Dereva Mwanamke wa Basi la la
Shabiby, Nusra Maguluko, akizungumza wakati alipoalikwa mbele ya
viongozi kutoa ushuhuda kuhusiana na kazi yake ya Udereva wa magari
makubwa kama Mwanamke, wakati wa hafla ya uzinduzi wa Jengo la Kampuni
ya usafirishaji ya DHL, iliyofanyika siku za hivi karibuni jijini Dar es
Salaam. Nusra alialikwa katika hafla hiyo baada ya kuwa ni mmoja kati
ya wanawake waliopata tuzo za Usafirishaji kutoka kampuni hiyo ya DHL.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bila,
Waziri wa Uchukuzi, Dkt. Harrison Mwakyembe, Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Mkurugenzi wa DHL na Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano
Zanzibar, Rashid Seif Suleiman, wakiwa katika picha ya pamoja na Nusra
Maguluko, wakati wa hafla ya uzinduzi wa jingo la DHL, hivi karibuni.
***********************************
*Ana ndoto za kufungua Chuo cha mafunzo ya udereva kwa wanawake ili waweze kuendesha magari makubwa.
*Basi lake hugombaniwa na abiria popote anapopakia, hujaza kwanza na kuondoka kisha mabasi mengine
NUSRA Maguluko (28)
ni msichana jasiri na anayependa kujaribu na kupata mafanikio ya
majaribio yake bila woga wala kujali ni aina gani ya kazi anayotakiwa
kufanya yeye kama mwanamke na ipi asiyostahili kufanya yeye kama
mwanamke.
Ni ujasiri wake hasa
ndiyo ulimuwezesha kumfikisha hatua aliyonayo kwa sasa, ambaye ni
miongoni mwa wanawake wachache na hasa kwa Tanzania waliopata kuifikia
na kujiamini hadi kuwa na ujasiri wa kubeba roho za watu zisizopungua 40
kila safari moja ya kwenda Dodoma ama kotoka Dodoma kuja Dar.
Nusra ni mzaliwa wa
Mkoa wa Manyara katika wilaya ya Kiketo, na ni mtoto wa nne kuzaliwa
kati ya 12 wa familia ya baba yake mzazi mzee, Maguluko na Elimu yake ni
Kidato cha pili tu.
Alimaliza elimu ya
Msingi mwaka 1997, katika Shule ya Msingi Matui iliyoko Wilayani Kiteto,
baada ya kuhitimu elimu ya msingi alijiunga na elimu ya Sekondari
ambayo kwa bahati mbaya hakuweza kumaliza na kuishia Kidato cha pili
baada ya kusumbuliwa na maumivu ya kichwa mara kwa mara.
Nusra, alishauriwa
na madaktari kupumzika kwa muda wa miaka mitatu bila kusoma ama kuwa
akiangalia karatasi nyeupe mara kwa mara, jambo ambalo lilimfanya kuamua
kumsumbua Baba yake mkubwa, Hamis Mang'endi aliyekuwa ni fundi wa
magari ili amfundishe ufundi na udereva wa gari.
Baada ya kumsumbua
sana baba yake mkubwa, kwa kuwa akiripoti katika gereji yake kila
asubuhi na kushinda hapo huku akimfuatilia kila analofanya katika
magari, Mzee Hamis, baada ya kuona kuwa Nusra alikuwa na moyo wa kweli
wa kujifunza ufundi, aliamua kuanza kumfundisha ufundi hatua kwa hatua.
Baada ya kumudu kidogo kushika
Spana, Mzee Hamis, mwaka 1998, alianza kumfundisha udereva, tena kwa
kumfundishia katika gari aina ya Comb Volkswagen, ambapo baada ya miezi sita tu Nusra tayari alishamudu kuendesha gari na kutulia barabani.
Nusra alipomudu kufanya vurugu za
barabarani, alikabidhiwa na baba yake mzazi, Canter ya Tani 3 na robo
ili aweze kufanyia kazi ya kubebea mizigo, huku akikodishwa ambapo
alifanya kazi hiyo kwa muda wa miaka miwili.
Hatimaye mwaka 2001, Nusra,
aliamua kuachana na kazi ya kuendesha Canter ya kubeba mizigo na kuamua
kuanza kazi ya kulima kwa Treka, ambapo alikuwa akikodishwa na wakulima
na alimudua kulima hadi Heka 10 kwa siku kwa ujira wa Sh. 10, 000 kwa
kila heka moja.
Mwaka 2003, Nusra alianza
kuendesha Min Bus, huku akiwa na Leseni ya Class C baada ya wakati huo
kudanganya umri ili aweze kupata uhalali ya kufanya kazi anayoipenda ya
udereva.
Alifanya kazi hiyo ya kutoa huduma
usafiri kwa abiria kutoka Wilaya ya Kiteto kwenda Vijijini hadi mwaka
2006, alipokabidhiwa Basi aina ya Fuso lenye uwezo wa kubeba abiria 40,
nakutoa huduma hiyo ya usafirishaji wa abiria kutoka Wilaya ya Kiteto
hadi Dodoma, kazi aliyoifanya hadi mwaka 2011.
Baada ya kuchoshwa na njia za
Vijijini na kile alichodai kuaua kutafuta maslahi zaidi, Nusra, aliamua
kuvaa, Mbunge wa Gairo, he Shabiby, na kumuomba kazi jambo ambalo
lilimshangaza na kumuhoji kama anaweza kweli kuendesha gari kubwa tena
la abiria.
''Baada ya kuniuliza swali hilo,
mimi nilimjibu Mheshimiwa samahani wewe nisaidie unipe kazi, halafu
ndiyo utaniona nikiwa kazini kama naweza ama siwezi, kwani najiamini na
ndiyo maana nimekuja kwako''. alisimulia Nusra
Baada ya maongezi marefu ya
maswali na majibu juu ya ujasiri wa Binti huyo, aliyeonekana mdogo akiwa
na maelezo ya mambo makubwa, Mhe. Shabiby, aliamua kumwajiri, Nusra
ambapo hadi sasa anapiga mzigo katika kampuni hiyo ya Shabiby, akiburuza
Basi linalofanya safari zake Dar-Dom.
Hivi Sasa Binti huyo, anandoto za
kufungua Chuo cha Mafunzo ya Udereva kwa wanawake, akiwa na lengo la
kuwafikisha mbali wanawake wenzake ili waweze kuwa na ujasiri wa
kuendesha magari makubwa na si gari ndogo pekee.
Kwa hatua hiyo sasa Nusra,
ameanza kusaka wafadhili, ili aweze kutimiza ndoto zake hizo, ambapo
amewamba wadau mbalimbali pamoja na Serikali kujitokeza kumsapoti, ili
kufanikisha kufungua chuo hicho chenye lengo la kuwainua Kinamama.
Post a Comment