Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

NYUFA 10 ZA UKUTA WA UKAWA

NIMEREJEA salama jiji hapa baada ya katikati mwaka wiki hii kuwa Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine, nilibahatika kuhudhuria Mkutano wa Viongozi Wastaafu wa Afrika.

Nikiwa katika mkutano huo ulioandaliwa na Taasisi ya Uongozi (Uongozi Institute) chini ya Uratibu wa Mzee Benjamin Mkapa, nikastushwa kusikia chama cha upinzani cha Chadema wameazimia kuendesha maandamano ya nchi nzima chini ya Mkakati walioupa jina la Ukuta!

Tatizo langu na Chadema au huo Ukuta si haki ya watu kuandamana katika kuelea hisia zao; bali tatizo ni unaandamana kwa hoja gani? Hapo tu ndipo penye shida. Tena kubwa. Nimezitazama baadhi ya hoja zinazolalamikiwa kwa hakika nikahuzunika sana. Ni huzuni hiyo iliyonifanya leo nitafakari nawe nyufa 10 nilizozibaini katika ‘Ukuta wa Chadema.” 

  1. Kupigwa Marufuku Siasa    
Moja ya hoja iliyotumika kujenga uchungu wa kuhalalisha kuandamana nchi nzima ni hii. Huwa nikisikiliza hoja hii nacheka sana. Nacheka kwa sababu jinsi inavyopotoshwa na kisha wapotoshaji wakauamini upotofu wao wenyewe ni sawa na mtu anayejiteka halafu anaanza kuhaha kujiokoa!

Rais Magufuli alieleza wazi na nimemsikia tena juzi akisisitiza hadharani; hajamzuia mtu kufanya siasa zake wala kukutana na wapigakura wake wala wanachama wake wala Chama kufanya vikao vyake. Rais yuko wazi; hataki siasa za majitaka za kumkwamisha kutekeleza aliyoyaahidi. Anapokea ushauri na si shinikizo. 
Rais anatakiwa kuachwa atekeleze aliyoyaahidi kwa  umma
Kuzuiwa kuandamana bila hoja na kuzungukazunguka nchi nzima kuhadaa watu wasishiriki maendeleo ila waandamane tu ndio siasa wananchi zilizotuchosha na naamini hata Rais hazitaki. Nchi haina muda huo tena.

Rais angekuwa amezuia maandamano kwa tafsiri hii ya wanaojipotosha wale wanaharakati walioandamana kuunga mkono Taifa la Palestina mwezi uliopita wangebanwa. Angekuwa amezuia wale mawakili walioandamana juzi Arusha kueleza hisia zao dhidi ya mwenzao aliyeshikiliwa kwa muda huko wangebanwa.

Hawa wote wanatekeleza haki yao ya kuandamana lakini si kuandamana tu ambako Chadema wanataka kuliambukiza Taifa; kwamba unajiteka (kwa kutoka mwenyewe Bungeni) unakuja mtaani unazoa vijana, kuwalipa na kuwashawishi muandamane! Ukizuiwa, umeonewa! 

Kwamba unajiteka (kwa kila siku Mbunge wa jimbo la mikoani kuwa Dar) na kushindwa mwenyewe kwenda jimboni kwake kisha anasimama anasingizia umezuiwa kufanya siasa na kutaka maandamanao. Maandamano ya aina hii hata mie siyakubali.


  1. Kupiga Marufuku Bunge “live”
Hii hoja siielewi na sitakaa niielewe. Kwanza aliyezuia Bunge kuoneshwa “live” ni Rais au uongozi wa Bunge? Naona anahamishiwa vita mtu asiyehusika nayo na ambaye siku zote wanamtaka asiingilie mihimili mingine.

Hivi Chadema wanataka kutuambia kwamba kama Rais leo ataingilia uhuru wa Bunge kwa kuliamuru liende laivu ndio hawatamuona tena kuwa ni “Dikteta?” Kumbe udikteta ni Rais kufanya yanayowakwaza maslahi yao hata kama yana manufaa kwa wananchi wengi?

