Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

CECAFA CHALLENGE CUP KUANZA RASMI NOV 24

Uganda, mabingwa wa kihistoria wa Challenge


NA MAHMOUD ZUBEIRY

MICHUANO ya soka ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama CECAFA Challenge Cup, mwaka huu itafanyika mjini Kampala, Uganda kuanzia Novemba 24 hadi Desemba 8.

Kampuni ya Bia Afrika Mashariki (EABL), kupitia bia yake ya Tusker Lager, ndio wadhamini michuano hiyo kwa dau lao la dola za Kimarekani 450,000 walizitoa kwa ajili ya michuano ya mwaka huu ya Kombe la CECAFA –Tusker Challenge Cup.

Katibu wa CECAFA, Nicholas Musonye alisema mapema tu wakati wa maandalizi ya awali ya michuano hiyo, kwamba lengo la michuano hiyo ni kuzisaidia maandalizi timu za Afrika Mashariki na Kati katika kuwania tiekti ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014 nchini Brazil.

Udhamini wa mwaka huu huo ni ongezeko la aslimia 5, kutoka michuano ya mwaka jana mjini Dar es Salaam, ambayo Uganda waliibuka mabingwa.

Ni udhamini ambao utahusu usafiri, malazi na huduma nyingine, wakati jumla ya dola za Kimarekani 60.000 zitakuwa kwa ajili ya zawadi, bingwa akipewa dola 30.000, mshindi wa pili dola 20.000 na dola 10.000 mshindi wa tatu. Kama ilivyo ada, mechi zote za michuano hiyo zitaonyeshwa na Televisheni ya Super Sport ya Afrika Kusini.

Michuano hiyo huandaliwa na CECAFA, Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati, ambalo lina wanachama 12.

Japokuwa ukanda wa CECAFA ndiyo eneo linalojikongoja kwa sasa katika soka ya kimataifa, lakini ukweli ni kwamba, mpira wa miguu barani Afrika, ulianzia ukanda wa Afrika Mashariki.

Michuano ya kwanza kabisa mikubwa barani Afrika, ilihusisha mataifa manne, Kenya, Uganda, Tanganyika (sasa Tanzania Bara) na Zanzibar, ikijulikana kwa jina la Kombe la Gossage.

Michuano hiyo ya Gossage ambayo sasa imekuwa Kombe la Challenge, ilifanyika mara 37 kuanzia mwaka 1926 hadi 1966, ilipobadilishwa jana na kuwa michuano ya wakubwa ya soka kwa mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, ilifanyika mara saba kati ya mwaka 1965 na 1971, ilipozaliwa rasmi CECAFA Challenge.

Tanganyika ilianza kushiriki michuano hiyo tangu mwaka 1945, wakati Zanzibar ilijitosa miaka minne baadaye, 1949.

Michuano hiyo ilikuwa ikidhaminiwa na bepari aliyekuwa akimiliki kiwanda cha sabuni, William Gossage, aliyezaliwa Mei 12 mwaka 1799 na kufariki dunia Aprili 9, mwaka 1877.

Michuano hiyo mikongwe zaidi barani, imekuwa ikiandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), ikihusisha timu za taifa za ukanda huo.

Hadi inafikia tamati michuano ya Gossage, Uganda ilikuwa inaongoza kwa kutwaa taji hilo, mara 22, ikifuatiwa na Kenya iliyotwaa mara 12 na Tanzania mara tano.

Mwaka 2005, michuano hiyo ilifanyika chini ya udhamini wa bilionea wa Ethiopia mwenye asili ya Saudi Arabia, Sheikh Mohammed Al Amoudi na kupewa jina la Al Amoudi Senior Challenge Cup, lakini sasa Tusker ndiyo mambo yote.



