Na Charles Charles
“KUZUNGUKA huku na huko kwa CCM ni kutuiga sisi.
Tumeanza muda mrefu baada tu ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010”, ndivyo anavyosema
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod
Slaa.
Anaongeza kwamba “Chadema ni mwalimu” huku Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kikiwa mwanafunzi anayefuata nyayo kwa mambo yanayofanywa na
chama chake hicho. Alikuwa akizungumza na gazeti moja la kila siku nchini
kufuatia ziara iliyofanywa hivi karibuni na Katibu Mkuu wa CCM, Kanali
Abdulrahman Kinana katika mikoa minne ya Arusha, Geita, Mtwara na
Rukwa.
Siku chache baadaye, yeye mwenyewe alifanya ziara katika
majimbo matatu ya Temeke, Kigamboni na Kinondoni jijini Dar es Salaam na kukumbana
na hali ngumu kuliko wakati wote uliopita.
Tatizo hilo liliambatana na ‘kudoda’ kwa harambee ya
kuchangia kile kinachoitwa kuwa ni Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) iliyofanyika
jijini Mwanza, na kukitia chama hicho hasara ya shilingi milioni
tisa.
Wakati hayo yakiendelea, Katibu wa Halmashauri Kuu ya
Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye aliibua tuhuma kwa Dk. Slaa
kuwa pamoja na kuwashambulia sana viongozi wenzake wilayani Temeke akisema ni
mamluki wa CCM, yeye mwenyewe ana kadi ya chama hicho kinachotawala, jambo
alilokiri ni kweli na ataendelea kuitunza katika maisha yake
yote.
Tayari hali hiyo imeibua mtafaruku katika chama chake
ambapo kuna wanachama, viongozi na wafuasi wake hivi sasa hawana tena imani naye
na kuanza kumtilia wasiwasi kwa kusema inawezekana pia ndiye anavujisha siri
nyingi za Chadema kwa watu wasiohusika.
Wanadai hata siasa zake za vurugu, uchochezi na uvunjaji
wa sheria kwa makusudi unalenga kuifanya Chadema ichukiwe na wananchi. Anataka
ionekane kuwa inahamasisha umwagaji wa damu, mkakati ambao unafanyika chini kwa
chini kwa kisingizio cha M4C ili wananchi wasigundue.
Nashukuru kwamba hatimaye wengi wameanza kukielewa chama
hicho na siasa zake za kitapeli. Wameanza kukitenga wakiwemo viongozi wake
waandamizi kama wenyeviti na makatibu wa
wilaya, mikoa, madiwani na kadhalika.
Wamo kwa mfano aliyekuwa Katibu wa Chadema wa Mkoa wa
Morogoro, Abel Luanda; aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema wa Wilaya ya Morogoro,
Rajabu Ali; aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema wa Wilaya ya Iramba, Mkumbo;
waliokuwa madiwani wa Arusha Mjini ambao ni Rehema Mohammed (Viti Maalum), Frank
Takachi (Kata ya Olasiti), Simba Salum (Kata ya Kati) na viongozi wengine
lukuki.
Akihutubia mkutano wa hadhara wa CCM kwenye Uwanja wa
Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, Rehema alisema wazi kwamba Chadema ni kama kampuni binafsi ya Dk. Slaa na hivyo anaweza kufanya
lolote, wakati wowote na mahali popote ili kukidhi matakwa yake mwenyewe kwa
kutumia kisingizio chochote.
Alisema amekuwa akitimua viongozi na kuweka wengine
jinsi anavyotaka kwa kuwatuhumu kuwa ni mamluki wa CCM, vinginevyo huwatwisha
lawama kwamba wanavunja Katiba ya Chadema ambayo hata hivyo haipo matawini,
majimboni, wilayani na mikoani isipokuwa kwake mwenyewe.
Ndiyo maana alikwenda akavuruga uteuzi wa mgombea nafasi
ya Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza kwa kuwapelekea
mgombea ambaye alimteua yeye jijini Dar es Salaam. Aligoma kumtambua diwani
aliyegombea kwa njia zote halali, akashinda kura za maoni za ndani ya chama
akidai kuwa alishavuliwa uanachama.
Akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji
cha Ndago wilayani Iramba wiki tatu zilizopita, Mkumbo alisema ameamua kuacha
uenyekiti wa wilaya wa Chadema na kuingia CCM ili apone moyo wake kuliko
kuendelea kunyanyaswa kisiasa na viongozi wake wakuu.
Alisema hawezi kuendelea kuwa mwanachama na hata
kiongozi wa Chadema katika ngazi yoyote “kwa vile ni chama kilichojaa majungu,
fitina na chuki nyingi”.