Hivi kama suala la live ni la kitaifa na lenye kuleta uwajibikaji zaidi kama inavyodaiwa, mbona watetezi wake wanataka Bunge tu na si mihimili mingine kama Mahakama? Mbona wao wenyewe vikao na mikutano yao haiko laivu. Wanavunja haki za watu wao? 

Waswahili husema ukarimu huanzia nyumbani. Kituko ni hiki; katika wiki mbili hizi Chadema wamefanya mikutano yao kadhaa ya kimkakati kama ule wa Mameya (Arusha), Baraza la Vijana (Dar) na Baraza Kuu (Dar). Yote hii haikuwa laivu! Vipi?

  1. Kudhibitiwa Wabunge Bungeni
Mara kadhaa wamesusa wenyewe Bunge
Nimeshangazwa kuona hili wanalitaja kwenye moja ya vijenzi vya kuhalalisha maandamano ya nchi nzima. Hivi nani anayewabana huko Bungeni na kwa nini? Ni Rais? Kama si Rais kwa nini wanahamisha ugomvi huu kwa Rais?

Bungeni waliandamana sana (kwa kutoka nje ya Bunge) kila huyo anayewabana akisimamia Bunge. Imekuwaje haikutosha? Vipi yaje maandamano nchi nzima dhidi ya mtu ambaye hahusiki na kanuni mlizojiwekea na mnazozisimamia wenyewe? Naona ufa katika Ukuta huu!

  1. Kuingilia Mhimili wa Mahakama
Hii hoja nayo eti ni sehemu ya malalamiko ya kuhalalisha maandamano nchi nzima!Naona kuna kila dalili Mahakama ya Mafisadi imeanza kuwachanganya watu! Hoja hii kwamba Rais alipoahidi kuipa mahakama fedha (na kwa hakika akaitoa) alikuwa anaishawishi na kuingilia mhimili huo au kuwataka kesi ziende haraka ni kosa haina tija.

Maandamano yao mengi miaka ya nyuma yaliwakwaza raia wengine
Hakuna asiyejua kwamba Mahakama inalipwa na fedha za wananchi zinazotolewa na Serikali. Majaji wanalipwa na Serikali, wanateuliwa na Serikali, wanatumia magari ya Serikali na hata ofisi zao ni za Serikali.

Kama hiki ni kigezo cha wao kutotenda haki au kuingiliwa basi wabunge wa upinzani wasingeshinda hata kesi moja ya uchaguzi nchini na isingetokea Serikali ikaangushwa Mahakamani.

Madai na malalamiko hayo yanaweza kutolewa tu na mtu ambaye kwa upana wake ni majeruhi wa kasi, ari na nguvu mpya anayoitumia Rais katika kutaka mambo yaende na haki za wananchi zisicheleweshwe.

  1. Serikali Inatishia Ukuaji wa Uchumi
Hii ni kauli nyingine inayoweza kutolewa tu na mtu asiyetaka kulipa kodi, asiyetaka kuona juhudi za kuhimiza matumizi mazuri ya fedha za umma na mtu ambaye anaumizwa kuona Serikali inakusanya fedha zaidi ili iwatumikie wananchi

Nimeona katika tamko la Chadema kuwa eti: “Uwekezaji wa mitaji umekuwa ikiporomoka kwa kasi kubwa sana nchini mwetu na hata baadhi ya wawekezaji wanaondoa mitaji yao.

Kauli hii nayo ni mfano mwingine wa kujiteka (mtu anasambaza uongo halafu anaanza kuuamini yeye mwenyewe). Tofauti na tamko la Ukawa, taarifa iliyotolewa Mei, 2016 na Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC) inaonesha kuongezeka kwa uwekezaji tena kwa asilimia 20 zaidi katika miezi sita ya mwanzo ya utawala wa Rais Magufuli. 

Takwimu hizo zinaonesha kuwa jumla ya miradi 551 ya uwekezaji yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 9.2 ilisajiliwa na yote kwa pamoja ikiwa na uwezo wa kuajiri Watanzania 55, 970 ukiacha faida nyingine mtambuka. Kama kuna mwekezaji aliyekimbia basi ni mkwepaji si mwekezaji.


