
Alisema hiyo ndiyo itakuwa agenda yake ya kwanza anayotarajia kuifanya wakati wa kikao cha Bunge kinachotarajiwa kuanza Februari mwakani
“Nasisitiza kuwa Waziri Mkuu, alilidanganya Bunge kuhusu chanzo cha maandamano yaliyofanyika Januari 5, mwaka uliopita yaliyosababisha vifo vya watu watatu pia Uchaguzi wa Meya wa Jiji la Arusha,” alisema Lema na kuongeza:
“Nataka nikute majibu ya hoja yangu mezani. Kama mimi nilisema uongo, basi niliombe Bunge radhi na kama Waziri Mkuu alisema uongo ijulikane hadharani,” alisema Lema.
Aliongeza kwamba alisikitishwa na kauli ya Spika Makinda, kuzima hoja yake bungeni, licha ya kutakiwa kuweka hadharani maelezo yake, kama ilivyoombwa na Mnadhimu wa Kambi wa upinzani bungeni, Tundu Lissu.
“Walinitaka nitoe maelezo juu ya kauli yangu kuwa Waziri Mkuu amelidanganya Bunge, nikawapa na ushahidi wote tangu mwezi Februari, lakini wamekaa kimya na Spika akasema mbunge akiondolewa na hoja yake imekufa. Sasa narudi Bunge lijalo nataka nikute majibu yangu,” alisema Lema.
Akizungumzia suala la Lyimo, Lema alisema msimamo wake na chama chake ni uleule wa kutomtambua Meya huyo na kusisitiza kuwa hatashirikiana naye kwa kuwa hakupatikana kihalali.
“Msimamo wangu ni uleule Arusha haina Meya na bado naitaka Serikali kuitisha uchaguzi wa meya kwani aliyepo siyo halali,” alisema.
Alisema ingawa CCM ndicho chenye madiwani wengi katika Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Arusha na anajua uchaguzi ukirudiwa CCM itashinda, lakini anachotaka ni kujenga misingi ya kuheshimu sheria na taratibu.
“Mgogoro huu ulisababisha tupoteze madiwani watano na msimamo wa Chadema bado haujabadilika hadi sasa. Nitashauriana na Kamati Kuu (ya Chadema), kuona hatua zaidi tunazoweza kuchukua kama Serikali ikikaa kimya na moja ya hatua hizo ni kumfungia milango meya asifanye kazi,” alisema Lema.
chanzo: Mwananchi
Post a Comment