MABINGWA CHALLENGE;

Mwaka Bingwa

1973 Uganda

1974 Tanzania

1975 Kenya

1976 Uganda

1977 Uganda

1978 Malawi

1979 Malawi

1980 Sudan

1981 Kenya

1982 Kenya

1983 Kenya

1984 Zambia

1985 Zimbabwe

1986 Haikufanyika

1987 Ethiopia

1988 Malawi

1989 Uganda

1990 Uganda

1991 Zambia

1992 Uganda

1993 Haikufanyika

1994 Tanzania

1995 Zanzibar

1996 Uganda

1997 Haikufanyika

1998 Haikufanyika

1999 Rwanda B

2000 Uganda

2001 Ethiopia

2002 Kenya

2003 Uganda

2004 Ethiopia

2005 Ethiopia

2006 Zambia

2007 Sudan

2009 Uganda

2009 Uganda

2010 Tanzania Bara

2011 Uganda



KUNDI A: Uganda, Kenya, Ethiopia na Sudan Kusini

KUNDI B: Tanzania, Sudan, Burundi na Somalia

KUNDI C: Malawi, Eritrea, Rwanda na Zanzibar



RATIB KUNDI A:

Novemba 24, 2012:

Ethiopia v Sudan (Saa 9:00 Alasiri)

Uganda v Kenya (Saa 12:00 jioni)

Novemba 27, 2012:

Sudan Kusini v Kenya (Saa 9:00 Alasiri)

Uganda v Ethiopia (Saa 12:00 jioni)

Novemba 30, 2012:

Kenya v Ethiopia (Saa 9:00 Alasiri)

Sudan Kusini v Uganda (Saa 12:00 jioni)



RATIBA KUNDI B:

Novemba 25, 2012:

Burundi v Somalia (Saa 9:00 Alasiri)

Tanzania v Sudan (Saa 12:00 jioni)

Novemba 28, 2012:

Somalia v Sudan (Saa 9:00 Alasiri)

Tanzania v Burundi (Saa 12:00 jioni)

Desemba 1, 2012:

Sudan v Burundi (Saa 9:00 Alasiri)

Somalia v Tanzania (Saa 12:00 jioni)



RATIBA KUNDI C:

Novemba 26, 2012:

Zanzibar v Eritrea (Saa 9:00 Alasiri)

Rwanda v Malawi (Saa 12:00 jioni)

Novemba 29, 2012:

Malawi v Eritrea (Saa 9:00 Alasiri)

Rwanda v Zanzibar (Saa 12:00 jioni)

Desemba 1, 2012:

Malawi v Zanzibar (Saa 9:00 Alasiri)

Eritrea v Rwanda (Saa 12:00 jioni)



ROBO FAINALI:

Desemba 3, 2012

Mshindi Kundi C vs Mshindi wa Pili Kundi B (Saa 10:00 jioni)

Mshindi Kundi A vs Mshindi wa Tatu Bora wa pili (Saa 1:00 usiku)

Desemba 4, 2012 (16:00):

Mshindi Kundi B vs Mshindi wa Tatu Bora wa kwanza (Saa 10:00 jioni)

Mshindi wa Pili Kundi A vs Mshindi wa Pili Kundi C (Saa 1:00 usiku)



NUSU FAINALI:

Desemba 6, 2012

Nusu Fainali ya Kwanza (Saa 10:00 jioni)

Nusu Fainali ya Pili (Saa 1:00 usiku)



MSHINDI WA TATU:

Desemba 8, 2012

Waliofungwa Nusu Fanali (Saa 10:00 jioni)



FAINALI:

Desemba 8, 2012

Walioshinda Nusu Fainali (Saa 1:00 usiku)

 