Madai hayo yanafanana pia na yale yaliyotolewa na
aliyekuwa Katibu wa Chadema wa Mkoa wa Morogoro, Abel Luanda alipohutubia
mkutano wa hadhara wa CCM uliofanyika kwenye Uwanja wa Mashujaa mjini
humo.
“Ndani ya Chadema tuliingia kwa bahati mbaya. Ilikuwa
kama uko barabarani unasubiri gari na linalotokea unapanda, lakini ukishakuwa
ndani unagundua kuwa ni mkweche na kushuka ili usubiri jingine. Tumeshuka na
tumepanda gari la kweli linaloitwa CCM”, alisema wakati alipokaribishwa
kuzungumza ili kuwawakilisha wenzake wote na kuendelea:
“Nilishikilia chama kizima mkoani, nawahakikishia kuwa
hakuna cha maana kinachoendelea kule. Ndani ya Chadema hakuna sera za kumkomboa
mlalahoi, badala yake kuna udikteta tu unaofanywa na viongozi wa ngazi za
juu”.
Hatua ya kuanza kusambaratika kwa Chadema ilithibitika
pia katika ziara ya siku tatu ya Dk. Slaa wilayani Temeke na Kinondoni jijini
Dar es Salaam .
Alikuwa akiwashutumu viongozi wenzake kuwa ni mamluki wa CCM kwa sababu tu
mahudhurio aliyoyakuta huko ni hafifu.
Mathalani, Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chadema wa Jimbo
la Kinondoni walimsotesha ukumbini akiwasubiri kuanzia saa 4.00 asubuhi hadi saa
6.47 mchana alipochoka, akafungua kikao hicho na kuzungumza na hao wachache
waliofika baada ya wao pia kubembelezwa sana kwa kupigiwa simu zao za
mikononi.
Badala ya wajumbe 130 waliotakiwa kuhudhuria ili kujua
ni kitu gani wanaambiwa na bosi wao, wale waliofika mkutanoni hadi wakati huo
walikuwa chini ya 50 tu huku wakionekana kutokuwa tayari kumsikiliza kwa muda
mrefu isipokuwa vinginevyo.
“Chadema ni chama ambacho kinajiandaa kushika dola mwaka
2015, endapo hali hii ya wajumbe kutafutana kwa simu itaendelea ni hatari wakati
wa kuunda Baraza la Mawaziri”, alisema na kukiri: “Bila kujipanga wakati huu
hakika hali ni ngumu huko tunakokwenda”.
Nimekuwa nawaambia rafiki zangu kuwa tokea mfumo huu wa
vyama vingi vya siasa nchini ulipoanza tena mwaka 1992 ili kukidhi matakwa ya
Ibara ya 3(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , hakuna mpinzani aliyewahi kuwa ‘lulu’
kwa wafuasi wake kama aliyekuwa Mwenyekiti wa
Taifa wa chama cha NCCR – Mageuzi, Augustine Mrema.
Aliaminiwa na kuungwa mkono kila mahali mijini na
vijijini. Aliteka hisia za wengi kuanzia wazee, kina mama na vijana, matajiri na
masikini, wasomi pamoja na makundi mengine.
Ndiyo maana gari lake anapomaliza kuhutubia mikutano ya
hadhara hasa mijini kama Dar es Salaam lilikuwa likisukumwa na mamia ya vijana,
tena kwa hiari na matakwa yao wenyewe hata kwa zaidi ya saa nzima mpaka
wanapokuja kusambaratishwa na polisi waliofanya hivyo ili kumlinda dhidi ya
vibaka, wezi na waporaji wengine linapoanza giza.
Lakini alipotamba kwa miaka minne akiwa katika hali hiyo
kuanzia mwaka 1995 – 1999, Mrema aligundulika kuwa ni ‘msanii’, muongo, mzushi,
mchochezi na mtu anayependa zaidi kusifiwa binafsi akitumia kila aina ya ujanja
wa kisiasa kwa kuwadanganya wafuasi wake.
Hapo ndipo umaarufu wake wote uliposambaratika kama
kishada kilichokwenda harijojo na kubaki na kikundi kidogo cha watu wenye
malengo yao
binafsi. Hao bado wanaendelea kumuunga mkono hadi leo na baadhi yao wapo radhi na tayari hata kumfia utadhani kupe
linavyong’ang’ania ngozi ya mnyama hususan ng’ombe, mbuzi ama kondoo bila
kuiachia hata kama haina damu tena au tayari
ameshakufa!
