Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Othman Chande akitoa ufafanuzi kwa wanabari
(hawapo pichani) kuhusu uandishi bora wa habari za Mahakama wakati wa
ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa Habari za Mahakama
leo jijini Dar es salaam.
Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Othman Chande (kushoto) na Meneja wa Maadili wa
Baraza la Habari Tanzania (MCT) Allan Lawa (kulia) wakifuatilia mada
mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa wakati wa mafunzo ya kuwajengea
uwezo waandishi wa habari za Mahakama yaliyoandaliwa na Mahakama ya
Tanzania leo jijini Dar es salaam.
Rais
wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) Jaji Mstaafu Thomas Mihayo akitoa
ufafanuzi kwa waandishi wa Habari namna wanavyoweza kuandika habari za
Mahakama kwa kuzingatia weledi wa taaluma zao.
Washiriki
wa mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa Habari za Mahakama wakiwa
katika picha ya pamoja na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Othman Chande leo
jijini Dar es salaam.
Baadhi
ya wanahabari wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa
wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa Habari za Mahakama
leo jijini Dar es salaam.
Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
Waandishi
wa habari nchini wametakiwa kuzingatia weledi wa taaluma zao
wanapoandika habari za Mahakama ili kuepuka kuandika habari zinazowatia
hatiani watuhumiwa na kushindwa kutofautisha kati ya mshitakiwa na
mtuhumiwa pamoja na haki zake.
Akifungua
mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa Habari za Mahakama leo jijini
Dar es Salaam, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Othman Chande amesema
waandishi wa habari wanalojukumu la kuwapatia wananchi taarifa sahihi
kuhusu masuala yanayowahusu na kuepuka uandishi wa habari zenye
kuhukumu.
Amesema
kisheria mtuhumiwa huwa hana hatia mpaka itakapothibitishwa na
mahakama kuwa ametenda kosa na kuongeza kuwa kukosekana kwa weledi
katika uandishi wa habari za mahakama huleta mkanganyiko miongoni mwa
jamii kuhusu ukweli na kuondoa imani ya watu kwa mahakama.
Ameongeza
kuwa baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa Vikitoa habari zisizo mpatia
mtu fursa na haki ya kujibu tuhuma huku vingine vikitoa taarifa
nusunusu na kushindwa kuwa na mwendelezo wa habari za mashauri
mbalimbali mahakamani.
Mhe.Chande
ameeleza kuwa waandishi wamejikita katika uandishi wa taarifa zenye
mvuto kwa jamii na kusahau nyingine walizo anza nazo jambo
linalosababisha wananchi kuachwa njia panda bila kupata taarifa za
kina kuhusu mwisho wa mambo yanayoanzishwa.
"
Mimi sitaki kuingilia utendaji wa kazi zenu za kila siku ila nachotaka
kusema ni kuweka msisitizo wa utoaji wa habari za mashauri mbalimbali
mnayoanza kuyaripoti kwa mwendelezo ili msiwachanganye wananchi"
Amesisitiza.
Amewataka
waandishi wa habari kuandika habari sahihi na kuepuka upendeleo na
maslahi binafsi ili kulinda taaluma na imani katika jamii juu ya
utendaji wa vyombo vya habari.
Mhe.
Chande ametoa wito kwa waandishi wa habari kuepuka uandishi wa habari
zilizojaa chuki zinazoweza kuleta mgawanyiko katika jamii na kusisitiza
habari za kuisaidia jamii kukabiliana na changamoto mbalimbali.
Kuhusu
Mahakama amesema itaendelea kuboresha huduma na miundombinu yake katika
maeneo yasiyofikiwa ili kuendelea kutoa haki kwa wakati pia
kushirikiana na waandishi wa habari wa ndani ili kuimarisha utendaji
wao.
Aidha amevipongeza vyombo vya habari kwa ukomavu viliouonyesha wakati wa utoaji wa taarifa za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Kwa
upande wake Rais wa Baraza la Habari Tanzania Mhe. Jaji Mstaafu
Mhe.Thomas Mihayo akizungumza kwa niaba ya Baraza hilo ametoa wito kwa
waandishi wa habari kuzingatia weledi katika uandishi wa habari za
mahakama ili kuepusha madhara katika jamii.
Amewataka waandishi kujikita zaidi katika uandishi wa habari zenye uhakika kuliko kuwa na taarifa zenye mlengo wa kuuza gazeti.
Amesema
kuwepo kwa mafunzo hayo ambayo yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania ni
ishara nzuri ya uboreshaji wa taaluma ya habari hasa uongezaji wa
ushirikiano katika kutekeleza majukumu ya kimahakama hapa nchini.
Amewataka
wanahabari kujifunza na kufuatilia miongozo na kufuatilia taarifa
mbalimbali zinazoweza kuboresha uandishi wao kwa kupata maneno sahihi ya
kimahakama.Amesema Semina hiyo itawasaidia waandishi wa habari kujenga
weledi katika uandishi wa habari za mahakama.
Ametoa
tahadhari kwa waandishi kuepuka uandishi wa habari zenye uchochezi ili
kuepuka kushtakiwa na jamii, kuepuka lugha za kishabiki na upendeleo.
Naye
Meneja wa Maadili wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) Allan Lawa
akizungumza kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo amewataka kuepuka
kuandika habari zinaonyesha upendeleo na kubainisha kuwa kuwa ipo haja
kwa vyombo vya habari kutenga maeneo madawati ya habari hizo
Post a Comment