Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Serikali Yahimiza Halmashauri Kubuni Miradi Ya Kimkakati Ili Kujiongezea Mapato

Serikali imeeleza kuwa Uchukuaji wa baadhi ya vyanzo vya mapato katika halmashauri ulifanyika kwa mujibu wa Sheria ya Bajeti iliyoridhiwa na Bunge ya mwaka 2015 kifungu namba 58 ikiwa na lengo la kuongeza ufanisi wa ukusanyaji na matumizi ya mapato hayo.

Hayo yameelezwa Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) alipokuwa akijibu swali la Msingi la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Suzana Mgonukulima, aliyependekeza itungwe sheria ya kuibana serikali ikiwa haitarejesha fedha zilizotokana na vyanzo vya mapato vilivyopo kwenye Miji, Halmashauri, Manispaa na Majiji zitakazokusanywa na kuwekwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.

Akijibu swali hilo Dkt. Kijaji alisema kuwa  kwa mujibu wa kifungu cha 44 cha Sheria ya Bajeti, mgao wa fedha kutoka katika Mfuko Mkuu wa Serikali utazingatia  bajeti iliyoidhinishwa, upatikanaji na mtiririko wa fedha, utekelezaji mpango wa ununuzi na mpango wa kuajiri hivyo hakuna Fungu litakaloruhusiwa kufanya matumizi ya aina yoyote mpaka kuwe na fedha za kulipa matumizi husika.

“Usimamizi wa  Mapato hayo kwa mujibu ya Sheria ya Bajeti ya Mwaka 2015 Kifungu namba 58  unazingatia mapato kuingizwa kwenye Sheria ya Kuidhinisha Matumizi ya Fedha za Serikali, aliyepewa mamlaka ya kukusanya mapato ya Serikali atawajibika katika ukusanyaji wenye ufanisi, utunzaji wa hesabu, utoaji wa taarifa na kuzuia ufujaji wa mapato”, alisema  Dkt. Kijaji. 

Alisema Usimamizi wa mapato na matumizi umebainishwa vizuri na hivyo hakuna haja ya kutunga sheria nyingine ya kuibana Serikali ikiwa haitapeleka fedha kwenye, Miji, Halmashauri, Manispaa na Majiji.

Aidha akijibu swali la nyongezai la Mhe.  Mgonukulima  kuhusu kutokuwa na usawa katika utoaji wa fedha za maendeleo katika Wilaya, Dkt. Kijaji alisema kuwa tarehe 5 Mei, 2018 Serikali ilizindua Mkakati wa kuziwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa kutekeleza miradi yenye kuchochea upatikanaji wa Mapato ili ziweze kujitegemea  hivyo ni vema Halmashauri zikabuni miradi ya maendeleo itakayoongeza mapato.

Akieleza kuhusu utaratibu wa malipo ya Kodi ya Majengo kutoka katika Halmashauri nchini Naibu Waziri Dkt. Kijaji, alisema kuwa Majengo yasiyofanyiwa tathimini yanatakiwa kutozwa kiwango sawa cha Sh. 10,000 na majengo ya juu (ghorofa) yanatakiwa kutozwa kiwango sawa cha Sh. 50,000.

Alisema majengo yaliyofanyiwa tahimini ndiyo yanayoweza kulipiwa kodi zaidi ya kiasi hicho, hivyo wakurugenzi wa Halmashauri wanapaswa kuzingatia utaratibu huo uliowekwa katika ukusanyaji wa kodi hiyo, alieleza Dkt. Kijaji.

Imetolewa na;
Benny Mwaipaja
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango

HIVI NDIVYO WATENDAJI WATATU KITUO CHA UWEKEZAJI NCHINI WALIVYOPATA AJALI MBAYA NA KUFARIKI DUNIA

21
Na Ripota Wetu,Globu ya jamii

WATENDAJI watatu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania(TIC)  wakiwamo Wakurugenzi wawili na Meneja mmoja wamefariki dunia baada ya gari waliyokuwa wakisafiria kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma kupata ajali ya kugongana uso kwa uso na Scania katika Kijiji cha Msoga Chalinze mkoani Pwani.

Akizungumza na Michuzi Blog kwa njia ya simu leo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Jonathan Warioba amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusababisha vifo hivyo ambapo amesema  Zacharia Kingu na Martin Masalu ambaye ni Meneja wa Utafiti walifariki papo hapo wakati Said Amir alifariki dunia baada ya kufikishwa 
hospitali kwa matibabu.

