Loading...
Ziara ya Tizeba yaibua mazito
**************
NAIBU Waziri wa Uchukuzi, Charles Tizeba ameitaka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na Mamlaka ya Anga Tanzania (TCAA) kuhakikisha ndege haziruki bila kuwa na taarifa maalum za kiusalama ikiwemo ya hali ya hewa.
Dk Tizeba alitoa maagizo hayo baada ya kufanya ziara katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere Dar es Salaam jana, kuelezwa kuwa zipo ndege zinazoruka bila kuwa na taarifa hiyo kutoka Mamlaka ya hali ya hewa ya kiwanja hicho, badala yake kutumia za nchi zilipotoka au zinapokwenda.
Taarifa hiyo, Flight Forder, huonyesha hali ya hewa na kila ndege na kisheria ndege kabla ya kuruka lazima iwe na taarifa hiyo ambayo ina umuhimu mkubwa kwa kuwa hali ya hewa hubadilika kila wakati.
Katika ziara hiyo Naibu waziri huyo alitembelea mtambo wa kuongozea ndege DVOR/DME na ofisi zake, ofisi za kitengo cha Hali ya Hewa cha uwanja huo, mitambo ya kuongozea ndege, ofisi ya rada, kikosi cha zimamoto na uokoaji pamoja na eneo la jenereta za uwanja huo.
Akizungumza wakati akiwa katika ofisi za hali ya hewa, Tizeba aliwabana kwa maswali wafanyakazi wa ofisi hiyo huku akitaka kupewa maelezo ya kina kuhusu usalama wa ndege hasa hali ya hewa inapokuwa mbaya.
Baada ya maelezo yake marefu, Msimamizi wa Kituo Kikuu cha kuongoza ndege, Elieza Mwalutende alisema kuwa zipo ndege zinazoruka bila kuwa na taarifa hiyo, kwamba zinaweza kutumia taarifa za nchi zilipotoka huku akitolea mfano uwanja wa ndege wa Nairobi, Kenya.
“Wapo wanaotumia taarifa za Nairobi kwa sababu inawezekana taarifa za hali ya hewa zikawa hazijabadilika katika muda waliotoka Dar es Salaam kurudi tena Nairobi” alisema Mwalutende.
Hali hiyo iliibuka baada ya msimamizi huyo kueleza kuwa kama ndege itaruka bila kuchukua taarifa hizo, huwa zinabaki katika uwanja huo na hakuna hatua zozote zinazochukuliwa kwa ndege iliyoruka bila kuwa na taarifa hiyo.
“Hivi sheria inasemaje, anayetakiwa kuchukua taarifa hizi ni nani piloti au” alihoji Tizeba na kufafanua, “Jamani hebu muwabane hawa watu kama sheria zipo wazi mnaweza kuwazuia kurusha ndege mpaka watakapochukua taarifa hii.”
Alisema kuwa wanatakiwa kuwa wakali kwa sababu kama likitokea tatizo shutuma zote humwangukia waziri wa wizara husika.
“Nasema hivi kwasababu likitokea jambo hapa tunaolaumiwa ni sisi, sio nyie, hivyo lazima mjipange kukabiliana na watu hawa na ikibidi hata kuwanyang’anya leseni” alisema Tizeba na kuongeza;
“Hakikisheni ndege kabla ya kuruka inakuwa imekamilisha taratibu zote za kiusalama.”
Alisema kuwa tatizo kama hilo pia lipo Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na kusema kuwa linatakiwa kufanyiwa kazi ili kuhakikisha kuwa linapotokea tatizo kila kitengo kiwe kimewajibika ipasavyo.
Pia Tizeba alikitaka kikosi cha zimamoto na uokoaji katika uwanja huo kuboresha utendaji wake wa kazi ikiwa ni pamoja na kuwa na maji ya kutosha kwa ajili ya kuzima moto pale linapotokea tatizo.
“Muda wa kuzima moto kwa kutumia lita 10,000 za maji ni dakika mbili ila kupakia hayo maji katika magari ni dakika 10 hadi 15, hii ni changamoto mnatakiwa kuifanyia kazi kwa kuwa muda wa kupakia ni mrefu na kama moto unaendelea kuwaka ni wazi kuwa utateketeza vitu vingi” alisema Tizeba.
Alikitaka kikosi hicho kuhakikisha kuwa kinakuwa na maji ya kutosha katika matenki yake yenye uwezo wa kuhifadhi lita 450,000 za maji, pamoja na kuwa na pampu za kutosha kwa ajili ya kusukumia maji hayo.
Katika majumuisho ya ziara yake Tizeba alisema mradi wa upanuzi wa kiwanja cha ndege (Terminal III) ambao mwekezaji aliyechukua tenda hiyo alijitoa dakika za mwisho, hivi sasa serikali imeanza kutenga fedha kwa ajili ya upanuzi huo na ipo katika hatua za kutafuta mzabuni.
Alisema kuwa pia Serikali inajipanga kutafuta fedha kwa ajili ya kuwalipa wananchi wa eneo la Kitunda wanaotakiwa kuhamishwa katika maeneo yao kupisha upanuzi wa kiwanja hicho.
“Tathimini ilifanyika mwaka 1997 na kipindi hicho watu hawa walitakiwa kulipwa Sh7bilioni, lakini kwa kuwa hawakulipwa fedha hizo sasa zimeongezeka mpaka kufikia Sh14bilioni” alisema Tizeba na kuongeza;
“Siwezi kusema watalipwa lini kwa kuwa hili ni jambo ambalo linatakiwa kupendekezwa katika bajeti ili fedha ziweze kutafutwa.”
Naibu waziri huyo pia aligusia suala la kampuni ya ndege ya Fastjet ambayo ndege zake zinaanza kuruka leo na kuongeza kuwa Serikali itahakikisha kuwa inatoa huduma nzuri.
“Kama mnavyojua ndege hizi gharama yake ya usafiri ipo chini hivyo tutahakikisha kuwa gharama hiyo ndogo haigeuki kuwa kero kwa abiria” alisema Tizeba.
Alisema kuwa pamoja na kukuta mapungufu madogo madogo katika uwanja huo, amefurahishwa na utendaji wake wa kazi, kwamba mambo mengi yanafanywa kwa ukamilifu.
BLOG RAFIKI
-
-
-
Duniani Leo2 hours ago
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
Post a Comment