Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Mtuhumiwa Escrow augua ghafla


UPANDE wa Tetezi katika Kesi ya Uhujumi uchumi inayomkabili Bosi wa IPTL Harbinder Singh Seth na James Rugemalira wameiomba Mahakama kumruhusu Mteja wao akatibiwe nje ya nchi kutokan na Maradhi yanayomkabili

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, jana ilikataa ombi hilo na  badala yake kumtaka atibiwe na Hospitali ya Jeshi la Magereza.

Mahakama hiyo imeeleza kuwa Sethi hana sababu ya kwenda nje ya nchi kwa sasa ili kutibiwa ugonjwa huo wa tumbo na badala yake, madaktari wake kutoka nje ya nchi wanaweza kutua nchini na kushirikiana na wale wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) katika kumtibu ikiwa atazidiwa.

Maelekezo hayo ya mahakama yalitolewa jana baada ya mawakili wa Sethi kuomba mteja wao aruhusiwe kwenda kutibiwa nje ya nchi kutokana na maradhi ya uvimbe tumboni yanayomsumbua kwa sasa wakati akiwa mahabusu.

Mshitakiwa huyo (Sethi) alipelekwa mahabusu katika Gereza la Keko baada ya kukosa dhamana alipofikishwa kortini kwa mara ya kwanza na kusomewa mashtaka kadhaa, likiwamo la utakatishaji fedha.

Awali, mawakili hao wa Sethi, jana waliwasilisha mahakamani maombi ya kutaka mteja wao akatibiwe nje ya nchi, lakini mahakama ikasisitiza kuwa mshtakiwa huyo ataendelea kuwa mahabusu (Keko) huku Jeshi la Magereza likisimamia kuimarika kwa afya yake.

Mbali na Sethi, mshtakiwa mwingine ni James Rugemarila, ambao wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka ya kugushi, utakatishaji fedha na kusababisha hasara ya dola za Marekani milioni 22.1 pamoja na Sh. bilioni 309.4.

Amri ya kutaka Sethi aendelee kutibiwa maradhi ya tumbo akiwa mahabusu nchini, ilitolewa na Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi, baada ya upande wa utetezi kuwasilisha nakala za ripoti ya madaktari kutoka Afrika Kusini anakohudhuria matibabu na kuomba kibali cha kwenda kutibiwa.

Wakili wa utetezi, Alex Balomi, alidai kuwa mshtakiwa anasumbuliwa na maradhi ya tumbo na nakala za vyeti zinaonyesha kwamba ana uvimbe tumboni.

"Mheshimiwa hakimu, upande wa utetezi tunaomba kibali cha mshtakiwa kwenda kutibiwa nje kwa sababu wiki ya nne sasa anakosa usingizi na hali yake inazidi kuwa mbaya kutokana na maumivu anayoyapata," alidai Balomi.

Hata hivyo, upande wa Jamhuri ukiongozwa na Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai, akisaidiana na Janeth Kafuko, ulipinga maombi hayo.

Swai alidai kuwa upande wa utetezi hauna mamlaka ya kuwasilisha nakala za vyeti hivyo na kwamba aliyetakiwa kuwasilisha na kuieleza mahakama ni daktari wa mshtakiwa.

Pia alidai kuwa vyeti hivyo vilitakiwa kuwasilishwa mahakamani vikiwa halisi na si nakala, hivyo kwa mujibu wa sheria, aliomba mahakama kutupilia mbali maombi hayo.

Hakimu alisema suala la ugonjwa si la kufumbia macho, hivyo Magereza wahakikishe wanasimamia matibabu ya mshtakiwa na kwamba ikishindikana wampe rufani kwenda kutibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

"Madaktari wa Hospitali ya Muhimbili watashirikiana na madaktari wake walioko nje kwa ajili ya kumpa matibabu akiwa hapa nchini," alisema Hakimu Shahidi baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili na kutupilia mbali hoja ya utetezi.

Alisema kesi hiyo itatajwa Julai 28, mwaka huu na washtakiwa wataendelea kukaa mahabusu.

Awali, upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na hivyo, uliomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Rugemarila ni Mkurugenzi Mtendaji wa VIP Engineering na mmiliki mwenza wa zamani wa Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Ltd (IPTL) na Seth ni Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Power African Power (PAP) Tanzania Limited. Wote walirudishwa mahabusu.

