Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Tanzania yawa soko kuu la nyama la kimataifa

TANZANIA kuanzia Januari mwakani itarejea kwa kishindo katika soko la nyama la kimataifa wakati kiwanda cha nyama cha kisasa cha machinjio na usindikaji cha Nguru Hills kilichopo Mvomero, Morogoro kitakapoanza kazi.

Kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuchinja ng’ombe 300 na mbuzi 2,000 kwa siku. Ujio wa kiwanda cha Nguru unaleta matumaini mapya kwa sekta ya nyama baada ya Tanzania kutamba kati ya mwaka 1947 na 1975 kupitia kiwanda cha Tanganyika Packers Ltd (TPL) ambacho kilisafirisha nyama iliyosindikwa hadi soko la Ulaya.

Wakati huo kiwanda hicho kilipokuwa kinafanya kazi kilikuwa ni kiwanda tanzu cha kampuni ya Uingereza ya kusindika nyama ya Liebig’s Extract of Meat Corporation (Lemco). Kabla ya kutaifishwa mwaka 1974, TPL ilikuwa imeajiri watu 1,200.

Tanzania ilipata pigo kubwa wakati Lemco walipoondoa chata yao katika leseni ya soko. Kuondolewa kwa leseni hiyo kulileta mgogoro mkubwa wa uzalishaji na mwaka 1993 kiwanda kilifungwa rasmi. Wakati TPL ikifanya kazi ilikuwa inachinja ng’ombe 550 kwa siku katika shifti mbili za kufanyia kazi.

Kuanza kwa usindikaji huo katika kiwanda cha Nguru baada ya miaka 25 ya kuondoka katika soko la kimataifa kutasaidia ufugaji na wafugaji ambao kwa sasa wanalalamikia soko.

Hii ina maana kwamba, wafugaji wa Tanzania sasa watakuwa na soko la uhakika wa mifugo yao, kwani kwa kiasi hicho, ina maana kwa mwezi, ng’ombe 9,000 watachinjwa, sawa na ng’ombe 108,000 kwa mwaka.

Aidha, mbuzi 60,000 watachinjwa kwa mwezi, sawa na mbuzi 720,000 kwa mwaka. Aidha, kiwanda hicho ambacho kitapeleka asilimia 80 ya nyama katika soko la nje, hasa nchi za Mashariki ya Kati na Mashariki ya Mbali, kitatoa ajira za moja kwa moja kwa wafanyakazi 500 na nyingine nyingi zisizo za moja kwa moja.

Mkurugenzi Mkuu LAPF, Elliud Sanga alisema hivi karibuni kuwa, asilimia 20 ya bidhaa zinazozalishwa zitalenga soko la kimataifa, asilimia 20 itakuwa kwa ajili ya hoteli za Tanzania, taasisi zenye uhitaji wa nyama bora na ya uhakika, lakini pia kwa Watanzania kwa ujumla, kwani itafikiria kuwa na maduka yake katika baadhi ya maeneo.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu, LAPF imewekeza dola 3,900,000 (Sh bilioni 8) na hivyo kumiliki asilimia 39 ya hisa zote, huku wawekezaji wengine wakiwa kampuni ya Eclipse (asilimia 46) na Busara Investment yenye asilimia 15. “Jamani, hii ni fursa ya kipekee kwa wakulima na wafugaji wetu…

Ukiacha faida za moja kwa moja kwa moja kwa wafugaji na jamii inayozunguka kiwanda, tutarajie pia ongezeko la fedha za kigeni kwa kuuza bidhaa za nje na kuiinua sekta ya mifugo nchini,” alisema.

Aidha kuwapo kwa uzalishaji kutasaidia kuondokana na migogoro baina ya wakulima na wafugaji katika maeneo mengi ya Tanzania kwa kuwa wafugaji watakuwa na uhakika wa soko la mifugo.

