Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

MAGUFULI ACHARUKA AFRIKA MASHARIKI

Dar es Salaam. Staili ya Rais John Magufuli ya kubana matumizi nchini sasa imepanua wigo baada Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuanza kutekeleza agizo lake kwa kupunguza matumizi.

Sekretarieti hiyo imepunguza matumizi ya uendeshaji katika idadi ya wajumbe wanaogharimiwa na Jumuiya, idadi ya vikao na gharama nyingine.

Wakati bajeti ya EAC kwa mwaka ujao ikipunguzwa, wajumbe wa sekretarieti hiyo wametakiwa kutumia zaidi mawasiliano ya mtandao ya video kuendesha mikutano na vikao vyao ili kuokoa fedha ambazo zingetumika kuwasafirisha maofisa wa Serikali kutoka nchi wanachama.

Miezi miwili iliyopita, Rais Magufuli ambaye sasa ni mwenyekiti wa jumuiya hiyo, alisema uongozi wake utajikita zaidi katika kubana matumizi na kuwaagiza watendaji wakuu kuangalia namna ya kupunguza gharama za uendeshaji, huku akiwakumbusha kuwa nchi wanachama zina wananchi maskini wa kipato.

Aliwataka kutazama upya gharama za vikao vyao, usafiri, pamoja na posho wanazolipwa wanaohudhuria mikutano, sambamba na zile za kuwatumia washauri waelekezi kufanikisha miradi mbalimbali inayotekelezwa na jumuiya.

Katibu Mkuu wa EAC, Dk Liberat Mfumukeko alitangaza utekelezaji huo na kubainisha kuwa wataalamu wasiozidi wawili kutoka kila nchi ndio watagharamiwa na jumuiya hiyo wakati wowote watakapotakiwa kuhudhuria mkutano wa kitaalamu baina ya nchi wanachama, linaandika gazeti la The Daily Nation.

“Idadi hiyo pia haitazidi watumishi watatu wa sekretarieti na mikutano haitapaswa kuendeshwa kwa zaidi ya siku nne,” gazeti hilo linakariri kanuni mpya za jumuiya hiyo.

Akionyesha kuunga mkono matumizi ya teknolojia ya video kuendesha mikutano hiyo, Dk Mfumukeko alikaririwa na gazeti hilo akisema: “Walau asilimia 25 ya mikutano yote itaendeshwa kwa njia ya video na iliyosalia itafanyika kwenye kumbi za bure za Serikali husika ili kupunguza gharama.”

Taarifa zilizopo zinaeleza kuwa tangu kuzinduliwa kwa mfumo huo wa kuendesha majadiliano ya jumuiya hiyo mwaka jana, zaidi ya Sh8 bilioni zimeokolewa kwenye gharama za mikutano takribani 800 inayofanywa na sekretarieti pamoja na taasisi zake kila mwaka ambayo ilikuwa inalipiwa zaidi ya Sh24 bilioni.

Jana jumuiya hiyo imetangaza bajeti yake ya mwaka ujao wa fedha, ambayo imepungua kwa takribani asilimia 10.

Pamoja na utekelezaji wa agizo la kufunga mkanda, mishahara ya watendaji waandamizi wa Sekretarieti haijaguswa.

Watendaji wa jumuiya hiyo hawajafanya kama kile ambacho Rais Magufuli ametangaza kukifanya nchini; kushusha mishahara ya wakurugenzi na maofisa waandamizi wanaolipwa fedha nyingi kila mwezi.

Miongoni mwa watumishi wanaolipwa mishahara mikubwa ndani ya EAC ni katibu mkuu na manaibu wake ambao hulipwa hadi zaidi ya Sh40 milioni wakifuatiwa na wabunge wanaochukua zaidi ya Sh30 milioni, zinazotokana na michango ya kodi za raia wa nchi wanachama.

Bajeti hiyo imepungua kutoka Dola 110.66 milioni za Kimarekani (zaidi ya Sh221 bilioni) mpaka 101.37 milioni (zaidi ya Sh202 bilioni), jambo linaloilazimu kuchukua hatua za makusudi kupanga matumizi muhimu na kuyapunguza yasiyo na tija.

“Jumuiya inakabiliwa na changamoto ya ukwasi kutokana na kucheleweshwa kwa fedha za michango kutoka kwa wanachama na misaada ya wafadhili,” alisema katibu huyo mkuu.

