAC) NA JAMII

Zitto Kabwe, Mb
Mwenyekiti wa PAC, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Utangulizi

Baraza la Wawakilishi kama chombo cha kikatiba cha Kuisimamia na Kuishauri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar limepewa haki na Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984 ya kujiunda katika Kamati mbalimbali (Ibara ya 85 ya Katiba ya Zanzibar). Kamati ya PAC ndio haswa Kamati ya Usimamizi (oversight) wa Serikali na hivyo kuifanya kuwa Kamati muhimu kuliko Kamati nyingine zote za Baraza. Wakati Kamati nyingine za Baraza na Baraza kwa ujumla wake hutimiza wajibu wake kwa mujibu wa Ibara ya 88 ya Katiba ya Zanzibar, Kamati ya Hesabu za Serikali husimamia matumizi yote ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyoidhinishwa na Baraza na kutoa Taarifa yake kwa Umma. 
 
Kwa hiyo Kamati hii inapaswa kuwezeshwa na kujipambanua vilivyo katika kutekeleza majukumu yake. Ni muhimu kusisitiza kuwa Kamati nyingine za Baraza ni muhimu pia katika kusimamia utekelezaji wa Sheria zilizotungwa na Baraza la Wawakilishi (oversight over execution of laws by ministries and agencies).

Ukaguzi na Kamati

Baraza la Wawakilishi katika mkutano wake wa kila mwaka wa Bajeti hupitisha mpango wa mapato na matumizi ya Serikali ya Zanzibar. Baada ya makusanyo ya Mapato hayo na kugawanywa kwa kila Wizara hutumiwa kwa malipo ya Mjadala katika Semina ya Kamati ya PAC Zanzibar iliyofanyika katika Hotel yaSeaCliff tarehe 6 Disemba 2014.
 
 huduma, mishahara na miradi ya maendeleo. Mara baada ya kufungwa kwa mahesabu, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali hukagua na kuwasilisha Taarifa yake kwa Baraza la Wawakilishi. Kamati ya PAC sasa huchukua Taarifa hiyo na kuwahoji kila Katibu Mkuu wa Wizara kuhusu hoja za ukaguzi. Baada ya kukamilisha Taarifa yake PAC huwasilisha Taarifa hiyokwenye Baraza kwa mjadala na kupitisha Maazimio.

Hivyo Ripoti ya CAG ndio nyenzo kuu ya Baraza katika kusimamia fedha za Umma. Hata hivyo pale ambapo PAC huona inafaa, huweza kuagiza ukaguzi maalumu kwenye maeneo mahususi. Siku zilizopita nyenzo hii ya ukaguzi maalumu ilikuwa haitumiki sana. Kutumika kwake hivi sasa ni moja ya maendeleo ya kiusimamizi katika PAC. Huko Tanzania bara njia hii imekuwa ikitumika sana hivi sasa na kupitia njia hiyo mambo mengi yameibuliwa kuhusu matumizi ya fedha za umma.

CAG anatazama mambo mengi kwa wakati mmoja na ndani ya mwaka mmoja. Hivyo kuna nyakati mkaguzi anakuwa haoni masuala Fulani Fulani mpaka anapoombwa na vyombo vingine na hata wananchi. Ni vema Kamati ya PAC Zanzibar kutumia pia njia hii ili kuimarisha usimamizi bora wa fedha za Umma katika Nchi ya Zanzibar kama ilivyo sasa katika Jamhuri ya Muungano.

Ni muhimu sana kuzingatia kwamba Wawakilishi ndio chombo za mwisho cha maamuzi kuhusu masuala ya wananchi wa Zanzibar ikiwemo matumizi ya fedha za umma. Kwa hiyo ni wajibu wa PAC kuhakikisha kuwa Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali inafikishwa Barazani, inajadiliwa na kuamuliwa. Muhimu zaidi kuhakikisha kuwa Wizara ya Fedha ya Zanzibar inajibu hoja za PAC ( treasury notes) na hapo ndipo mzunguko wa uwajibikaji unakuwa umekamilika (accountability loop). Hata katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wakati mwingine ‘treasury notes’ hazipewi msukumo wa kutosha na Wabunge na hivyo kujikuta masuala mengi yanabaki yanaelea bila kumalizwa na kufanya mfumo wa Uwajibikaji kuwa dhaifu.

Mageuzi muhimu kufanyika Wakaguzi wa Mahesabu wana chombo chao cha Kimataifa ambacho kinatoa
miongozo ya mara kwa mara kuhusu masuala ya ukaguzi ( International Accounting Standards). Hii huwafanya kuleta mabadiliko ya mara kwa mara katika taaluma yao na kuboresha utendaji wa kazi zao. Siku hizi ukaguzi wa thamani ya fedha (value for money) hufanywa ili kugundua kama kweli fedha iliyotumika inaendana na huduma iliyotolewa. Kwa mfano, kama barabara imejengwa kwa tshs 50 bilioni, wakaguzi sasa wanaweza kuona kama kweli barabara hiyo ina thamani tajwa.