Kuwapo kwa kiwanda hicho kumewezeshwa na Mfuko wa Pensheni wa LAPF, ambayo imeungana na wadau wengine kuunga mkono kwa vitendo jitihada za Serikali ya Awamu wa Tano ya Rais, Dk John Magufuli za kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na hivyo kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2015.

Naye mtaalamu katika sekta ya nyama, Cerusiri Badrinath, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Zubair Corporation ya Oman ambayo ni kampuni mama ya Eclipse Investment yenye ubia katika kiwanda cha Nguru, alisema wamechagua eneo sahihi la uwekezaji, kwani nchi za Mashariki ya Kati na Mashariki ya mbali ni walaji wazuri wa nyama pengine kuliko sehemu nyingine duniani.

“Mfano, wao wastani wa kula nyama ni kilo 66 kwa mtu, na kumbuka wapo zaidi ya milioni 56… lakini kiwango cha dunia cha wastani wa kila mtu kula nyama hakifikia hata kilo 50 kwa mwaka.

Inakadiriwa katika miaka mitatu ijayo kiwango kinaweza kufikia asilimia 78. “Sasa hakika hili ni soko la uhakika mno. Kikubwa ni kuhakikisha nyama inayotoka Tanzania inakuwa na ubora wa kimataifa, na ndilo lengo letu. Hivi karibuni hawa waliagiza nyama yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni tano (Sh trilioni 12), hii si biashara ndogo hata kidogo,” alifafanua.

Tanzania ndiyo ya kwanza kwa nchi wanachama wa Afrika Mashariki (EAC) kuwa na idadi kubwa ya mifugo. Kwa mujibu wa ripoti ya ufugaji ya Wizara ya Mifugo ya mwaka 2013, Tanzania ina idadi ya ng’ombe zaidi ya milioni 22.8, mbuzi milioni 15.5, kondoo milioni 6.9 na nguruwe milioni 2.1 milioni.

Aidha, kwa mujibu wa Shirika la Chakula Duniani (FAO), wakati Brazil ikiongoza duniani kwa kuwa na ng’ombe milioni 211, Tanzania inashika nafasi ya 11 duniani. Kwa Afrika, Tanzania ni ya tatu, ikitanguliwa na Ethiopia yenye ng’ombe milioni 54 wanaifanya nchi hiyo ishike nafasi ya tano duniani. Sudan yenye ng’ombe milioni 41.9 inashika nafasi ya pili Afrika na ya saba duniani.

Kwa ukanda wa EAC, Tanzania inafuatiwa na Kenya yenye ng’ombe milioni 18.1, Uganda ng’ombe milioni 13, Sudan Kusini ng’ombe milioni 12, Rwanda ng’ombe milioni 1.4 na Burundi ina ng’ombe 777,786.

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Clifford Tandari alipongeza uwekezaji huo, akisema kwa yanayofanywa na wawekezaji kama LAFP yanatoa taswira halisi kwamba, `Tanzania ya Viwanda Inawezekana’ na kwamba unafungua fursa zaidi za ajira.

Regina Chonjo, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro anayekaimu pia Ukuu wa wilaya ya Mvomero, alisema kuanzishwa kwa kiwanda hicho ni furaha kwa wakulima na wafugaji ambao kwa miaka mingi walikuwa na migogoro kutokana na wafugaji kudaiwa kuvamia maeneo ya wakulima na kulisha mifugo yao mazao ya wakulima.

“Kwa ujio wa kiwanda hiki, nina uhakika ufugaji holela sasa utakoma na watu watahamia kwenye ufugaji wenye tija. Kila mmoja atataka kufuga kisasa ili kujiongezea kipato kwa sababu tayari kuna soko la uhakika, la kila siku. Kuchinja ng’ombe 300 na mbuzi 2,000 kwa siku si mchezo.

