Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Unafiki unaliangamiza Taifa

Image result for mbowe
Baba wa Taifa letu, Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kuja na ujenzi wa falsafa yake kuhusu dhana ya maendeleo. Kwa kutumia hekima, busara na kwa kinywa chake mwenyewe, Mwalimu Nyerere alisema “ili tuendelee tunahitaji vitu vinne ambavyo ni ardhi, watu, siasa safi na uongozi bora”
.
Tatizo linalotukumba ni uwepo wa laana inayotumaliza kutokana na kuiasi falsafa ya Baba yetu, Mwalimu Nyerere kwa kupuuzia dhana ya uwepo wa siasa safi na uongozi bora. Hatuwezi kuendelea kwa kuendesha ushabiki upofu ama siasa za maji taka, yaani siasa chafu za kuchafuana na kupakana matope kila kukicha. 

 Mbaya zaidi ni hayo madudu yamekuwa yakifanyika chini ya mwamvuli “unafki”. Kwa tafsiri ya haraka haraka neno unafki unaweza ukasema ni undumila kuwili wa kujivika sura mbili tofauti kwa nyakati moja lakini kwa mahali tofauti tofauti kulingana na muktadha husika. Lengo kuu la kufanya hivyo ni kutaka kuharibu uhalisia kwa njia ya mficho na wakati huo huo mtu huyo huyo aonekane mwema machoni.

Hali hii ya baadhi ya watu  kuwa wanafki haikuanza leo wala jana. Historia inatudhihirishia hilo kuwa hali ya baadhi ya watu kuutumia mwamvuli huu wa unafki na kuamua kuwa wanafki, haikuanza leo, wala jana kwani ulikuwapo tangu enzi za utawala wa kwanza wa Mwalimu Nyerere hadi hii leo katika utawala wa awamu ya nne yake Dk. Kikwete na utaendelea kuwepo.  Utofauti wa unafki upo kwenye ukomavu wake.

Tuweke kumbukumbu zetu sawa. Mwalimu Julius Nyerere wakati akiwa madarakani alimwagiwa lawama na tuhuma lukuki kwani wapo waliosema Mwalimu haambiliki na wengine wakadai anaendesha nchi kwa “remote” akiwa Butiama (kijijini kwao). Lakini mara baada ya kung’atuka kwa hiari Urais ndipo sifa za kinafki zilianza kummiminikia huku tukianza kumuita “Baba wa Taifa”. Mara baada umauti kumkuta ndipo unafki ulizidi kwake na leo hii kila kitu kibaya kinachotokea tunasema laiti Mwalimu Nyerere angekuwepo haya yote yasingetokea. Lakini angali hai ama madarakani hatukuyatambua haya zaidi ya kuuendekekeza unafki.

Ama Alhaji Hassan Mwinyi wakati akiwa Rais wa awamu ya pili walimwita mbinafsi, muuzaji nchi kutokana na ubinafsishaji lakini leo hii ni mstaafu wanaanza kummwagia sifa teletele  na hata kumwita “Mzee wetu” huku wakijivunia kuchota hekima na busara kutoka kwake lakini angali madarakani hatukuliona hilo. Huu ni unafki mtupu.

Pia  Benjamini Mkapa alidhihakiwa kweli kweli wakati wa uongozi wake hadi kufikia hatua ya kumwita ‘ukapa’ badala ya Mkapa kutoka katika neno la ‘ukata’. Lakini leo hii kila anapokatiza ni shangwe, makofi, vifijo, na vigelegele na tukisema afadhali ya Mkapa kuliko wote na wengineo tumewaona wakimpa hata tuzo ya heshima. Jamani! Kama huu si unafki, basi tuuiteje?

Hata Dk. Jakaya Kikwete (JK) alipokuwa madarakani walimuita majina mengi ya hovyo hovyo. Wapo waliomuita “Mzee wa kutabasamu”, Serikali yake ni dhaifa na legelege! Lakini hekima na busara kubwa aliyojaaliwa Dk. Kikwete hakuweza kuwajibu lolote waliokuwa wakimkejeli na badala yake aliwaambia mtanikumbuka.

Kikwete alisema: “Mtaumbuka baada ya 2015”. Dk. Kikwete aliwaambia wanaombeza sasa wataona aibu baada ya kumaliza kipindi chake. Naam! Ni kweli Watu waliokuwa wakimbeza wameanza kuumbuka na kunza kupayuka hadharani kuwa wana mkumbuka.

Wale waliokuwa wakidai JK ni legelege na dhaifu wanataka Rais mkali ndio hao hao leo hii wanasema Rais Magufuli ni dikteta; Wale waliokuwa wanasema JK hawezi kuchukua maamuzi magumu ya kutimua wanaoharibu, ndio hao hao leo hii wanaosema kuwatumbua “kuwafukuza”  wanaoharibu ni kinyume na haki za binadamu; Mara JK hakamati mafisadi Papa ama hawakamati wauzaji madawa ya kukevya, leo hii wameanza kukamatwa wanaanza kuwatetea kwa kusema si vyema kuwataja watu majina, mara si vyema kuwakamata waliolitumikia Taifa letu!