WASIFU WA TIMU ZINAZOSHIRIKI TUSKER CHALLENGE 2012


Kenya
NYOTA WA HARAMBEE:
Kenya ambayo timu yake ya taifa inaitwa Harambee Stars, imeshiriki mara tano fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, ingawa haijawahi kuingia raundi ya pili zaidi ya kunusa na kutolewa. Ilishiriki michuano ya kuwania kucheza fainali za Kombe la Dunia kwa mara yakwanza mwaka 1974 na imeendelea hadi fainali za mwaka huu zilizofanyika Afrika Kusini, lakini haijafanikiwa kufuzu. Mwaka 2004, FIFA iliisimamisha Kenya kushiriki michuano yote ya kimataifa kwamiezi mitatu, kufuatia serikali ya nchi hiyo kuingiliwa masuala ya soka, lakini kifungo hicho kilisitishwa baada ya nchi hiyo kukubalia kufuata masharti ya shirikisho hilo la kimataifa la soka. Oktoba 25, mwaka 2006, Kenya ilisimamishwa tena katika soka ya kimataifa kwa kushindwa kutekeleza makubaoliano yaliyofikiwa Januari mwaka huo ya kutatua matatizo yaliyokuwa yametawala kwenye shirikisho lao la soka, hata hivyo walipomaliza matatizo yao adhabu yao ilifutwa. Kenya waliosyhiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mara nne, katikamiaka ya 1988, 1990, 1992 na 2004 na mara zote wakitolewa raundi ya kwanza, ni mabingwa mara tano wa Kombe la Challenge la CECAFA katika miaka ya 1975, 1981, 1982, 1983 na 2002, wakati pia imeshika nafasi ya pili mara nne.

Sudan
MWEWE WA JANGWANI;
TIMU ya taifa ya Sudan inajulikana kwa jina la utani kama Sokoor Al-Jediane Kiarabu, Kiingereza Desert Hawks, yaani Mwewe wa Jangwani. Hii ilikuwa moja ya nchi tatu tu nyingine zikiwa ni Misri na Ethiopia zilizoasisi Kombe la Mataifa Huru ya Afrika mwaka 1957 na ilifanikiwa kushinda taji hilo mwaka 1970, wakiwa wenyeji, baada ya kuwafunga Ghana 1-0 kwenye fainali, wakitoka kuifunga Misri 2-1 katika Nusu Fainali. Sudan ni miongoni mwa timu kongwe barani Afrika na ilikuwa ina historia ya utajiri miaka ya 1950 na 1970. Sudan pia ilishika nafasi ya pili kwenye michuano hiyo katika fainali za mwaka 1959 zilizofanyika mjini Cairo, Misri zikishirikisha nchi tatu, yani mbali na wenyeji, pia walikuwapo Ethiopia. Ilishika tena nafasi ya pili katika fainali za mwaka 1963 baada ya kufungwa na Ghana 3-0 kwenye fainali, wakati 1957 ilikuwa ya tatu. Sudan pia wametwaa mara tatu Kombe la Challenge katika miaka ya 1980, 2006 na 2007 na wamekuwa wa pili mara mbili 1990 na 1996 na washindi wa tatu mara mbili pia, 1996 na 2004.

Uganda
KORONGO WA KAMPALA;
Uganda ambayo timu yake ya taifa inaitwa The Cranes, yaani Korongo hawajawahi kufuzu kwenye fainali za Kombe la Dunia, na kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika matokeo yao mazuri kabisa ni kushika nafasi ya pili mwaka 1978, baada ya kufungwa na wenyeji Ghana 2-0 mjini Accra. Lakini Korongo wa Uganda wanajivunia kuwa timu iliyotwaa mara nyingi zaidi taji (mara 12) Kombe la Challenge, katika miaka ya 1973, 1976, 1977, 1989, 1990, 1992, 1996, 2000, 2003, 2008, 2009 na 2011 na pia imeshika nafasi ya pili mara nne.

Rwanda
NYIGU WA KIGALI;
Rwanda ambayo timu yake ya taifa inaitwa Amavubi Kinyarwanda, yaani (The Wasps), yaani Nyigu, pamoja na kwamba walichelewa kuingia kwenye soka ya kimataifa kutoka muda mrefu wa kutokuwa na amani nchini mwao, lakini tangu wamefunguliwa milango wanaonekana kuwa tishio. Walikuwapo kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2004 nchini Tunisia na wana taji moja la Challenge walilotwaa mwaka 1998, wakati wamekwishakuwa washindi wa pili mara tano katika miaka ya 2003, 2005, 2007, 2009 na 2011 na wameshika nafasi ya tatu mara tatu katika miaka ya 2001, 2002 na 2006.