“Lakini pia kuna manufaa mengi yatakayotokana na kiwanda hiki, wakulima watauza majani kwa ajii ya mifugo, ajira zitaibuka, nyingi tu, fursa mbalimbali zitaibuka kumbukeni kutakuwa na pia na pilika za magari hapa… sasa ni wakati wa wenyeji wa Morogoro kujiandaa zaidi kwa fursa zitakazofunguka hapa,” alisema.

Mbali ya nyama, ngozi na maziwa, kinyesi pia kitatumika kuboresha kilimo cha majani na mazao mengine kuzunguka kiwanda, kutakuwa pia na ufugaji wa kisasa wa samaki na kadhalika.

Kiwanda hicho kipo katika eneo lenye ukubwa wa ekari 6,000 ambapo ekari 1,200 zimejengwa miundombinu ya malisho ya mifugo itakayonenepeshwa katika kipindi cha siku 90 kabla ya kuchinjwa.

Tanzania ni nchi ya tatu barani Afrika kwa wingi wa mifugo ya asili, lakini wafugaji wengi wamekuwa wakiishi maisha duni, kwani mchango wa mifugo ni mdogo sana katika kubadili maisha ya wafugaji na kuchangia ipasavyo katika pato la taifa.

Wakati katika nchi nyingine sekta ya mifugo ikitegemewa na kuwa chachu ya kuinua uchumi wa wafugaji na taifa kwa ujumla, Tanzania ilibaki nyuma, hivyo kuanzishwa kwa kiwanda cha Nguru sasa kitakuwa kimeibua fursa mpya ya kuwaondoa wafugaji katika umasikini wa kipato.

KIWANDA KINGINE
Kuibuka kwa mradi wa kiwanda cha Nguru kumekuja wakati kiwanda kingine, Meat King Limited kilichopo nje kidogo ya jiji la Arusha kikitangaza kuwa mbioni kuanza kazi na kwamba kinatarajiwa kuzalisha tani 900,000 za nyama kwa mwaka huku kikipanga kukidhi mahitaji ya soko la ndani kabla ya kuingia katika soko la jumuiya ya Afrika mashariki (EAC).

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho, Lesley De Kock, watachakata mazao ya nyama na kufungasha, lakini pia watakuwa na duka la jumla na rejareja. Awali, kiwanda hicho kilikuwa na uwezo wa kuzalisha tani 300,000 za nyama kwa mwaka, lakini sasa wamejipanga kuzalisha tani 900,000 kwa mwaka.

UZALISHAJI NYAMA DUNIANI
Mwaka 2012, nyama ya takribani tani milioni 304 ilizalishwa duniani na makadirio ya wastani wa matumizi ya nyama yalikuwa kilo 42.8 kwa kila mmoja kwa mwaka kwa wakati huo. Mwaka 2014, FAO ilikadiria ongezeko la uzalishaji wa nyama duniani kufikia jumla ya takribani tani milioni 311.6.

FAO inakadiria kwamba ifikapo Mwaka 2050 (Idadi ya watu Duniani inakadiriwa kuwa bilioni 9.6), uzalishaji wa nyama duniani utafikia tani milioni 455. Mpaka sasa, takwimu zinaonesha kuwa, mwaka 2013 Brazil iliongoza duniani kwa kuuza tani milioni 1.85 (asilimia 20.17 ya mauzo duniani), ikifuatiwa na India tani milioni 1.77 (19.26%), Australia tani milioni 1.59 (17.38%), Marekani tani milioni 1.17 (12.79%) na New Zealand, tani 528,000 (5.77%) kwa Afrika, Afrika Kusini, yenye ng’ombe milioni 14 tu, ndiyo inayoongoza, kwani iliuza nyama tani 13,000 na inashika nafasi ya 22 duniani.

MAZIWA
Uzalishaji wa maziwa Duniani unakisiwa kuongezeka kwa zaidi ya asilimia 50 kutoka tani milioni 482 Mwaka 1982 hadi kufikia tani milioni 754 Mwaka 2012. India inaongoza kwa uzalishaji maziwa duniani, takribani tani 122 kwa mwaka, sawa na asilimia 16 ya maziwa yote ya duniani. Inafuatiwa na Marekani, China, Pakistan na Brazil.

