DUNIA ina mambo! Fundi wa magari mkoani Morogoro, Julius Mavella maarufu kama Papa Mavella, Machi 5 mwaka huu, majira ya saa saba usiku, alifariki dunia baada ya pikipiki aliyokuwa akiendesha, kugongana na nyingine, wakati akimkimbia mchumba’ke baada ya kuwa amefumwa akijirusha katika Klabu ya Itigi, iliyopo Msamvu inayodaiwa kutumiwa na machangudoa.
Klabu hiyo ambayo iliwahi kuvamiwa na makachero wa kikosi maalum cha Global Publishers cha Oparesheni Fichua Maovu (OFM) na kukutana na akina dada poa wengi wakijiuza waziwazi, haipendwi na wanawake walioolewa mjini hapa kwani inaonekana kama ni hatari kwa ndoa zao.
Papa Mavella aliwasha pikipiki yake na kuondoka ukumbini hapo, kitendo kilichomfanya mwanamke huyo kumwelekeza dereva wa bodaboda aliyopanda kumfuata.
Katika kuwakimbia wasimfikie, marehemu aliamua kuvunja sheria ya usalama barabarani kwa kufuata barabara upande wa kulia badala ya kushoto, hali iliyosababisha kugongana uso kwa uso na pikipiki nyingine iliyokuwa ikitokea Dodoma na madereva wote wawili kufariki hapohapo.
Dada wa marehemu, Melle Mavella aliyekuwa akiishi na marehemu ambaye pamoja na wanafamilia wengine walirejea Machi 14, mwaka huu kutoka mazishini, alisema alikuwa akiishi vizuri na kaka yake kwani awali, alimweleza kuwa angemnunulia pikipiki ili aitumie kufanyia biashara.
Kwa upande wake, mchumba wa Papa Mavella, Aisha Nasoro alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo, alikiri kumfukuza mumewe.
”Ni kweli nilikuwa namfukuza mwanaume wangu, lakini kwa bahati mbaya, alipita ‘saiti’ ambayo siyo yake na kugongana uso kwa uso na pikipiki nyingine, nilishuhudia mume wangu na dereva wa pikipiki nyingine wakifa papo hapo na juzi tumetoka Urambo kumzika,” alisema kwa njia ya simu.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.
GPL
Post a Comment