Serikali
imewataka wachambuaji na wasambazaji wa mbegu za pamba kuacha
kuwasambazia wakulima mbegu zilizozalishwa katika maeneo yaliyobainika
kuwa na ugonjwa wa mnyauko fusari (Fusarium Wilt Disease). Kauli hiyo
imetolewa leo na Mkurugenzi wa Huduma za Usimamizi, Bodi ya Pamba
Tanzania, Bwana James Shimbe.
Katika
taarifa yake kwa vyombo vya habari, Bwana Shimbe amesema, ugonjwa wa
mnyauko fusari unaweza kudhibitiwa ikiwa wakulima wa pamba watatumia
mbegu bora kutoka kwa wasambazaji wanaotambulika na Bodi ya Pamba
Tanzania.
Akizungumzia
tatizo la kuenea kwa ugonjwa huo Bwana Shimbe amesema kwa kiasi fulani
limetokana na baadhi ya wachambuaji wasio waaminifu kuendelea kusambaza
mbegu za pamba za kupanda ambazo zinaweza kuwa zimetoka katika maeneo
yaliyobainika kuwa na ugonjwa wa mnyauko fusari.
“Tulishatoa
maelekezo kwa kuwataka wasambazaji wa mbegu za pamba za kupanda
kutosambaza mbegu zilizozalishwa katika maeneo yenye ugonjwa.”
Hivyo
tunaendelea kusisitiza kuwa wakulima wawe makini wanapo nunua mbegu
kutoka kwa wasambazaji wasiotambulika na watoe taarifa haraka kwa Bodi
wanapoona mbegu hizo hazioti ili hatua za haraka zichukuliwe za kupeleka
mbegu zingine mbadala ili kuendana na msimu wa kilimo.
Aidha,
Bwana Shimbe amewataka wachambuaji wa pamba ambao ndio wasambazaji wa
mbegu kuacha mara moja kuwasambazia wakulima mbegu ambazo zimetoka
kwenye maeneo yaliyobainika kuwa na ugonjwa na badala yake mbegu za
pamba hizo zisindikwe kuzalisha mafuta ya kula kama walivyokuwa
wameelekezwa na Bodi hapo awali.
“ Bodi
ilishatoa maelekezo kwa wachambuaji wote wa pamba kote nchini, kutenga
mbegu za pamba za kupanda msimu huu wa kilimo kutoka maeneo yaliyo
salama kwa kuziwekea lebo ili kuzitofautisha na zile zinazotoka kwenye
maeneo yaliyobainika kuwa na ugonjwa, ambapo zile zinazotoka katika
maeneo yenye ugonjwa zisitumike kama mbegu za kupanda, bali zisindikwe
kupata mafuta ya kula kama sehemu ya kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa, na
zile mbegu ambazo zimetoka kwenye maeneo yasiyo na ugonjwa zisambazwe
kwa wakulima kwa ajili ya kupanda kwenye mashamba yao baada ya kufanyiwa
majaribio ya uotaji (seed germination test) na taasisi inayohusika na
udhibiti wa ubora wa mbegu (TOSCI)”
Aidha,
mbegu zinazofaa kutumika kwa sasa ni UKM08 iliyofanyiwa utafiti na
Kituo chetu cha Utafiti cha Ukiriguru, ambayo ubora wake umethibitishwa
na Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu (TOSCI) na inauwezo wa kuhimili
magonjwa pamoja na uzalishaji wenye tija zaidi. Mbegu hiyo itakuwa
inaiondoa kwenye uzalishaji ile ya zamani ya UK 91 ambayo imepungua
ubora wake. Katika msimu huu wa kilimo wa 2015/16 Mbegu ya UKM08
itaendelea kuzalishwa kwa wingi (seed multiplication) katika maeneo
salama yasiyo na ugojwa wa mnyauko fusari katika mkoa wote wa Singida na
wilaya ya Nzega na Igunga, mkoa wa Tabora.
Bwana
Shimbe ametoa wito kwa wakulima na wadau wote wa pamba nchini kufuata
kanuni za kilimo bora cha pamba ikiwa ni pamoja na kutumia mbegu bora za
pamba. Aidha, baadhi ya mawakala wa ununuzi wa pamba mbegu na wakulima
wenye tabia ya kuchanganya pamba mbegu na maji, mchanga, chumvi na
kemikali zingine kama vile “mafuta ya kenge” kwa madai ya kuongeza uzito
kwenye pamba yao waachane na tabia hiyo potofu, kwani kwa kufanya hivyo
kunachangia kuoza kwa kiini cha mbegu na kuharibu ubora wake na hivyo
kusababisha mbegu kutokuota.
Imetolewa:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali
Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika
Kilimo Complex
1 Mtaa wa Kilimo 15471
DAR ES SALAAM
Post a Comment