  1. Diplomasia au ghasia?  

Kijenzi kingine cha kulalamikia kuminywa kwa siasa nchini kiasi cha kuhitaji maandamano ni madai eti mabalozi kutakiwa kupata kibali Wizara ya Mambo ya Nje kabla ya kukutana na vyama vya siasa au asasi za kiraia.

Tamko la Ukawa likisema: “Utaratibu huu unaminya uhuru wa mabalozi na wanadiplomasia mbalimbali kufanya kazi zao nchini na ni utaratibu ambao unakiuka utamaduni uliokuwepo awali na pia unakiuka masharti ya Mkataba wa Vienna kuhusu mahusiano ya Kibalozi Duniani.”

Hii nayo ni kauli inayoweza kutolewa na mtu ambaye si tu neno diplomasia huenda amekuwa akilisikia tu kwenye vyombo vya habari; bali pia mwenye uvivu wa kusoma.

Nimeusoma Mkataba walioutaja kuwa umekiukwa. Hakika nimeona huzuni na aibu dhidi ya aliyeleta hoja hii na kuwashauri Chadema waiweke kwenye tamko lao.

Ibara ya 41(1) ya Mkataba huo wa Vienna iko wazi mno; inaanisha kuwa mwanadiplomasia yeyote pamoja na kinga aliyo nayo kidiplomasia bado atalazimika kufuata sheria na taratibu za nchi mwenyeji na hawataingilia masuala ya ndani ya nchi hizo. Ili kuondoa ubishi nainukuu Ibara hiyo kama ilivyo:

“41[1.] Without prejudice to their privileges and immunities, it is the duty of all persons enjoying such privileges and immunities to respect the laws and regulations of the receiving State. They also have a duty not to interfere in the internal affairs of that State.” 

Lakini ibara ya 41(2) ndiyo inatia kabisa ufa kwenye Ukuta wa Chadema. Ibara hii inaainisha tena kuwa shughuli zote za kikazi za Ubalozi zitaratibiwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi mwenyeji. Inasema:

“41[2] 2. All official business with the receiving State entrusted to the mission by the sending State shall be conducted with or through the Ministry for Foreign Affairs of the receiving State or such other ministry as may be agreed.” 

7. Uteuzi wa Wakurugenzi wa Halimashauri


Chadema wanalalamikia kuwa katika nafasi ambazo Rais amejaza za watendaji amekiuka Sheria za Utumishi wa Umma kwa kujaza watu wengi ambao ni makada wa CCM. Nimetazama sheria sijaona inaposema kuwa Rais aangalie chama cha mtu katika uteuzi.

Hata hivyo kwa mantiki tu tuchukulie madai hayo ni kweli hivi Chadema walitaka Rais ateue makada wao au wa CUF? Na kama makada wanazuia Chadema kushinda, Je, kote walikopata wabunge mwaka jana kama vile Dar es Salaam, Mbeya na Arusha na kwingineko watendaji waliosimamia huo uchaguzi walikuwa watumishi wa umma au makada wa Chadema? Kwa hiyo hili nalo ni la kumfanya mtu aandamane?

  1. Sheria Mkononi?
“Kamati Kuu imewataka wanasheria wa chama kukaa na kuyatazama mambo yote ambayo yametokea na kuchukua hatua za kisheria kwa lengo la kuyatafutia suluhisho la kisheria,” linasema tamko la Chadema la juzi.

Hapa sijaelewa, kama wanasheria wa chama wameambiwa wafungue kesi maandamano ya nini? Je, iwapo wanasheria hao watafungua kesi kabla ya Septemba Mbowe na wenzake hawaoni kwamba watakuwa wanaingilia uhuru wa Mahakama kwa kuandamana juu ya masuala yale yale ambayo wameyafikisha kortini?
  1. Demokrasia inabinywa!
“Ni wazi sasa kuwa kuna tishio kubwa dhidi ya ukuaji wa Demokrasia hapa Nchini mwetu kutoka kwa viongozi wa serikali hii ya awamu ya tano kukandamiza Demokrasia na madhara ya kukandamizwa kwa demokrasia yameshaanza kulitafuna taifa letu,” linasema tamko la Chadema.