Burundi
MBAYUWAYU WA BUJUMBURA;
Burundi ambayo timu yake ya taifa inaitwa Int’hamba Murugamba Kirundi, Les Hirondelles Kifaransa au The Swallows Kiingereza yaani Kiswahili Mbayuwayu, hii kwa pamoja na Eritrea na Djibouti ndio zinaweza kuwa zenye mafanikio duni kabisa katika ukanda wa CECAFA, kwani hazijawahi kushinda hata taji moja la Challenge wala hata kunusa kwenye fainali za Matafa ya Afrika.
Lakini ni nchi ambayo imebarikiwa wachezaji wenye vipaji, ingawa wengi baadaye huikana nchi hiyo na kuchukua uraia wa nchi jirani, kwa mfano Nonda Shabani aliyehamia DRC na Hamadi Ndikumana aliyejivika Unyarwanda.

Somalia
MABAHARIA WA MOGADISHU;
Somalia ambayo timu yake ya taifa inafahamika kama The Ocean Stars, yaani Nyotan wa Bahari ni nchi mwanachama wa mashirikisho ya mawili ya soka; kwanza Afrika (CAF) na pili Urabuni (UAFA). Haijawahi kufuzu kwenye fainali za Kombe la Dunia wala Mataifa ya Afrika na kwa sasa imezuiwa kucheza mechi nyumbani kwake, Somalia kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe inayoendelea. Lakini Somalia inapendewa soka yake maridadi, japokuwa haizalishi matokeo mazuri.

Zanzibar
MASHUJAA WA VISIWANI;
Zanzibar ambayo timu yake ya taifa inajulikana kama Zanzibar Heroes, au Mashujaa wa Visiwa vya Karafuu, kwenye soka ya kimataifa bado ni sehemu ya Tanzania, ingawa inapigania uanachama wake FIFA, ili iwe taifa kamili katika dunia ya soka. Lakini kwa CECAFA, Zanzibar inaingia kama nchi na imewahi kutwaa ubingwa wa michuano hiyo mwaka 1995, ikiwafunga wenyeji Uganda 1-0.
Zanzibar pia imewahi kuingia Nusu Fainali mara sita na mbili ikishika nafasi ya tatu, wakati michuano ya mwaka huu, inaeonekana kuwa na kikosi imara zaidi.

Ethiopia
SWALA DUME;
Ethiopia ambayo timu yake ya taifa inajulikana kama The Walya Antelopes, mchanganyiko wa maneno mawili, la Kiingereza na Kihabeshi, lenye maana ya ‘Swala dume’ ni miongoni mwa nchi tatu pamoja na Misri na Sudan zilizoasisi michuano ya Mataifa Huru ya Afrika mwaka 1957 na wakafanikiwa kutwaa taji hilo mwaka 1962 walipokuwa wenyeji, ingawa baada ya muongo huo, ilipoteza makali yake.
Baada ya kuzisakosa kidogo fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 2004, kwa kuzidiwa pointi tatu tu, baada ya kufungwa na Guinea, Ethiopia mwakani itashiriki tena fainali hizo nchini Afrika Kusini, baada ya miaka 31. Inajivunia pia kutwaa mataji ya Challenge katika miaka ya 1987, 2001, 2004 na 2005.