BIASHARA YA NGOZI
Ngozi za aina mbalimbali zinatokana na wanyama wanaochinjwa au kuuawa. Kati ya Mwaka 2008 na 2013, FAO inakadiria uchinjaji kwa mwaka ulikuwa hivi: kondoo 542.5 milioni na mbuzi milioni 426.6.

Afrika inakadiriwa kuwa na asilimia 15 ya jumla ya ng’ombe na takribani asilimia 25 ya kondoo na mbuzi wote duniani. Hata hivyo, mbali ya wingi huo wa mifugo, Afrika inazalisha asilimia 8 tu ya ngozi za ng’ombe na takribani asilimia 14 tu ya ngozi za kondoo na mbuzi duniani.

Idadi ya ngozi zinazozalishwa kote duniani kwa mwaka inakadiriwa kuwa takribani milioni 240. Matumizi ya kibiashara ya ngozi ni pamoja na kutengeneza viatu, mabegi, nguo, mikanda, viti, sofa na kadhalika kwa ajili ya soko la ndani na kwa masoko ya kimataifa.

Aidha, damu, mifupa na bidhaa nyingine zitokanazo na wanyama hao, zinaweza kutumika kutengeneza chakula cha mifugo, hivyo kuongeza mnyororo wa thamani wa kila kitokanacho na wanyama.

UFUGAJI WA KISASA
Kama ilivyo kwenye kilimo na uvuvi wa kisasa, hata ufugaji unahitajika kuwa wa kisasa kwa lengo la kuwa na bidhaa bora sokoni. Na ili kuufikia ubora huo, mambo kadhaa yanahitajika ambayo ni ardhi ya malisho kwa wafugaji, matumizi makubwa ya sayansi, teknolojia na ubunifu, rasilimali fedha, viwanda vya kuthaminisha na kukamilisha utengenezaji wa mazao ya mifugo, lakini pia sera na sheria za kustawisha ufugaji na wafugaji.

SEKTA YENYE NGUVU
Kwa mujibu wa Mwakilishi wa Taasisi ya kimataifa inayojihusisha na utafiti wa mifugo ya International Livestock Research Institute (ILRI) Tanzania, Amos Omore, mifugo ni sekta yenye nguvu ya kuleta mabadiliko kiuchumi.

Anasema mifugo ni rasilimali isiyoisha kwani ni jadidi na dunia nzima, watu bilioni moja huishi kwa kutegemea mifugo hasa wanawake na ajira kwa vijana. Asilimia 15 ya kalori na asilimia 25 ya protini inatokana na wanyama ambao ni muhimu katika mlo kamili na kuongeza uwezo kipato kwa idadi kubwa ya watu masikini.

Kwa mujibu wa Omore, ongezeko la thamani ya bidhaa za mifugo ni nzuri hasa kwa kilimo biashara kutokana na kwamba bidhaa sita za kimataifa zinatokana na kilimo ambacho chanzo chake ni wanyama ikiwemo (maziwa, nyama ya nguruwe, nyama ng’ombe, kuku na samaki) ambayo thamani yake inafikia Dola za Marekani bilioni 715.

Hilo si pato haba ukizingatia kuwa teknolojia inayotumika ni duni na haina ubunifu wa kina. Hata hivyo, ingawa mifugo inachangia asilimia 40 ya Pato la Taifa katika nchi nyingi ambazo ni masikini zaidi duniani, lakini zinapata asilimia 4 tu ya misaada ya maendeleo ya kilimo.

Kutokana na maelezo ya mwakilishi huyo, sekta ya mifugo Tanzania huchangia wastani wa asilimia 13 ya Pato la Taifa ambacho ni kiwango cha chini ikilinganishwa na nchi zenye mifugo wachache kama Botswana.
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top