Katika kesi ya msingi, Wakili wa Serikali Mwandamizi Shadrack Kimaro, alidai kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19 , 2014 jijini Dar es Salaam walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ili kutenda kosa.

Alidai katika mashitaka ya pili, kati ya Oktoba 8,2011 na Machi 19,2014 jijini Dar es Salaam, wakiwa si watumishi wa umma, walishirikiana na watumishi wa umma kutekeleza mpango huo wa uhalifu kwa lengo la kujipatia faida.

Katika mashitaka ya tatu yanayomkabili Sethi, inadaiwa kuwa Oktoba 10, 2011 katika mtaa wa Ohio, Ilala jijini Dar es Salaam, akiwa na nia ya ulaghai alighushi fomu namba 14 A ya usajili wa kampuni na kuonyesha kuwa yeye ni Mtanzania anayeishi Kitalu namba 887 Mtaa wa Mrikau, Masaki wakati akijua si kweli.

Pia Sethi anadaiwa kutoa nyaraka ya kughushi ambayo ni fomu namba 14 A ya usajili wa kampuni kwa Ofisa Msajili wa Kampuni, Seka Kasera, kwa njia ya kuonyesha kwamba yeye ni Mtanzania na mkazi wa Mtaa wa Mrikau, Masaki Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Aidha, Kimaro alidai katika mashitaka ya kujipatia fedha kwamba kati ya Novemba 28 na 29, 2011 na Januari 23, 2014 katika Makao makuu ya Benki ya Stanbic, Kinondoni na Benki ya Mkombozi Tawi la St. Joseph Cathedral, kwa ulaghai, washitakiwa hao walijipatia kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT), dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh. 309, 461,300,158.27.

Pia washitakiwa wote wanadaiwa kuisababishia serikali hasara. Inadaiwa walitenda makosa hayo Novemba 29, 2013 katika Benki ya Stanbic tawi la makao makuu Kinondoni na kwa vitendo vyao, waliisababishia Serikali hasara ya dola 22,198,544.60 na Sh. 309,461,300,158.27.

Kimaro alidai kati ya Novemba 29,2013 na Januari 23, 2014 maeneo tofauti Dar es Salaam kwa pamoja walitenda kosa la kutakatisha fedha kwa kuchukua fedha kutoka BoT ambazo ni dolamilioni 22.1 na Sh bilioni 309.4 wakati wakijua fedha hizo ni zao la kujihusisha na genge la uhalifu.

Katika mashitaka ya nane, Kimaro alidai kuwa Novemba 29, mwaka 2013, katika Tawi la Kati la Benki ya Stanbic Tanzania, Wilaya ya Kinondoni, Sethi alitakatisha fedha kwa kuchukua kutoka BOT, dola milioni 22.1 wakati akijua fedha hizo zimetokana na zao la kujihusisha na genge la uhalifu.

Aidha, Sethi anadaiwa kuwa kati ya Novemba 29, 2013 na Machi 14, 2014, katika Tawi la Kati la Benki ya Stanbic Kinondoni, Dar es Salaam, alitakatisha fedha, Sh. bilioni 309.4 kutoka BOT wakati akijua fedha hizo zimetokana na zao la uhalifu.

Katika mashitaka ya 10, inadaiwa Januari 23, 2014 katika Benki ya Mkombozi Tawi la St. Joseph Cathedral, Rugemarila alitakatisha fedha, ambazo ni Sh. bilioni 73.5 kutoka kwa Sethi wakati akijua fedha hizo zimetokana na zao la kujihusisha na genge la uhalifu.

Pia inadaiwa kuwa Januari 23, 2014, katika Benki ya Mkombozi, tawi hilo la St. Joseph Cathedral, Rugemarila alitakatisha fedha ambazo ni dola 22,000,000 kutoka kwa Sethi wakati akijua fedha hizo ni zao la uhalifu.

Kimaro pia alidai kuwa Seth anadaiwa kuwa Januari 28, 2014 katika Benki ya Stanbic Kinondoni, alihamisha Rand (ZAR 1,305,800) kwenda kwenye akaunti namba 022655123 katika Benki ya Standard Land Rover Sandton ya Afrika Kusini wakati akijua fedha hizo zimetokana na zao la kujihusisha na genge la uhalifu.

Washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top