Rais wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amesema hakuna hila
yoyote katika nia ya kutaka marekebisho matatu kwenye katiba kabla ya uchaguzi
na kuwataka wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF kuridhia mabadiliko hayo kwa maslahi
ya maendeleo ya mchezo huo.
Tenga
alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kufafanua juu ya
waraka wa kuomba ridhaa ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF kuridhia mapendekezo
matatu ya mabadiliko ya katiba yanayohusu uingizaji wa kipengele cha utoaji
leseni kwa klabu (Club Licensing); kuundwa kwa Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi wa
TFF na kuondoa nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais wa TFF.
Hatua ya
kutuma waraka wa kuomba ridhaa ya mabadiliko hayo imetafsiriwa tofauti na baadhi
ya wadau, wengine wakisema ni mbinu za uongozi wa sasa kutaka uendelee kukaa
madarakani wakati wengine wakitaka ufafanuzi wa vipengele
hivyo.
“Hakuna
hila hata kidogo. Yote ni mambo ya maendeleo na nia yetu ni kufanikisha ili
mambo yaendelee,” alisema Rais Tenga kwenye ukumbi wa mikutano wa
TFF.
“Tusifikie
sehemu tukaanza kulaumu kwa nini mtu ametaka maelezo. Lakini sikutarajia kuwa
mtu wa mpira akiambiwa hili ni agizo la FIFA (Shirikisho la Kimataifa la Mpira
wa Miguu), atasita; akiambiwa hili ni agizo la CAF (Shirikisho la Mpira wa Miguu
Afrika), atasita, au akaambiwa huu ni uamuzi wenu wenyewe,
akasita.”
Tenga
alisema nia ya Kamati ya Utendaji ya TFF ilikuwa ni kuitisha Mkutano Mkuu kwa
ajili ya mabadiliko hayo ya katiba, lakini akasema
baada ya
kutafakari kwa kina na kuangaliwa uwezo wa Shirikisho, Kamati iliona haiwezi
kuitisha mikutano miwili kwa sasa kwa kuwa TFF haina
fedha.
“Tumetoa
maelezo kuwa tunafahamu kuwa katika mazingira ya kawaida tungeitisha mkutano
mkuu; tuje tuzungumze na baadaye siku ya pili watu waondoke halafu tuwaite tena
kwa ajili ya mkutano wa uchaguzi,” alisema Tenga ambaye alibainisha kuwa gharama
za chini za mkutano mkuu wa TFF ni kati ya sh. milioni 90 na sh. milioni
110.
“Lakini
tumeeleza bayana kuwa uwezo huo hatuna, tungelikuwa nao wala tusingefika mahali
hapa; vijana wetu wanahangaika hadi tunatafuta watu watusaidie. Kwa hiyo
tukasema kuna dhambi gani kuwa wakweli. Katiba inasema mkitaka kufanya
mabadiliko ya katiba, itisheni mkutano mkuu. Unaita Mkutano Mkuu kwa sababu
gani, ili mlete wajumbe wa mkutano mkuu ambao ndio watakaopitisha mabadiliko
hayo na ndio maana tumeona dhana hiyo ya kutuma waraka.”
Kuhusu
mabadiliko hayo, Tenga alifafanua kuwa maagizo kuhusu utoaji leseni kwa klabu
(Club Licensing) na kuundwa kwa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi wa TFF yalitolewa
mwishoni Julai, ikiwa ni baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji cha Julai na
hivyo suala hilo kulazimika kuzungumzwa kwenye kikao cha
Septemba.
Alisema:
”Pamoja na kwamba Tanzania ilishaingiza kwenye kanuni za ligi masharti ya utoaji
leseni, CAF imekuja na maagizo kwamba ni lazima itamkwe kwenye katiba kuwa TFF
itatoa leseni kwa klabu kwa mujibu wa maagizo ya CAF na msipofanya hivyo klabu
zenu hazitaruhusiwa kushiriki mashindano ya klabu ya Afrika
mwakani,”
Simba na
Azam FC zitaiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya Klabu Bingwa ya Afrika na
Kombe la Shirikisho, hivyo kutopitishwa kwa mabadiliko hayo mapema kutasababisha
wawakilishi wa Tanzania wazuiwe kushiriki michuano hiyo.
Kuhusu
kuundwa kwa Kamati ya Rufani, Tenga alisema baada ya kuomba ufafanuzi wa utata
uliojitokeza katika vyombo vya maamuzi vya TFF, FIFA ilisema ili kuondoa
mgongano wa kimaslahi, ni muhimu ikaundwa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi wa TFF
badala ya mfumo wa sasa ambao Kamati ya Rufani hujigeuza kuwa Kamati ya Rufani
za Uchaguzi inapofikia wakati wa uchaguzi mkuu wa TFF.
“Kwa
hiyo tunachoomba hapa ni ridhaa ya wajumbe wa Mkutano Mkuu kwamba iwepo Kamati
ya Rufani ya Uchaguzi wa TFF ili kama mtu hatatendewa haki na Kamati ya Uchaguzi
ya TFF, basi akate rufani kwenye Kamati ya Rufani ya Uchaguzi badala ya chombo
kimoja kushughulikia mambo mawili,” alisema Tenga.
Kuhusu
kuondoa nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais wa TFF, kiongozi huyo alisema suala
hilo lilitokana na uamuzi wa Mkutano Mkuu uliopita kuwa Ligi Kuu na Ligi Daraja
la Kwanza ziendeshwe na chombo huru.
“Baada
ya hapo Kamati ya Utendaji iliziambia klabu kuwa tunaunda Kanuni za Kuendesha
chombo huru cha ligi, tunaomba mapendekezo yenu. Na ndipo walipotuletea
mapendekezo yao kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi atoke kwenye klabu sita za juu
na kwamba kiwango cha chini cha elimu kiwe Cheti cha Elimu ya Kidato cha Nne
kama ilivyo kwenye katiba,” alisema.
“Maana
yake ni kwamba sifa hizo hazikidhi utashi wa kikatiba wa sifa za mgombea wa
nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais wa TFF ambazo ni Elimu ya Chuo Kikuu, lakini
klabu zikasema hazina haja na nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais na ndio maana
tunaomba ridhaa sasa ya kuondoa nafasi hiyo.”
“Napenda
kusema jambo hili ni la maendeleo na hakuna hata moja ambalo si la maendeleo.
Tumepata barua kutoka Kagera ikieleza kuwa utaratibu huu haufai, Katibu Mkuu
amepata na atawajibu. Pwani nao wameomba ufafanuzi na tutatoa waraka wa
ufafanuzi kwa wote.
“Watu
wana haki ya kuhoji na sisi ni wajibu wetu kuwaelimisha. Ombi langu ni
tushirikiane ili twende kwenye mkutano mkuu wetu unaokuja ili tuchaguane.
Tukichaguana tutakuwa tumetimiza jambo muhimu kweli
kweli.”
Tenga
pia aliwasihi wajuimbe wa Kamati ya Utendaji kuendelea na jitihada za kuelimisha
wajumbe ili waridhie mabadiliko hayo na shughuli za maendeleo ya mpira wa miguu
ziendelee kama kawaida.
Post a Comment