Sielewi hata aliyeandika kama alisoma alichoandika. Demokrasia inabinywa huku anayesema hivyo akiongea anayoyasema akiwa hadharani na bila bughudha? Demokrasia inakandamizwa huku wabunge wawili wa huyo huyo anayelalamika juzi tu wameshinda kesi zao za uchaguzi dhidi ya Chama Tawala?

Demokrasia inabinywa katika nchi ambayo wabunge wa huyo huyo anayelalamika wanaamua ama watoke au wabaki Bungeni? Wanaamue waende jimboni au wabaki wakirandaranda Dar es Salaam? Hivi na hili nalo ndio sababu ya kuandamana kweli?

Image result for Demonstrations in USA
Maandamano ya tunaowaiga hutokana na masuala muhimu
 Lakini pia kuna mambo tunayatamka bila kuyapima na tunataka demokrasia nusunusu. Je, demokrasia ni kuandamana tu? Tumejifunza demokrasia ya tunaowaabudu? Tujifunze basi vitu vya maana-ukishindwa uchaguzi jipange kisiasa na sio kutaka kuzuia utekelezaji wa sera za aliyeaminiwa na wananchi tena kwa njia za mitaani.

Hivi Al Gore aliposhindwa na Bush, aliingia mitaani kuanzisha maandamano ya kila mara kupinga anachokifanya Bush? Au Mzee John McCain aliposhindwa na Obama, 2008 alianzisha maandamano ya kupinga kila anachokifanya Obama?

Wenzetu baada ya uchaguzi kazi inahamia kwenye mabunge yao ambako wanasiasa huoneshana kazi katika kutunga na kupitisha miswaada ya kutekeleza wanayoyaamini yatawasaidia wananchi.

Ukiwaona hao wa huko tulikoiga demokrasia bila kuielewa wanaingia barabarani basi wanaandamana kupongeza au kulaani suala mahsusi la kijamii na lenye maslahi yanayomgusa kila mwananchi kama vile haki za raia au kuunga mkono sera flani ya Serikali.
Sijaona Chadema wakiandamana kutaka kupigania maslahi ya moja kwa moja ya wananchi kama vile ajali nyingi kuondoa maisha ya watu, wakulima kupewa mbegu zisizoota au hata kuipongeza Serikali walau kwa kushinda mradi mkubwa wa bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Tanga litakaloinua uchumi wa nchi. Sasa kama mambo mengi yanayowagusa wananchi hayatuhusu sioni sababu ya maandamano haya, Sijaiona.


  1. Udikteta  

Ukitaka kujua walionyuma ya maandamano haya ni watu walioumizwa na mageuzi makubwa ambayo Rais Magufuli ameanza kuyafanya, itazame hoja hii.Na ukitaka kujua kwamba walionyuma ya hoja hii ni watu ambao hawaelewi wanasimamia hoja gani leo na watasimamia hoja ipi kesho, itazame hoja hii.

Ni hawa hawa mwaka jana walitaka mali za umma zisichezewe leo Rais Magufuli anazilinda kawa dikteta. Mwaka juzi walitaka nchi ikusanye kodi, leo Rais anakusanya kodi, wamenuna. Walijivika ajenda ya ufisadi lakini sasa wamejiteka, hawataki fisadi aguswe. Kama hii ndio sababu ya maandamano, yafutwe tu.
Madikteta hawana muda kama huu; kuhuzunika na wenzao


Nihitimishe: kwa nyufa hizo hapo juu mkakati mzima uitwao Ukuta unabaki kuwa jambo la mzaha. Ukuta wenye nyufa, tena dhaifu kama tulizoziona hapa, hauwezi kutuhakikishia usalama wa nyumba tunayoambiwa tukaishi.

Ndio maana katika makala haya leo nimeamua kusisitiza bayana kabisa hii ajenda ya Ukuta hainatija. Tuikatae.  

Alamsiki.


*Mwandishi wa makala haya ni Mtanzania aishie na kufanyakazi jijini Addis Ababa, Ethiopia na amebobea katika masuala ya taaluma za maendeleo.
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top