Polisi
imewakamata wasichana wawili wa Kitanzania katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Mwalimu Nyerere Dar es Salaam, wakiwa na zaidi ya pipi 187
walizokuwa wamezimeza za madawa ya kulevya kwa ajili ya kusafirisha
nchini China.
Aidha,
polisi imemtia mbaroni, raia wa China Guoyn Shen (44), kwa kukutwa na
madini aina ya quates kilo 19 aliyokuwa akiyasafirisha kwa njia ya ndege
kuelekea China.
Wasichana
waliokamatwa Jumatano ya wiki hii saa 11:00 jioni. uwanjani hapo
walikuwa kwenye harakati za kupanda ndege ya kampuni ya ndege ya Qatar
kuelekea China kupitia Hong Kong.
Kwa
mujibu wa Mkuu wa kitengo cha kupambana na dawa za kulevya, nchini
Kamanda Godfrey Nzoa, wasichana hao ni Mariam Makuhani (29) mkazi wa
Tabata Kimanga na Khadija Shomari (30), mkazi wa Magomeni Mapipa ambao
hadi jana asubuhi walikuwa wanaendelea kuzitoa pipi hizo kwa njia ya
haja kubwa.
Alisema
Mariam kwa wakati huo (saa 5:00) alikuwa ametoa pipi 65 wakati Khadija
alifanikiwa kutoa pipi 122 ambazo zitapelekwa kwa Mkemia Mkuu wa
Serikali kwa ajili ya kubaini ni za aina gani na thamani yake.
Alisema
wasichana hao bado wapo chini ya uangalizi ambapo baada ya kumaliza
zoezi hilo wataandaliwa mashitaka yao na kufikishwa mahakamani kujibu
makosa yanayowakabili.
Kaimu
wa Viwanja vya Ndege nchini, Mratibu wa polisi, Renatus Chalya, alisema
awali baada ya wasichana hao kukamatwa, Mariam alikiri kumeza pipi 72
huku Khadija akidai alimsindikiza Mariam.
Akizungumzia
changamoto za kupambana na madawa ya kulevya, Kamanda Nzoa alisema
wasafirishaji wamekuwa wakiibuka na mbinu tofauti na wengine
wakisafirisha viatilifu vya kutengenezea dawa hizo badala ya dawa
zenyewe.
Alisema mbinu hizo zimekuwa zikifanywa kwa msimu na kutaja njia ambazo hutumiwa kuwa ni majini, viwanja vya ndege na nchi kavu.
Kufuatia
changamoto hiyo, Tanzania na nchi nyingine duniani zilishiriki mikutano
mbalimbali ambapo wa mwisho ulifanyika mwezi Oktoba mwaka huu nchini
Afrika Kusini.
Alisema
katika mkutano huo washiriki pamoja na mambo mengine walipata fursa ya
kueleza changamoto wanazokabiliana nazo kwenye mapambano dhidi ya dawa
hizo ambapo lililojitokeza ni usafirishaji wa viatilifu.
"Tuliliongelea kwa upana wake suala hili na kuafikiana kuwepo kwa sheria
kali kwa kuwa tunayoitumia kwa mfano Tanzania haiwabani sana," alisema
na kuongeza:
Alisema nchi zilizoshiriki mkutano huo zilibaini hiyo ni moja ya
changamoto hivyo wakakubaliana kutungwe sheria itakayokuwa na makali
zaidi.
Kamanda
Nzoa aliwataja Watanzania wawili waliokamatwa kwa nyakati tofauti na
viatilifu Agnes Masogange, Afrika Kusini na mwingine aliyemtaja kwa jina
moja la Sada aliyekamatwa Tanzania ambao kutokana na sheria hiyo
walilipa faini ndogo na kuachiwa huru.
Alisema sheria iliyopo inatoa nguvu kwa mamlaka ya Chakula na Dawa
(TFDA) ambapo mtu akikamatwa na viatilifu hivyo bila kibali atachukuliwa
hatua za kisheria.
Kamanda Nzoa alisema kuanzia mwezi Machi hadi Julai mwaka huu, wamefanikiwa kukamata kilo 1482 ambazo tayari zilishaharibiwa.
Alisema dawa hizo zilikamatwa kwa nyakati tofauti kwenye meli ambapo moja ilikutwa na kilo 500, nyingine kilo 300.
"Ipo
iliyokutwa na kilo 200 meli nyingine ilikutwa na kilo 182 ambapo hata
hivyo kutokana na eneo walilokutwa walishindwa kuwafikisha mahakamani
badala yake waliharibu mzigo huo," alisema.
Kwa
upande wa njia ya anga, alisema kwa mwaka huu wamefanikiwa kukamata kilo
50 bila kuzijumlisha zinazoendelea kutolewa na wasichana hao wawili
waliokamatwa Jumatano.
"Ipo
kesi ambayo ukija hapa ofisi kwangu nitakuonyesha mlolongo mzima, huwezi
amini tulikamata watu tena wakazitoa dawa hizo kwa njia ya haja kubwa
lakini mahakama iliwaachilia, kama nilivyosema tunapoenda mahakamani
tunatakiwa kuthibitisha pasipo kuacha shaka," alisema.
Kamanda
Nzoa alisema kutokana na changamoto hizo, tayari wameshawapeleka vijana
wao nchi mbalimbali na kutaja baadhi kuwa ni Afrika Kusini, Ghana,
India, Iran, Ivory Cost kwa ajili ya mafunzo maalum.
Kuhusu
Mchina aliyekamatwana madini alisema kuwa Shen alikamatwa Jumatano wiki
hii uwanjani hapo akiwa kwenye harakati za kusafirisha mzigo huo
kuelekea nchini humo.
Alisema mtuhumiwa huyo alikuwa akisafiri na ndege ya kampuni ya ndege ya Ethiopia iliyokuwa iondoke jioni ya siku hiyo.
Alisema
mtuhumiwa huyo alipokamatwa alipotakiwa kutoa kibali cha kusafirisha
mzigo huo hakuwa nacho na alipoulizwa ameyapata wapi alidai ameyanunua
kwa wananchi.
Alitaja namba za hati ya kusafiria ya mtuhumiwa huyo kuwa ni
00609687.Alisema upelelezi wa tukio hilo unaendelea ikiwa ni pamoja na
kubaini thamani ya madini hayo.
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment