Na Regina Mkonde
Rais John Pombe Magufuli ameendelea kupongezwa na wananchi pamoja na Taasisi za kiraia mbalimbali kutokana na misimamo yake na kazi kubwa anayoifanya ya kupigania rasilimali za nchi, kwa masilahi ya wanyonge na masikini.
Pongezi hizo zimetolewa kwa nyakati tofauti leo, Julai 17, 2017 jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Masjid Ridhwaa, Alhaj Suleiman Seif Nassor na aliyekuwa mgombea wa CCM wa Ubunge Jimbo la Sengerema kupitia kura ya maoni, Laurence Mabawa.
Wakati akizungumza na wanahabari, Alhaj Nassor amesema bodi hiyo imemamua kumpongea Dkt. Magufuli kutokana na kazi nzuri anayofanya tangu alipoingia madarakani.
Kwa upande wake Mabawa, amesema licha ya kumpongeza Rais Magufuli, ameandaa kampeni kabambe inayojulikana kama ‘Magufuli Baki’ inayotarajiwa kufanyika hivi karibuni kwenye mikoa yote nchini, ambapo kupitia mikutano wananchi wenye nia njema watamuomba rais abaki katika msimamo wake wa kuwatetea wanyonge na masikini.
“Kampeni ya Magufuli Baki itahusisha mikoa yote ya Tanzania kwa kuwafikia wananchi wakiwemo wanafunzi wa sekondari kwa kufanya mikutano yenye nia njema ya kumwomba Rais abaki kwenye msimamo wake, kampeni hii itawapa fursa wananchi kutoa maoni yao kuhusu utendaji kazi wake iwe kwa kupongeza au kukosoa,” amesema.
Katika hatua nyingine, Mabawa amelaani baadhi ya wanasiasa na wananchi wanaotoa lugha za maudhi na kejeli kwa watu wanaojitokeza hadharani kumpongeza Rais Magufuli na serikali yake.
“Niombe TCRA kuwachukulia hatua kali wote wanaotumia mitandao ya kijamii vibaya kwa kuwatolea maneno ya kejeli na kuudhi watu wanaojitokeza kumpongeza Rais,” amesema.
Post a Comment