
WANAUME HUPENDA KUOA MWANAMKE WA AINA HII
Habari za wiki hii mpenzi msomaji. Mimi namshukuru
Mungu kwa kuweza kunikutanisha na nyinyi kupitia safu hii ambayo pamoja na mambo
mengine nazungumzia juu ya mada mbalimbali ambazo zinagusa maisha yetu ya kila
siku.
Wiki hii nitazungumazia juu ya aina ya wanawake ambao
wanaume wengi hupendelea kuoa. Wanaume wengi wanapofikia hatua ya kuoa si kwamba
wanakurupuka tu na kuoa mwanamke yeyote mwenye sura nzuri, bali huchukua muda
wao mwingi kuchunguza mambo mengi juu ya wake ambao wanadhani kwamba wanaweza
kuwa pamoja kwa kipindi chote cha maisha.
Wanawake wengi wanajisahau na kudhani kwamba kitu
kinachoweza kuwafanya wakapata wachumba ni uzuri hivyo kupoteza muda wao
kujichubua na kujiremba ili wawavutie wanaume bila kujua kwamba kuolewa ni zaidi
ya uzuri.
Hali sasa hivi imebadilika ni tofauti na kipindi cha
nyuma ambapo ukiwa na sura nzuri na umbo la kuvutia basi una asilimia 100 za
kuolewa. Utafiti ambao nimeufanya unaonesha kwamba zaidi ya uzuri wa tabia na
umbo, kuna kuna sifa nyingine za msingi ambazo mwanamke anatakiwa kuwa nazo ili
aweze kuwa katika mazingira mazuri ya kupata mchumba wa kumuoa kiasi kwamba
asipokuwa nazo ataishia kuchezewa tu lakini haitatokea mtu kumtakiwa kwamba
anataka kumuoa.
MWEYE MAPENZI YA KWELI
Lengo kubwa la mwanaume kuoa ni kutaka kupata mapenzi
ya kweli kutoka kwa mwanamke na ikiwezekana waweze kupata watotoa ambapo watoto
mara ndio wamekuwa furaha ya ndoa. Wapo wanawake wengine ambao wanonesha wazi
kutokuwa na mapenzi ya kweli bali wanakuwa na mapenzi ya kuzuga. Wanachotaka wao
aidha kupata umaarufu tu kwamba yuko na mtu fulani ama kuweza kupata pesa
alizonazo mwanaume lakini sio kwamba ana mapenzi ya dhati kutoka moyoni mwake.
Mwanamke asiye na mapenzi ya dhati utamgundua tu, muda mwingi utamuona macho
yake yako kwenye mfuko wa mwanaume. Akiona kwamba mfuko umetuna utaona anaonesha
mapenzi ya hali ya juu lakini pindi hali inapokuwa kubwa mbaya kifedha mapenzi
yanaanza kufifia.
Kwanini wanaume wanapenda wana wake wenye mapenzi ya
dhati kutoka mioyoni mwao na si kutokana na fedha walizonazo? Hii inatokana na
ukweli kwamba maisha siku zote yanabadilika, kama waswahili wanavyosema, kuna
kupanda na kushuka.Sio kwamba kila siku utakuwa na maisha mazuri na kama
itatokea hivyo basi ushukuru mungu.Hivyo basi mwanamke wa kuoa lazima afahamu
hivyo na awe tayari kuonesha mapenzi yake ya dhati wakati wote wa maisha yao na
si kwa kipindi fulani tu cha neema.
Si hivyo tu pia asilimia kubwa ya maisha ya ndoa
yanatawaliwa na mapenzi, kwa hiyo nyanja hiyo inakuwa ya msingi sana kwa wanaume
wengi kuiangalia ili wasije wakajikuta wanaoa mwanamke ambaye baada ya muda
mapenzi yanakwenda likizo hali ambayo inaweza kuwafanya wasiishi maisha ya raha
mustarehe.
WENYE TABIA NZURI
Tabia njema ndio silaha ya maisha, ukiwa na tabia nzuri
kila mtu atakupenda, hiyo ni katika maisha ya kawaida. Lakini linapokuja suala
na kuoa tabia inakuwa kitu cha awali sana kungaliwa na hiyo inaweza kuwa na
ukweli kwa sababu wapo wasichana wazuri wenye mvuto wa aina yake na maumbile
mazuri, lakini wanakosa wanaume wa kuwaoa, ukiuliza kwani utaambiwa anatabia
mbaya. Naweza kusema hilo ndilo limekuwa tatizo kubwa kwa baadhi ya wanawake
kukosa wanaume wa kuwaona. Hakuna mwanaume hata mmoja kati ya wale ambao
nimejaribu kuongea naye ambaye ameonesha kulidharau suala hilo la
tabia.
Si hivyo tu wapo wanaume ambao wameingia kichwa kichwa
na kuoa kwa kuangalia sura tu bila kujali tabia, matokeo yake baada ya siku
chache yanatokea machafuko ya aina yake hali ambayo imepelekea kuvunjika kwa
ndoa kutokana na tabia mbaya alizonazo mwanamke.
WENYE UCHU NA MAENDELEO
Hivi karibuni kumekuwepo na mabadiliko ya aina yake kwa
wanaume, wengi sasa hivi hawapendi kabisa kuoa mwanamke ambaye hana kazi yaani
'golikipa'. Kama atakuwa hana kazi basi awe na uchu wa maendeleo kwa kujituma
kufanya kazi mbalimbali za kimaendeleo kama vile kilimo kwa wale walio vijijini
na biashara ndogondogo kwa wale ambao wako mijijini na hata vijijini. Ile dhana
ya kusema mwanamke ni mama wa nyumbani wa kukaa na kujipodoa akimsubiria mwnaume
arudi amstarehesha, sasa hivi imepitwa na wakati. Wanaume wengi wanapenda
wanawake ambao ni wahangaikaji, wenye ndoto za maendeleo katika maisha yao. Hata
kama watakuwa si wafanyakazi lakini wawe wenye kutoa ushauri kwa waume zao juu
ya jinsi gani wafanye ili wafanikiwe.