Mabadiliko haya yanatokea wakati mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Rais Magufuli akiwa amechukua hatua kadhaa za kubana matumizi nchini kiasi cha kuigwa na mataifa mengine ya Afrika.

Siku chache baada ya kuzuia safari za viongozi wa Serikali nje ya nchi isipokuwa kwa kibali cha Ikulu, Rais wa Rwanda, Paul Kagame naye alifuata nyayo, huku akiwatuhumu mawaziri wake kutojali maslahi ya taifa.

Aliwatuhumu mawaziri wake wasiopungua watano kuwa wanasafiri mara tatu kwa wiki kushiriki mikutano ya EAC popote inapotokea na kwamba ziara hizo zinaigharimu Serikali yake fedha nyingi na kuahidi kwamba suala hilo litaachwa kwa waziri husika.

Hata Dk Magufuli alipochukua hatua dhidi ya wafanyakazi hewa, Rais wa Nigeria, Mohammed Buhari naye alifanya hivyo. Wakati Tanzania ikiwa imewabaini zaidi ya watumishi hewa 10,000, Buhari anao zaidi ya 40,000 waliokuwa wanalipwa na hazina ya taifa hilo kubwa kiuchumi Afrika.

Wakati Rais Magufuli akielezewa kuchukua hatua muhimu kwa taifa, gazeti la The Economist la Uingereza limedai kuwa kiongozi huyo anaonekana kupendwa, lakini ameifanya Tanzania isiwe na mazingira mazuri ya uwekezaji, jambo ambalo limepingwa vikali na Kituo cha Uwekezaji cha Tanzania (TIC).

Katika toleo hilo, The Economist limemlaumu Magufuli kwa kutimua watumishi wa umma, likidai hafuati taratibu na kutochukua hatua kufanya marekebisho ya kiuchumi.

“Muhimu zaidi ni kwamba ameonyesha utashi mdogo katika kupanua wigo wa mabadiliko ya kiuchumi yanayolenga kuongeza ukuaji wa uchumi,” inasema makala ya gazeti hilo.

“Anaonekana kuweka mazingira magumu ya kuwekeza kwenye nchi ambayo tayari inashika nafasi ya chini kwenye orodha ya Benki ya Dunia ya nchi zenye mazingira mazuri kwa biashara, ambako inashika nafasi ya 136 kati ya nchi 189.”

Lakini meneja mahusiano wa TIC, Daudi Ruganda alipinga kauli hiyo, akisema tangu Magufuli aingie madarakani Serikali imeandikisha miradi 551 ya uwekezaji yenye thamani ya dola 9.211 bilioni za Kimarekani (karibu Sh20 trilioni) kuanzia Desemba 2015 hadi Mei mwaka huu.

Alisema kati ya hiyo, miradi 229 inamilikiwa na wazawa, huku 215 ikimilikiwa na wageni na miradi 105 ni ya ubia kati ya wazawa na wageni na kwa pamoja inatarajia kuzalisha ajira 55,970.

“Taarifa hii inapotosha umma. Tanzania ni nchi ya amani na ina sera nzuri za uwekezaji zinazowavutia wawekezaji wengi kuja kuwekeza,” alisema.

Ruganda alieleza kuwa ongezeko la miradi kwa kipindi cha miezi sita tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani ni tofauti na miezi sita ya nyuma kwenye uongozi wa Awamu ya Nne ambayo kwa kipidi cha Juni mpaka Novemba 2015, miradi 458 ya uwekezaji ilisajiliwa na TIC.

Alifafanua kuwa kati ya hiyo, miradi 201 ilikuwa ni ya wazawa na 159 ilimilikiwa na wageni kutoka mataifa ya nje, huku miradi 98 ikiwa ya ubia ambayo ina thamani ya dola 5.727 milioni za Kimarekani (karibu Sh12.6 trilioni) na ilizalisha ajira 39,361 kwa wananchi.

Ruganda aliwataka wananchi kupuuza habari hizo na kusisitiza kuwa mafanikio ni makubwa katika sekta ya uwekezaji.

Alisema Tanzania ni ya kwanza kwa kuingiza mitaji ya moja kwa moja katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki.

Kaimu mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Zamaradi Kawawa alisema Serikali imeliandikia barua gazeti hilo kupitia ubalozi wake nchini Uingereza kulitaka liombe radhi kwa upotoshaji.
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top