Hivyo ndivyo wanavyofanya wafuasi wa Chadema wakiwemo
hadi wasomi, ngumbaru na kadhalika. Wapo ambao pia wamejitokeza kuthibitisha
umahiri wao wa kuitetea kwa uongo, uzushi na majungu ya aina
zote.
Wanafanya hivyo kwa kupewa matumaini ‘hewa’ na viongozi
waandamizi wa chama hicho wakiongozwa na Dk. Slaa mwenye uwezo mkubwa wa
ghiliba, uzushi na kufanya kila aina ya siasa za ‘kisanii’.
Wafanya hivyo kwa kusingizia jambo lolote, wakati wowote
na mahali popote ili mradi tu wanakidhi matakwa yao wenyewe, watu ambao siku zote wanaishi kwa
kutegemea majungu, umbeya na uzandiki wa namna yoyote ile dhidi ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM), serikali na viongozi wake.
Wamekuwa mahiri wa kuhubiri siasa za kikabila, kikanda
na kadhalika kwa kutaka Tanzania itenganishwe kwa utawala wa kimajimbo, ule
ambao Mchagga au Mpare kutoka Kilimanjaro hataweza tena kupata uongozi wowote
katika mikoa ya Kigoma, Kagera, Mara au Ruvuma.
Itakuwa marufuku kwa Msukuma kutoka Mwanza, Simiyu,
Shinyanga au Tabora kushika uongozi wa ngazi yoyote katika mikoa kama ya Njombe,
Iringa, Mbeya, Rukwa, Katavi, Dodoma , Lindi, Mtwara, Pwani, Tanga na
kadhalika.
Hata hivyo hali hiyo imekuwa kinyume baada ya miaka
miwili tu ya wanachama, viongozi na wafuasi wa Chadema kudanganywa na kuamini
uongo, lakini hivi sasa wameanza kujua ukweli.
Mbali na viongozi waliohama katika mikoa ya Arusha,
Singida na Morogoro, watu kama Naibu Katibu
Mkuu (Tanzania Bara), Zitto Kabwe naye haelewani kabisa na Mwenyekiti wa Taifa,
Freeman Mbowe kutokana na kila mmoja kutaka ateuliwe yeye kuwa mgombea urais wa
chama hicho mwaka 2015.
Mbali na hao, Afisa Mwandamizi wa Kurugenzi ya Sera na
Utafiti, Mwita Waitara na Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (Bavicha),
Juliana Sonza nao hawaelewani na Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza hilo, John
Heche.
Tayari mgogoro huo pia umeanza kuenea nchini ambapo kwa
mfano, Katibu wa Chadema wa Mkoa wa Mbeya, Eddo Mwamalala amesimamishwa uongozi
kwa sababu anapinga udikteta, lakini viongozi wa Bavicha wa Mkoa wa Mwanza na
sehemu nyingine wanamtaka Dk. Slaa ajiuzulu kwa madai kuwa anakivuruga chama
hicho.
Ndiyo maana sasa amechanganyikiwa kiasi cha kupayuka
bila mpangilio wowote mdomoni ikiwemo kudai eti CCM inapofanya ziara zake
inakuwa inaiiga Chadema, jambo ambalo hata mwendawazimu hawezi
kuliamini.
Haiwezekani kwa namna yoyote kuwa viongozi wa CCM ambayo
ilianzishwa mwaka 1977 wawe hawajafanya kabisa ziara mpaka walipoiga Chadema
wiki tatu zilizopita!
Ndiyo maana Dk. Slaa sasa na ‘vigogo’ wenzake wa kitaifa
wamechanganyikiwa baada ya kuanza kususiwa mikutanoni huku viongozi wengine
wakisema wamechoshwa na udikteta, kuburuzwa kusikoisha na siasa za kitapeli.
Ndiyo maana sasa wamechanganyikiwa kuona chama hicho
kinakosa mpaka wachangiaji katika harambee zake kama ilivyotokea majuzi jijini Mwanza, kikatumia shilingi
milioni 15 kugharamia maandalizi, lakini kikachangiwa shilingi milioni sita
tu.
Tayari wimbi kubwa la wanachama, viongozi na wafuasi wa
Chadema linazidi kukimbilia CCM baada ya kuchoshwa na siasa za fitina, uzushi,
uongo na kila aina ya ghiliba tokea kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa rais,
wabunge na madiwani wa mwaka 2010.
Wanasema waziwazi kuwa “imetosha”, na sasa ‘arobaini’ ya
Chadema hatimaye imewadia!
Mwandishi wa makala hii ni Katibu Msaidizi, Idara ya
Siasa na Uhusiano wa Kimataifa ya CCM. Anapatikana kwa Simu Na. 0659 220 220 na
0762 633 244
Post a Comment