WASIOPENDA MAKUU
Kuna wanawake wengine wanakuwa na tabia za ajabu sana
kiasi kwamba yaweza kuwa kero kwa wanaume. Wapo wanawake ambao wanapenda makuu
bila kujali hali halisi ilivyo. Kuna wanawake naweza kusema wana tamaa, kila
wikiendi utamsikia "leo tunakwenda wapi dear?" Akimuona rafiki yake kanunua
simu ya laki tatu na yeye utamsikia akisema, ‘na mimi naomba uninunulie simu
kama ya Grace’. Ukienda naye Pub anakuambia, "mimi sinywi pombe za chupa
natumia za kopo tena Heineken’. Yeye hajali kiasi cha pesa mwanaume alicho
nacho na usipotekelezea anachukia na anaweza hata kupunguza
mapenzi.

Wanawake kama hawa wako katika mazingira magumu sana ya
kuweza kupata wanaume wa kuwaoa. Mara nyingi katika maisha fedha huzungumza,
kama mwanaume atakuwa na pesa ya kutosha itakuwa rahisi sana kwa mwanamke kupata
kila atakachopenda lakini si kwa kumwambia mimi nataka kitu fulani.Mwanaune
mwenyewe utamsikia akisema, ‘unataka nikununulie simu ya aina gani, au leo
unataka twende wapi?’ hapo ndipo utakuwa na nafasi ya kusema, ‘mimi nataka
uninunulie simu kama ya fulani ama leo nataka twende sehemu
fulani.’
Wanaume ni warahisi sana wa kuwapatia wale ambao
wanatarajia kuwaoa chochote ambacho watahitaji kama tu pesa haitakuwa tatizo.
Kitu ambacho kinawaudhi wanaume wengi ni ile tabia ya mwanamke kupenda mambo
makubwa bila kuangalia uwezo uliopo kwa mwanume.
Kuna wanawake wengine wao si wasemaji kabisa, yeye
anasubiri leo amemletea hiki, anapokea na kushukuru, kesho akiambiwa twende
beach anakubali. Au wengine wanasubiri mpaka waulizwe wanataka nini, ndio
wanasema.
Sisemi kwamba uwe mkimya tu hata kama una shida ya kitu
fulani na unafahamu kwamba ukimweleza mwenza wako anaweza kukusaidia, hapana!
kama unaona kwamba uwezekano wa kupata kile ambacho unakihitaji upo mweleze kwa
utaratibu naamini atakuelewa na kukutimizia.Tabia ambayo hawaipendi wanaume
wengi ni ile ya kulazimisha ufanyiwe kitu fulani wakati inawezekana uwezekano
haupo.
WAVUMILIVU
Wapo wanawake ambao sio wavumilivu kabisa katika
maisha.Tunajua kwamba maisha siku zote hayatabiriki, yanaweza kutokea matatizo
ya kiafya ama kifedha.Huu ndio wakati wa kuona uvumilivu wa mtu.Kama mwanamke
anatarajia kwamba siku zote ni za raha tu na pindi matatizo yanapotokea
anachukua uamuzi wa kumtoroka mwanume, huyo siyo mwanamke wa kuoa.Wangapi leo
hii huwatoroka waume zao pindi inapotea kuumwa, kufilisika ama kupatwa na tatizo
lolote ambalo kwa namna moja ama nyingine yanaweza kuwafanya maisha yao
kutingishika?
Uvumilivu kwa mwanamke utakuwepo kama tu atakuwa na
mapenzi ya dhati kama nilivyozungumza hapo awali. Mwanamke mweye mapenzi ya
dhati ni lazima atakuwa mvumilivu na atakuwa tayari kuishi katika maisha ya aina
yoyote, yawe ya raha ama ya starehe.Hawa ndio wale ambao wanaume wengi
wengependa kuwa nao maishani mwao.
Licha ya kupenda kuoa wanawake amabo wana tabia
hizo nilizozitaja hapo juu, wanachukizwa sana na wanawake ambao wanavijitabia
vidogo vidogo ambavyo kimsingi havikubaliki katka jamii.Tabia hizo ni kama
wambea, wasio wakweli na wawazi, wasioridhika, wagumu kusamehe na wapesi wa
kuchukia, wagomvi na wenye roho ya kwanini.
Utafiti huu umefanyikwa kwa baadhi ya wanaume ambao
wanatarajia kuoa wanawake ambao wanaoishi katika maeneo mbalimbali jijini
Dar-es-Salaam. Kwa maana hiyo basi hiyo iwe changamoto kwa wanawake. Wajue
kwamba wanaume wanafurahi kuwa na wanawake wa aina gani. Hata kama utakuwa
umeshaolewa, kama kuna wakati kunakuwa na kutokuelewana baina yenu, chunguza
yawezekana kwamba unakosa mojawapo ya tabia ambazo nimezitaja hapo juu. Waweza
kubadilika kwani inawezekana.
Via http://irenemwamfupejamii.blogspot.com/p/mahusiano.html
Via http://irenemwamfupejamii.blogspot.com/p/mahusiano.html


Post a Comment