Kamati ya PAC pia huweza kutembelea miradi kujiridhisha kama taarifa ya mkaguzi inakubaliana na mradi uliopo. Hata hivyo, Wawakilishi kama ilivyo Wabunge wanaweza wasiwe na taaluma husika katika jambo linalofanyiwa ufuatiliaji wa thamani ya fedha. Ni muhimu basi kuwa na mahusiano ya karibu kati ya CAG na PAC ili lugha ya kikaguzi kuwa ni lugha inayoeleweka kwa Wawakilishi.

Wawakilishi wanapaswa kuendana na mageuzi ya mara kwa mara katika ukaguzi na usimamizi wa fedha. Kwa mfano, badala ya kusubiri Taarifa ya mwaka ya CAG ndio wafanye kazi, PAC yaweza kuona ni jambo gani katika jamii ambalo linalalamikiwa na wananchi kwamba kuna matumizi mabaya na kuagiza ukaguzi maalumu katika eneo hilo. Katika Bunge la Jamhuri ya Muungano mijadala mingi Bungeni yenye hoja kali kali zenye kuleta mabadiliko makubwa imetokana na ukaguzi maalumu. Hii hoja iliyomalizika katika Mkutano wa Bunge wa 16 na 17 ( Tegeta Escrow ) ilitokana na habari ya Gazeti la kila siku la The Citizen. Kutokana na uzito wa hoja hiyo PAC iliagiza ukaguzi maalumu na hatimaye kuwasilishwa Bungeni.

Mwezi Februari katika Taarifa ya mwaka ya PAC moja ya taarifa itakayowasilishwa inahusu ukaguzi maalumu kuhusu mchakato wa ubinafsishaji wa Benki ya Taifa ya Biashara mwaka 2000 na mapitio ya mkataba wa uendeshaji wa Benki hiyo kati ya mwekazaji kama mwanahisa mmoja na Serikali
kama mwanahisa mwingine.

Mageuzi muhimu sana kufanyika ni hayo, PAC Zanzibar itoke katika kutegemea tu Taarifa ya mwaka ya CAG na ijielekeze pia katika masuala yanayozungumzwa na Jamii kuhusu matumizi ya Fedha za Umma.

Eneo lingine la kusisitiza katika mageuzi ni eneo la itikadi za vyama. Iwapo PAC ikifanya kazi kwa kuegemea itikadi za vyama za wajumbe, kazi ya usimamizi wa Serikali haitafanyika. Ni vigumu kwa wajumbe kusahau vyama vilivyowaingiza barazani, lakini ni muhimu wajumbe kufahamu kuwa utendaji mbovu wa Serikali
unaathiri wananchi wote bila kujali itikadi. Kazi za PAC zinakuwa na ufanisi mkubwa pale ambapo wajumbe wake wanaweka mbele maslahi ya Taifa.

Kwenye Nchi za Jumuiya ya Madola PAC hufanya ‘postmorterm’. Kwamba jambo limekwisha fanywa ndio ukaguzi unafanyika na mjadala kufuata. Kuna haja ya kutazama upya mfumo huu kwani mara nyingi hausaidii. Ni wakati wa kufikiria namna ambavyo CAG na PAC wanaweza kutimiza wajibu katika kuzuia matumizi yanayoelekea kutokuwa na ufanisi. Nchini Ujerumani PAC ni sehemu ya Kamati ya Bunge ya Bajeti, hivyo inashiriki katika kupitisha Bajeti na kusimamia utekelezaji wa Bajeti. Pale ambapo PAC inaona kuwa Wizara Fulani katika mwaka uliotangulia imepata hoja ya ukaguzi katika eneo Fulani, inaweza kuzuia Bajeti ya ‘item’ hiyo mpaka CAG aridhie majibu ya hoja ya ukaguzi. Iwapo Zanzibar itaridhia mfumo kama huu fedha nyingi za Umma zaweza kuokolewa na Jamhuri ya Muungano yaweza kujifunza baada ya kuona matunda yake Zanzibar.

Hitimisho

Usimamizi ya Fedha za Umma ni jukumu endelevu. Kamati ya PAC inapaswa kukua kwa kujifunza ukuaji wa sekta ya ukaguzi na vile vile kuangalia malalamiko ya wananchi. Mageuzi yaliyoainishwa hapo juu ni sehemu tu ya maeneo ambayo PAC inaweza kutafakari na kufanyia kazi ili kuboresha wajibu
wake.
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top