Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Tabora Wapewa Maisha Mapya.......Rais Magufuli Azindua Miradi Mbalimbali ya Maendeleo

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli jana tarehe 24 Julai, 2017 ameweka jiwe la msingi katika miradi mikubwa miwili ambayo ni mradi wa maji kutoka ziwa Victoria kwenda miji ya Tabora, Igunga na Nzega na mradi wa ukarabati na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Tabora, na amefungua barabara mbili za Tabora – Nyahua na Tabora – Puge – Nzega.

Mradi wa maji kutoka ziwa Victoria utatekelezwa kwa muda wa miezi 30 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 600 ikiwa ni Mkopo kutoka Serikali ya India na utazalisha takribani lita Milioni 80 za maji kwa siku kwa ajili ya wakazi wa Tabora ambao kwa sasa wanahitaji lita Milioni 36 na pia utamaliza tatizo la maji katika miji ya Igunga, Nzega, Tinde, sehemu ya Wilaya ya Uyui, Shinyanga Vijijini na Vijiji 89 vilivyo kando ya mabomba ya mradi huo.

Mradi wa ukarabati na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Tabora unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu kuanzia sasa na ni miongoni mwa miradi inayotekelezwa kwa awamu tatu katika Mikoa ya Bukoba, Kigoma, Tabora na usanifu wa viwanja vingine 11 katika Mikoa mbalimbali nchini kwa gharama ya Shilingi Bilioni 69.7.

Barabara ya lami ya Tabora – Nyahua yenye urefu wa kilometa 85 imejengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 123.773 na barabara ya Tabora – Puge – Nzega yenye urefu wa kilometa 114.9 imejengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 160.515, fedha zote zikiwa zimetolewa na Serikali ya Tanzania.

Baada ya kuweka mawe ya msingi na kufungua miradi hiyo, Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli alifanya mkutano wa hadhara katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Mjini Tabora ambapo aliipongeza Wizara ya Maji na Umwagiliaji na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa kutekeleza miradi hiyo, na pia alimuomba Balozi wa India hapa nchini Mhe. Sandeep Arya kumfikishia shukrani zake na za Watanzania kwa Waziri Mkuu wa India Mhe. Narendra Modi kwa kutoa mkopo wa Shilingi Bilioni 600 kwa ajili ya kufanikisha mradi huo wa maji na pia kutoa fedha nyingine Shilingi Trilioni 1.2 kwa ajili ya kutekeleza miradi mingine 17 hapa nchini.

Mhe. Rais Magufuli alimtaka Mkandarasi anayejenga mradi wa maji kutoka ziwa Victoria kuharakisha kazi hiyo na kuikamilisha kabla ya miezi 30 ili wananchi wa Tabora na maeneo yanayosubiri maji ya mradi huo waanze kunufaika mapema na pia ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuongeza urefu wa njia ya kurukia ndege ya uwanja wa Tabora kutoka kilometa 1.9 waliyopanga hadi kufikia kilometa 2.5 na kujenga jengo kubwa zaidi la abiria litakaloweza kuchukua abiria laki 5 kwa mwaka badala ya abiria 50,000 kama ilivyopangwa hali itakayouwezesha uwanja huo kupokea ndege kubwa na ndogo.

Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia wananchi wa Tabora kuwa Serikali yake imejipanga kutekeleza ahadi alizotoa ikiwemo kujenga reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) itakayoanzia Dar es Salaam – Morogoro – Dodoma – Tabora hadi Kigoma ili kurahisisha usafiri na kukuza biashara ya ndani na nje ya nchi na amewataka wote waliojenga majengo katika hifadhi ya reli kujipanga kuondoa majengo yao kwa hiari kwa kuwa Serikali haitawalipa fidia yoyote.

Kuhusu kero mbalimbali ambazo wananchi wengi wamekuwa wakitaka kumweleza Rais katika mikutano na kwa kutumia mabango Mhe. Dkt. Magufuli aliwaagiza viongozi wa Mikoa na Wilaya kutenga muda kila wiki kwa ajili ya kusikiliza kero hizo na ameonya kuwa kuendelea kwa vitendo hivyo kunaashiria kuwa viongozi wa maeneo husika hawatekelezi wajibu wao ipasavyo.

Pamoja na Mawaziri Prof. Makame Mbarawa Mnyaa na Mhandisi Gerson Lwenge mkutano huo umehudhuriwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Prof. Norman Sigalla King na Wabunge wa Mkoa wa Tabora ambao walimtaka Mhe. Rais Magufuli kutokatishwa tamaa na watu wanaobeza juhudi kubwa anazozifanya kuwapigania Watanzania, na wamemhakikishia kuwa Wabunge wote wenye nia njema na Tanzania wataendelea kumuunga mkono katika dhamira yake ya kuijenga Tanzania Mpya.

 Leo tarehe 25 Julai, 2017 Mhe. Rais Magufuli ataendelea na ziara yake Mkoani Singida ambako atafungua mradi wa barabara ya Manyoni – Itigi yenye urefu wa kilometa 89.3

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Tabora
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top