Amefafanua ajali hiyo imehusisha magari mawili ambayo ni gari namba STK 923 aina Toyota Landcruiser mali ya Wizara ya Viwanda,Biashara na Uwekezaji iliyokuwa ikiendeshwa na Priscus Peter(23) mkazi wa Dar es Salaam kugongana na scania namba T 620AQV/ T 407DBY.

"Mei 21 mwaka huu saa 15:30 maeneo ya Msoga-Chalinze katika barabara ya Msoga/Msolwa Wilaya ya kipolisi Chalinze Mkoa wa Pwani, gari hizo ziligongana na kusababisha vifo na majeruhi,"amefafanua Kamanda Warioba.

Ameongeza majeruhi katika ajali hiyo ni Godfrey Kilolo(45) na dereva Priscus Peter ambao walipelekwa Hospitali ya Msoga kwa matibabu na tayari wameruhusiwa na miili ya marehemu imehifadhiwa Hospitali ya Tumbi Kibaha mkoani Pwani.

Eneo la ajali hiyo kwa mujibu wa taarifa limekaguliwa na na  ASP. Solla-Occid(W) akisaidiwa na INSP.MS Mkojera - DTO (W) Chkojera pamoja na F7704 PC Hamza ambaye ndiye mpelelezi wa tukio hilo.Hata hivyo juhudi za zinafanyika kumpata dereva wa Scania kwa mahojiano zaidi kwani alikimbia baada ya ajali kutokea.

Uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha  ajali ni uzembe  wa dereva wa gari namba STK 5923 T ambaye alihama kutoka upande wake na kwenda kugongana na Scania hiyo.
23w
Pichani ni  gari namba STK 5923 aina Toyota Landcruiser mali ya Wizara ya Viwanda,Biashara na Uwekezaji iliyokuwa ikiendeshwa na Priscus Peter(23) mkazi wa Dar es Salaam kugongana na scania namba T 620AQV/ T 407DBY na kupelekea vifo na majeruhi. 
index

Vigogo CHADEMA wavuliwa Uanachama

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema, Patrick Ole Sosopi, ametangaza kuwafuta uanachama wanachama wawili wa chama hicho.

Waliofutwa uanachana ni pamoja na aliyekua Naibu Katibu Mkuu Bara, Getrude Ndibalema na Mwenyekiti wa Bavicha mkoa wa Kilimanjaro, Dickson Kibona.

Akizungumza jana Mei 21, katika mkutano na waandishi wa habari jijini Arusha, Ole Sosopi alisema kwamba uamuzi huo umekuja baada ya kufuata taratibu zote za kuwahoji kupitia tume iliyoundwa.

Alisema viongozi hao wamehojiwa baada ya kuwepo tuhuma za usaliti ambalo ni kosa kubwa kwenye chama hicho.

Sosopi amesema Bavicha imeridhia kuwaondoa wanachama hao baada ya kujiridhisha kwa makosa waliyoyafanya.

Wabunge Wa CUF Wamfagilia Rais Magufuli ....Wasifu Kasi Yake Na Waziri Mkuu Ya Uletaji Maendeleo

WABUNGE watatu kutoka Chama cha Wananchi (CUF) mikoa ya Lindi na Mtwara wamepongeza kasi ya utendaji kazi ya Rais John Pombe Magufuli katika kutatua kero za wananchi wa mikoa hiyo.

Wabunge hao Bw. Selemani Said Bungara (Kilwa Kusini), Bw. Zuberi Mohammed Kuchauka (Liwale) na Bw. Maftaha Abdallah Nachuma (Mtwara Mjini) walitoa pongezi hizo jana, (Jumatatu, Mei 21, 2018) wakati walipopewa nafasi ya kusalimia wananchi kwenye mikutano ya hadhara ambayo Waziri Mkuu alihutubia.

Akiwa wilayani Lindi, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mara baada ya kuzindua kituo cha kuunganisha umeme wa gridi ya Taifa katika kijiji cha Mahumbika, aliwapa fursa wabunge wote alioambatana nao katika ziara hiyo maalum kwa ajili ya uzinduzi wa miundombinu ya nishati kwa mikoa ya Kusini.

