
KWENU mnaohusika na sanaa ya filamu Bongo. Mnajitambua sina haja
ya kuwataja mmojammoja kwa majina, nitamaliza ukurasa bure. Mimi najua mpo
poa, mnaendelea na majukumu yenu ya kila siku. Binafsi niko poa, naendelea na
majukumu yangu ya kila siku ikiwamo hili la kuwaandikia barua.
Barua yangu leo moja kwa moja nailekeza kwa
nyinyi wote ambao watu sasa hivi wanawatambua kwa jina la mastaa wa filamu
katika soko la Bongo, Bongo Movies.
Kikubwa ni kwamba, natambua mchango mlionao katika kusogeza
gurudumu la maendeleo ya nchi. Natambua umuhimu wenu wa kuwatibu watu
kisaikolojia kupitia filamu zenu mnazozifanya.
Hongereni kwa hilo.Katika
taaluma yangu ya uandishi wa habari, mara kadhaa nimeshuhudia uwezo wenu katika
kufanikisha mambo yanayowahusu, iwe ni sherehe au misiba.
Eeeh, kwenye sherehe basi mnalipuka na kushangweka kwelikweli.
Kwenye misiba, mnahakikisha mnamsindikiza mtu anayewahusu kwa hadhi
anayostahili.
Hoja hapa ni kwamba, hadhi ile ambayo
mnajitutumua hadi kwenye misiba, kwa nini tusioneshe kwa mkongwe wa sanaa
nchini, Said Ngamba ‘Mzee Small’? Tunashindwa nini? Mbona pesa zipo?
Kwa nini tusimsaidie mzee wetu ambaye tunaimani alikuwa chachu ya
vijana wengi kuingia kwenye sanaa?
Mzee wetu anasumbulia na ugonjwa wa kupararazi.
Anashindwa kufanya shughuli zake za sanaa ambazo ndiyo chanzo cha pato lake la
kila siku.
Binafsi nilisikitishwa na kupongeza kitendo cha
Rais wa Shirikisho la Filamu nchini TAFF, Saimon Mwakifwamba kuingilia kati na
kuanza kutembeza ‘bakuli’ la michango kwa ajili ya kumsaidia mzee huyo.
Nilisikitika kwani sikuona haja ya yeye kuingilia
kati suala hilo ambalo naamini lilikuwa chini ya uwezo wenu, mnaweza bwana!
Kikubwa ni kipi haswa? Mbona mna ‘mauwezo’, msinifanyie hivyo bwana.
Kwani kuna tatizo gani tukiweka nukta katika
starehe hata kwa siku moja, tusipige kilevi siku hiyo halafu tujichangishe
fedha za kumpa sapoti mwenzetu kwenye kipindi hiki ambacho anaumwa?
Hakika hili ni dogo, tukiamua tunaweza tena
haliwezi kuharibu bajeti zenu hata kidogo.
Ni yule yule,
Mkweli Daima.
Joseph Shaluwa
Post a Comment