Ajabu na kweli ni kuibuka kwa Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe kusema hali ya kimaisha wakati wa utawala wa Kikwete ilikuwa bor zaidi. “Maisha yalikuwa safi enzi za Kikwete” amesema Mbowe.

Mbowe ameanza kujivua nguo kwa kutaka leo hii kuwaaminisha Watanzania kwamba maisha yalikuwa mazuri kipindi cha JK kuliko kipindi hiki cha JPM. Kibaya zaidi hajaja na utafiti wa kitaalamu kuthibitisha kauli yake bali kaamua kujisemea tu ilimradi asikike kuwa anasema.

Kama kweli maisha yalikuwa mazuri kwanini walikuwa wakimkashifu mtu (JK) ambaye amewanyooshea Watanzania maisha yao? Kulikuwa kuna sababu gani kwa Mbowe na kundi lake kumfedhehesha majukwaani kwamba Serikali yake ilikuwa dhaifu na maisha yalikuwa magumu? Leo hii wanamponda Rais Magufuli, kwanini tusiamini kwamba akitoka madarakani nae wataanza kumsifia?

Jana wakati Kikwete yupo madarakani walisema maisha magumu, leo hii hayupo madarakani wanamsifu kuwa maisha yalikuwa bora! Huu ndio unafki wenyewe unaofanywa na Wanasiasa usio na tija kwa umma.

Bila shaka haya marashi ya kinafki yalioanza kupulizwa tangu enzi za utawala wa awamu ya kwanza hautaiacha awamu hii ya tano. Leo hii Rais Magufuli anatukanwa vibaya mno kwani kila mtu anayejisikia kumuongea vibaya anafanya hivyo. Lakini subiria akitoka madarakani, hizo sifa atakazo mwagiwa, usizipimie kabisa!. Rais Magufuli awe sawa kimkao na marashi haya ya kinafki.

Unafki niliouzungumzia ni sehemu ya khulka ya kawaida kabisa kwa asilimia kubwa ya watu kutokupenda kuzungumzia mazuri ya mtu akiwa hai wanasubiria mpaka awe amefariki ndipo wamzungumzie kwa mema; Ama wale walio katika uongozi huwa hawasifiwi kwa kile wanachokifanya mpaka wamalize muda wao wa uongozi ndipo sifa kedekede huanza kumiminika. Yote hayo ni sehemu ya unafki wetu sie tusio na shukrani.

Hivi watapungukiwa na kitu gani endapo watamsifia Rais Magufuli kwa utekelezaji wa ilani anaoufanya? Watapungukiwa na nini wakimsifia kuwa anatoa elimu bure, amenunua ndege 4 mpya, anajenga reli ya kisasa, anafuta kodi kero kwenye kilimo, anapeleka umeme vijijini, anapeleka maji vijijini! Watapungukiwa nini wakimsifia? Watapungukiwa nini wakisema ukweli amepunguza kasi ya kiwango cha rushwa na kurejesha nidhamu ya uwajibikaji kwa Watumishi wa umma. Kwanini hawajifunzi kuusema ukweli wa hali ilivyo?

Baadhi ya Watanzania wanashindwa kuunga mkono ama kutoa ushirikiano wa kutosha kwa juhudi zinazofanywa na Serikali kwa sababu tu wapo Watu wachache ambao kazi yao kuupindisha ukweli, kazi yao kuhakikisha wanarudisha nyuma maendeleo kwa maslahi yao binafsi na si ya kitaifa. Kuna haja ya kuanza kutokufuata mkumbo wa kuamini kila lisemwalo nao kuwa ni sahihi kwani mara baada ya mtu kutoka madarakani huanza kumsifia wakati hapo awali walikuwa wakimponda.

Hila, roho mbaya, tamaa za fisi za uchu wa madaraka na mali huwafikisha kwenye upindishaji wa mambo kwa maksudi ilimradi ukweli uonekane ni uongo, kwa kuwaamisha watu uongo wao pasipo kujua kuwa umma wanaujua uongo wao. 

Ipo mifano mingi tu ya kuelezea jinsi gani unafki unaofanywa, unavyotuletea umaskini. Unafiki umezaa kitendo cha kupuuzia falsafa ya Mwalimu Nyerere kwa kudharau dhana ya uwepo wa siasa safi na uongozi bora ambayo alituasa tuyazingatie.

Laiti kama unafki ungelikuwa ni pesa, basi watu wangekuwa matajiri. Kwani leo hii baadhi ya watu wameigeuza nchi hii kuwa kama Taifa la Makambare. Si Mtoto, Mama wala Baba wote ni wanafiki watupu. Tuukatae unafki huu! Na Emmanuel J. Shilatu
Download Our App

1 comments:

Unafiki ni mbaya na Wahenga waliisha sema,"Msemakweli ni mpenzi wa Mungu"!

Wabariki Mungu anawaona!

Ya Mbowe na Kampuni yake:CHADEMA iliyokodiwa na Bilionea Lowassa hatuyashangai kuwa na "ndimi-mbili", jana wakituaminisha pale MwembeYanga wanao ushahidi Lowassa FISADI #9, na leo hii ni Kamanda, akigombea na Urais!

Unafiki utawaadhibu kwenye Sanduku la Kura!

Reply

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top