Akizungumza na wananchi na viongozi wa taasisi mbalimbali mkoani humo waliohudhuria uzinduzi huo, Mbunge wa Kilwa Kusini, Bw. Bungara ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wabunge wanaotoka Mkoa wa Lindi alisema analishukuru Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuisimamia vizuri Serikali ya CCM.

“Faida ya demokrasia ya vyama vingi ni kwamba CCM bila CUF, CCM hakuna na CUF bila CCM, kama ambavyo hakuna Simba bila Yanga wala hakuna Yanga bila Simba. Tuwe kitu kimoja tu, Kusini kwanza, vyama baadaye!” alisisitiza.

Alitumia fursa hiyo kumpongeza Waziri Mkuu kwa juhudi zake za kuwaunganisha wabunge wa mikoa ya Kusini bila kuwabagua au kujali itikadi zao.

Naye Mbunge wa Liwale, Bw. Kuchauka alisema: “Niwapongeze wewe Waziri Mkuu pamoja na Mheshimiwa Rais Magufuli kwa yale ambayo mnayasimamia na mnaamini kwamba yataleta ukombozi kwa wananchi wa Tanzania. Lazima nikiri kwamba wakati mnazindua sera ya uchumi wa viwanda, nilikuwa siamini katika hiyo sera yenu kwa sababu niliona ni moja ya mbinu zenu za kututenga sisi watu wa mikoa ya Kusini.”

“Niliona hivyo kwa sababu nilijiuliza unawezaje kuwa na uchumi wa viwanda wakati huna nishati ya uhakika ya umeme? Sasa nimeona mwanga kwamba mikoa ya Kusini nayo inaweza kushiriki kwenye uchumi wa viwanda,” alisema huku akishangiliwa.

Alisema hivi sasa hakuna asiyeona mambo yanayotekelezwa na Serikali ya awamu ya tano kwani dunia yote imekuwa kama kijiji na lolote linalofanywa na Mhe. Rais au Waziri Mkuu hakuna asiyejua. “Lolote analolifanya Mheshimiwa Rais au wewe Waziri Mkuu Watanzania wote watalijua, hakuna asiyeliona. Hivi sasa hakuna haja ya kubishana nani kafanya nini, jambo kubwa ni kuungana na tuangalie Tanzania yetu. Vyama vyote baadaye, Kusini kwanza,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Mbunge wa Mtwara Mjini, Bw. Maftaha alisema mwaka 2006 baada ya kuhitimu kidato cha sita, alipangiwa afanye mafunzo ya ualimu kwa vitendo katika shule ya sekondari Mingoyo, eneo la Mnazi Mmoja lakini alitafuta nyumba ya kuishi yenye umeme hakupata.

“Wakati ule nyumba zenye umeme zilikuwa hazizidi hata 10, na kulikuwa na simba na wadudu wa kila aina. Leo nafarijika kuona kwa kasi ya ajabu, ninyi viongozi tuliowapa dhamana, mnatumia rasilmali za nchi hii, mnasambaza umeme kwa wananchi wa mikoa ya Kusini, na pale Mnazi Mmoja leo hii, umeme siyo tatizo tena.”

Wabunge wengine waliofuatana na Waziri Mkuu ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na Mbunge wa Mtwara Vijijini, Bibi Hawa Ghasia; Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Bi. Hamida Mohammed Abdallah (Viti Maalum). Mbunge wa Nachingwea, Bw. Hassan Elias Masala, Mbunge wa Nanyamba, Bw. Abdallah Dadi Chikota.

Waziri Mkuu alizuru pia mkoa wa Mtwara na kukagua ujenzi wa bandari, ukarabati wa mabomba ya kupokelea mafuta, matenki ya kuhifadhi mafuta, kuzindua upanuzi wa kituo cha kufua umeme kwa kutumia gesi asilia na kuzungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa bandari.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,

Ripoti ya Ufisadi Mali za CCM Yatua kwa Rais Magufuli

Tume ya kuhakiki mali za Chama Cha Mapinduzi (CCM), iliyoundwa na Rais John Magufuli, imebaini madudu ukiwamo utapeli na usimamizi mbaya wa mali hizo.

Kamati hiyo iliyoundwa na Rais Magufuli kukagua mali za chama hicho, imefanya kazi hiyo kwa miezi mitano ambapo imekusanya taarifa, kuhakiki na kuchambua taarifa na nyaraka zenye maelezo kuhusu idadi, aina na hali ya mali zinazomilikiwa na kusimamiwa na chama hicho.

