Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Wakimbizi 6,700 raia wa Burundi kurejea makwao kwa Hiari

Kufuatia wito wa Rais John Pombe Magufuli alioutoa hivi karibuni, hadi kufikia tarehe 01 Agosti, 2017 jumla ya wakimbizi 6,700 raia wa Burundi wameshajiorodhesha kurejea nchini mwao kwa hiari.

Kufuatia hatua hiyo, Mkutano wa pande tatu utakaojumuisha Serikali za Tanzania, Burundi na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) unatarajiwa kufanyika mwishoni wa mwezi huu kujadili namna ya kuwarejesha nchini mwao wakimbizi hao kwa kuzingatia sheria za kimataifa zinazohusu wakimbizi.

Katika mahojiano na mwandishi wetu ofisi kwake jana, Mkurugenzi Idara ya Huduma za Wakimbizi katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Bwana Harrison Mseke alieleza kuwa tangu kutolewa kwa wito huo, Wizara imekuwa ikiwamahasisha wakimbizi hao kujiorodhesha kwa hiari ili waweze kurejea nyumbani.

Akiwa katika ziara yake kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa, Rais Magufuli alitoa wito kuwataka wakimbizi raia wa Burundi kurejea nyumbani kwa hiari kwa kuwa hali ya usalama nchini mwao ni nzuri ambapo wakati akitoa wito huo tarehe 20 Julai, 2017 huko Ngara aliambatana na Rais wa Burundi, Pierre Nkurunzinza ambaye nae aliwahakikishia wakimbizi hao kuwa hali ni shwari nchini Burundi.

Kwa mujibu wa Bwana Mseke, hivi sasa kuna wakimbizi raia wa Burundi 276,692 kati ya wakimbizi 348,019 walioko nchini. Wengine ni  wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) 70,840, Wasomali 150, na wengine (mchanganyiko) 337.

Alifafanua kuwa kati ya idadi hiyo ya wakimbizi raia wa Burundi 242,340 waliingia nchini baada ya mwezi Aprili, 2015 kufuatia machafuko ya kisiasa nchini humo.

Akizungumzia mwendo wa uingiaji wakimbizi kutoka Burundi, alieleza kuwa kwa sasa kasi imepungua kutoka wastani wa wakimbizi 1,000 kwa siku kati ya mwezi Agosti hadi Disemba, 2016 hadi wastani wa wakimbizi kumi kwa siku katika miezi ya hivi karibuni.

“Mwezi Januari mwaka huu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi alifuta tamko la Primafacie alilolitoa mwezi Mei, 2015 ambalo linataka wakimbizi wanaokimbia machafuko nchini kwao waruhusiwe kuingia kwa makundi bila ya utambuzi,” alieleza Bwana Mseke.

Alibainisha  kuwa, bila ya tamko hilo “Kwa wastani wa wakimbizi 1000 kwa siku kuanzia Januari, 2017, tungekuwa tunapokea wastani wa wakimbizi 30,000 kwa mwezi na hadi kufikia sasa tungekuwa tumepokea wakimbizi wapatao 240,000”.

Aliongeza kuwa hatua hiyo ya Waziri kufuta tamko hilo ilizingatia hali halisi ya utulivu na usalama nchini Burundi ambapo ilikuwa imetengamaa na maisha yamerejea katika hali ya kawaida.

Mkurugenzi huyo wa Huduma za Wakimbizi alieleza kuwa raia wa Burundi ambao walikuwa wakiingia nchini mwaka jana wengi walikuwa wakikimbia hali ya upungufu wa chakula nchini humo tatizo ambalo lilizikumba pia baadhi ya nchi nyingine katika ukanda huu.

Wakati akitoa wito huo, Rais Magufuli aliiagiza pia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kusitisha mara moja kuwapatia uraia wakimbizi raia wa Burundi.

Bwana Mseke alibainisha kuwa serikali tangu Awamu ya Kwanza imekuwa ikiwapatia uraia wakimbizi kutokana na hali halisi ambapo mwaka 1983 wakimbizi 32,000 raia wa Rwanda walipewa uraia. Kati ya mwaka 1995 na 2012 wakimbizi wa kisomali wenye asili ya kibantu 3,000 walipewa uraia na mwaka 2014 wakimbizi raia wa Burundi 162,156 walipewa uraia.

Agizo hilo la Rais la kusitisha utoaji uraia kwa wakimbizi linatarajiwa kusaidia kupunguza idadi ya wakimbizi nchini kwa kuwa imeibainika baadhi yao huja nchini kwa nia ya kujipatia uraia.
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top