Tanzania Bara
NYOTA WA KILIMANJARO;
Tanzania, ambayo kabla ilikuwa ikijulikana kama Tanganyika, timu yake ya taifa inaitwa Kilimanjaro Stars- ingawa nje ya michuano ya CECAFA inatambulika kama Taifa Stars, kwa sababu inaungana na Zanzibar kuunda timu moja.
Haijawahi kushiriki fainali hata moja za Kombe la Dunia, lakini inajivunia kucheza fainali moja za mwaka 1980 za Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Nigeria, sambamba na kutwaa mara tatu Kombe la Challenge katika miaka ya 1974, 1994 na 2010 na kushika nafasi ya pili mara tano.
Malawi
MWALE WA NYASA;
Malawi iliyokuwa ikijulikana kama Nyasaland kabla ya mwaka 1966, ambayo timu yake ya taifa inaitwa The Flames, yaani Mwale (mwako wa moto) hawajawahi kufuzu kwenye fainali za Kombe la Dunia, lakini wameshiriki fainali mbili za Kombe la Mataifa ya Afrika katika miaka ya 1984 na 2010, mara zote wakiishia raundi ya kwanza.
Mafanikio yao makubwa katika soka ya kimataifa ni kushika nafasi ya tatu katika Michezo ya Afrika mwaka 1987. timu hiyo ambayo kwa sasa iko chini ya kocha mzalendo Kinnah Phiri, imewahi kushika nafasi ya pili mara mbili katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Kusini mwa Afrika (COSAFA), wakati kabla ya kuhami huko, ikiwa bado mwanachama wa CECAFA, ilitwaa Kombe la Challenge mara tatu katika miaka ya 1978, 1979 na 1988 na pia kushina nafasi ya pili mara tatu. Imekuja tena kushiriki Challenge mwaka huu kama mgeni mualikwa.

Sudan Kusini
NYOTA ANGAVU WA SUDAN KUSINI;
Sudan Kusini, au Bright Star, yaani Nyota Angavu kwa jina la utani, huyu ni mwanachama mpya kabisa wa CECAFA, nchi iliyojigawa kutoka Sudan ambayo sasa inatambulika katika familia ya soka kama taifa kamili. Kwao hizi zitakuwa fainali za kwanza kabisa za Challenge. Sudan Kusini rasmi ilicheza mechi yake ya kwanza ya kimataifa Julai 10, mwaka huu na kutoka sare ya 2-2 na Uganda nyumbani. Hii ni kuashiria kwamba, pamoja na upya wao si timu ya kubeza kwa kitendo cha kutoka nguvu sawa na mabingwa watetezi wa michuano hii.

Eritrea
WAVUVI WA BAHARI NYEKUNDU ERITREA;
Imekosekana katika fainali mbili zilizopita za Challenge kutokana na tabia ya wachezaji wake kuzamia nchi za watu wanapokwenda kucheza mechi. Wachezaji wanne wa klabu ya Red Sea FC walizamia Nairobi baada ya mechi ya Ligi ya Mabingwa na wengine 12 wa timu ya taifa wakazamia Tanzania mwaka 2007 baada ya Challenge. Wachezaji wengine sita walizamia Angola Machi mwaka 2007 baada ya mechi ya kufuzu ya Kombe la Mataifa ya Afrika. Wachezaji wengine watatu zaidi walizamia Sudan, hivyo Eritrea ikajitoa kwenye soka ya kimataifa kwa ujumla ili kutafuta dawa ya kukabiliana na tatizo hilo na sasa serikali ya nchi hiyo inamtaka kila mchezjai kuweka nakfa 100,000 (fedha za kwao) kabla ya kusafiri nje. Timu yao ya taifa inaitwa Red Sea Boys, yaani vijana wa Bahari Nyekundu na haina cha kujivunia kwenye mashindano haya, ikiwa ilicheza mechi yake ya kwanza ya kimataifa Juni 26, mwaka 1992 na kutoka 1-1 na Sudan.

VIWANGO VYA UBORA FIFA
NCHI NAFASI
Uganda 86
Malawi 101
Ethiopia 102
Sudan 102
Rwanda 122
Burundi 128
Kenya 130
Tanzania 134
Zanzibar 134
Somalia 193
Eritrea 192
Sudan Kusini 200
(Viwango hivi vimetoka mwezi huu)
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top