Akikabidhi ripoti hiyo kwa Rais John Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Dk. Bashiru Ally, amesema tume yake pia ilibaini usimamizi mbovu wa mali za chama.

Akielezea namna tume hiyo ilivyofanya kazi, Dk. Bashiru amesema pamoja na mambo mengine, tume iliangalia vyanzo vya udhaifu wa mifumo na taratibu za usimamizi wa mali, imekusanya ushauri mbalimbali na kutoa mapendekezo ya mikakati na ushauri wa kusimamia mali za chama.

Katika ripoti hiyo, Dk. Bashiru ameeleza tume imebaini uwepo wa upotevu mkubwa wa mali za chama uliosababishwa na mikataba mibovu, ubadhirifu, wizi, usimamizi mbaya wa mali, utapeli na ukosefu wa maadili katika uendeshaji wa miradi ya chama.

“Uhakiki huo umefanyika kwa kutembelea maeneo yenye mali za chama, kuwahoji watu mbalimbali wakiwamo viongozi waliohusishwa na mali zilizokuwa zikihakikiwa, upitiaji wa nyaraka na kufuatilia uhalisia katika ofisi za mamlaka husika, kufanya uchambuzi wa taarifa na kutoa mapendekezo,” amesema.

Kwa upande wake Rais Magufuli ameipongeza tume hiyo kwa kazi kubwa iliyoifanya na amesema ripoti hiyo itawasilishwa katika vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM kwa ajili ya kufanyiwa uamuzi.

“Nilipokuwa nateua tume hii, nilikuwa najua ugumu wa kazi, nilikuwa najua kuwa mtapata shida kwenda kuwahoji watu licha ya kwamba niliwapa uhuru wa kumhoji mtu yeyote na mmefanya kazi nzuri sana, kilichobaki sasa ni kuifanyia kazi” amesema Rais Magufuli.

Hamisa Mobetto afunguka kuhusu kupigwa na mama DiamondMwanamitindo Hamisa Mobetto amefunguka kuhusu taarifa zilizodai kuwa amepigwa na mama mzazi wa Diamond Platnumz, Sanura Kassim ‘Sandra’.

Hapo jana katika uzinduzi wa kipindi cha Nyumba ya Imani cha Wasafi TV, Hamisa alipata time ya kuzungumza na waandishi wa habari na kusema jambo hilo ni binafsi zaidi ila kugombana kwa binadamu ni kitu cha kawaida.

“Hilo siwezi kuliongelea, yeah!. is too person, is too private, is too family. Hata vikombe kwenye kabati vinagong’ana, so sisi binadamu vinaweza kutokea,” amesema.

Alipoulizwa iwapo kwa sasa yeye na mama Diamond wana maelewano mazuri, alijibu; ‘Sina kinyongo na mtu, sina bifu na mtu, mimi am just fine, may be yeye mwenyewe sio upande wangu wa kuweza kuelezea,’.

Taarifa za Hamisa kupigwa na mama Diamond zilianza kusambaa Jumatatu ya wiki iliyopita, May 14, 2018 ambapo usiku ya jana yake Hamisa na Diamond walihudhuria katika uzinduzi wa filamu ya Aunt Ezekiel ‘Mama’ na baada ya hapo anadaiwa waliongozana hadi Madale kwa kina Diamond ambapo ndipo kisa hicho kinadaiwa kutokea.

Serikali Yatoa Bilioni Kumi Kuboresha Reli Ya Tazara

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa shilingi bilioni kumi kwa ajili ya kuboresha reli ya TAZARA nchini ili iweze kujiendesha kwa kusafirisha mizigo na abiria kati ya Tanzania na Zambia, kuzalisha faida na kuchangia ukuaji wa uchumi na pato la taifa kwa nchi mbili.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua njia ya reli ya TAZARA na miundombinu yake katika eneo la Mlimba, Morogoro hadi Makambako, Iringa lenye umbali wa kilomita 163.

Mhandisi Nditiye amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ametoa fedha hizo ili kuhakikisha kuwa Tanzania tunafanya majukumu yetu kwa upande wetu ambapo reli ya TAZARA inaendeshwa na nchi mbili.

Ameongeza kuwa fedha hizo zitatumika kununua traction motors saba zenye gharama ya shilingi bilioni saba kwa ajili ya kufunga kwenye injini 42 za vichwa vya treni ili kuhakikisha kuwa treni inasafiri kwa usalama na kwa uhakika kutoka eneo moja kwenda lingine bila kuharibika njiani na kuchelewesha safari za abiria au mizigo ya wateja ambapo itaboresha utendaji kazi wa TAZARA na hivyo kuongeza makusanyo ya mapato yake.

