Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

MENEJA WA DIAMOND APELEKWA MAHABUSU

Na Karama Kenyunko, blogu ya jamii

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam imeamuru Mkurugenzi wa Kampuni ya Tip Top Connection ya jijini Dar es Salaam, Hamis Taletale a.k.a Babu Tale,  kurudishwa Mahabusu ya polisi mpaka Msajili wa Mahakama hiyo atakaporudi kutoka Dodoma.

Amri hiyo imetolewa leo na Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Lucy Massam baada ya Babu Tale na Mhadhiri wa Dini ya Kiislamu, Sheikh Hashim Mbonde kushindwa kufikia makubaliano licha ya msajili kuwapa muda wa dakika 10 pande zote wajadiliane namna ya kulimaliza suala hilo.

Babu Tale ambaye pia ni Meneja wa mwanamuziki maarufu wa Bongo Fleva Nassib Abdul 'Diamond Platnumz', amefikishwa mahakamani hapo leo akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi kusikiliza kesi inayomkabili.

Babu Tale, amekamatwa kutokana na amri iliyotolewa Februari 16 mwaka huu na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam Wilbard Mashauri iliyoamuru mtuhumiwa huyo na ndugu yake, Idd Taletale wakamatwe.

Amri hiyo pia, ilielekeza watuhimiwa hao wakikamatwa wapelekwe Gereza la Ukonga wakiwa wafungwa wa kesi ya madai, hadi hapo Mahakama hiyo itakapotoa maelekezo mengine.Hata hivyo, mtuhumiwa Babu Tale baada ya kufikishwa mahakamani hapo jana kesi yake ilishindikana kusikilizwa kwa kuwa Msajili Mashauri yuko Dodoma kikazi.

Kutokana na kushindwa kufikia muafaka baada ya dakika hizo kumi kuisha, Msajili Massam ameamuru babu Tale arudishwe mahabusu ya polisi mpaka Msajili Mashauri atakaporudi kwa ajili ya maelekezo mengine.

Hata hivyo kipindi chote cha majadiliano Babu Tale alikuwa katika mahabusu ya mahakama hiyo wakati ndugu zake wanajadiliana na mdai wake kabla ya kuieleza mahakama muafaka watakaofikia na kisha mahakama kutoa maelekezo.

Awali Mahakama hiyo iliwaamuru watuhumiwa hao kumlipa Mhadhiri wa Dini ya Kiislamu, Sheikh Hashim Mbonde kiasi cha Sh.milioni 250 baada ya kupatikana na makosa ya ukiukwaji wa haki za hakimiliki kwa kutumia masomo yake kibiashara bila ridhaa yake kinyume cha Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki.

Katika kesi ya msingi, Sheikh Mbonde alikuwa akidai kuwa aliingia mkataba na kampuni ya kina Babu Tale (Tiptop Connection) ili wamrekodi mahubiri yake kisha wayauze na kugawana mapato.Hata hivyo baada ya kurekodi masomo saba, walimkatia mawasiliano na alipowatafuta na kukutana nao wakamweleza kuwa wameamua kuachana na mpango huo.

Sheikh Mbonde alidai kuwa akiwa kwenye mahubiri Dodoma ndipo akakutana na mikanda ya video katika mfumo wa DVD yenye mahubiri yake huku kukiwa na namba za simu za viongozi hao wa Tiptop.

Sheikh Mbonde alidai baada ya kufanya uchunguzi alibaini kuwa DVD hizo zilikuwa zikiuzwa katika mikoa mbalimbali, ndipo akawafungulia kesi ya madai ya fidia kutokana ukiukwaji wa Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki.
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top