Amefafanua kuwa, fedha nyingine kiasi cha shilingi bilioni tatu zitatumika kukununua mtambo na vitendea kazi kwa ajili ya kiwanda cha kutengeneza kokoto cha TAZARA ambapo kokoto hizo zinatumika kuimarisha njia ya reli ya TAZARA na miundombinu yake, kuzuia mmomonyoko wa udongo, kuota kwa nyasi na kupunguza mtetemo wakati wa safari.

Wakati wa ziara yake, Mhandisi Nditiye amebaini wizi wa vyuma kwenye njia za reli, madaraja na miundombinu yake ambapo vinaibiwa na hivyo kuhatarisha usalama wa safari na kuharibu miundombinu hiyo. “Naitaka TAZARA mshirikiane na SUMATRA na muwe walinzi wa reli hii na miundombinu yetu”, amesema Nditiye.  

Pia, ametoa rai kwa wanunuzi wa vyuma chakavu kuwa waangalifu wasinunue vyuma vya reli. Ameilekeza TAZARA kwa kutumia kitengo chake cha Polisi kufanya ziara za kushtukiza kwa wanunuzi na wafanyabiashara wa vyuma chakavu, wakibainika na kuthibitika wananunua vyuma hivyo, wakamatwe na sheria ichukue mkondo wake.

Vile vile ameilekeza SUMATRA kuendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye njia ya reli ili kuhakikisha usalama wa usafiri wa njia ya reli.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TAZARA, Dkt. Befram P. Kiswaga ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha hizo ambazo zitawawezesha kufanya ununuzi wa traction motors hizo na mitambo ya kiwanda cha kutengeneza kokoto ili TAZARA iweze kujiendesha kwa faida kama ilivyokuwa hapo awali badala ya kuitegemea Serikali kulipa mishahara ya wafanyakazi wake kama inavyofanyika hivi sasa.

Mkaguzi Usalama wa Reli wa SUMATRA, Mhandisi Hanya Mbawala amemweleza Mhandisi Nditiye kuwa nia yao ni kulinda usalama wa usafiri wa njia ya reli ambapo ripoti ya SUMATRA ya hivi karibuni imeonesha kuwa hakuna hali hatarishi yoyote kwenye njia hiyo ambayo itazuia reli ya TAZARA kwa sasa kusafirisha abiria na mizigo. Aidha, amemhakikishia Mhandisi Nditiye kuwa, wataendelea kufanya ukaguzi huo mara kwa mara na kuielekeza TAZARA hatua stahiki za kufuata pale inapohitajika kuhusu usalama wa reli na miundombinu yake.

Reli ya TAZARA ina jumla ya kilomita 1,860 kutoka Dar es Salaam, Tanzania hadi Kapirimposhi, Zambia. Kati ya kilomita 1,860, jumla ya kilomita 975 zipo nchini Tanzania kati ya Dar es Salaam na Tunduma, mpakani mwa Tanzania na Zambia. Pia, reli ya TAZARA ina jumla ya madaraja 318 ambapo madaraja 272 yapo nchini Tanzania na 46 yapo upande wa Zambia. Aidha, ina mahandaki yapatayo 23, na 22 kati ya hayo yapo Tanzania na handaki moja lipo mpakani mwa Tanzania na Zambia na kati ya hayo, mahandaki 18 yapo katika eneo la Mlimba, Morogoro hadi Makambako, Iringa.

Kwa upande wa Tanzania, reli ya TAZARA ina daraja refu kuliko yote, daraja Na. 117 la Ruipa lililopo kati ya eneo la Mlimba na Makambako lenye urefu wa mita 502. Pia, katika eneo hilo, kuna daraja Na. 190 lenye kina kirefu cha mita 50 kwenda chini lililopo eneo la Kitete. Vile vile, kuna handaki refu kuliko mahandaki yote, handaki la Iganga lenye urefu wa mita 817. Reli ya TAZARA inaendeshwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia ambapo ilikamilika ujenzi wake na kuanza kutumika mwaka 1970.

MAGAZETI YA LEO JUMANNE MEI 22, 2018 YA NDANI NA NJE YA TANZANIA
BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top