Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiagana na balozi mdogo
wa Oman aliyepo Zanzibar Sheikh Mansoor Al-Busaid baada ya mazungumzo yao
yaliyofanyika ofisini kwake Migombani.
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na Balozi
mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar Sheikh Mansoor Al-Busaid ofisini kwake
Migombani.
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akimshindikiza balozi
mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar Sheikh Mansoor Al-Busaid baada ya mazungumzo yao
yaliyofanyika ofisini kwake Migombani
(Picha
na Salmin Said, OMKR)Na Hassan Hamad OMKR
Oman
imeahidi kuendeleza mashirikiano yake na Zanzibar katika sekta mbali mbali
zikiwemo elimu, habari, utunzaji wa kumbukumbu na majengo ya asili.
Balozi
mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar Sheikh Mansoor Al-Busaid ameeleza hayo wakati
akizungumza na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad
ofisini kwake Migombani.
Balozi
Al-Busaid ambaye alionana na Makamu wa Kwanza wa Rais kwa ajili ya kumuaga baada
ya kumaliza muda wake wa utumishi hapa nchini, amesema mashirikiano hayo
yataendelezwa kwa maslahi ya pande zote mbili.
“Hivi
sasa waandishi wawili wa gazeti la Zanzibar Leo wako nchini Oman, tumewapeleka
kwa ajili ya kuripoti uchaguzi wa mabaraza ya miji ‘municipality election’ na
pia tunatarajia kuchukua waandishi wengine wawili wa magazeti kwenda
Oman”,alieleza balozi Al-Busaid.
Ameishukuru
Serikali pamoja na wananchi wa Zanzibar kwa kumpa ushirikiano mzuri katika
kipindi chote cha utumishi wake, na kuahidi kuwa balozi mzuri wa kuzidi
kuitangaza Zanzibar nje ya nchi.
Amefahamisha
kuwa Zanzibar ni nchi ya amani na pahala pazuri pa kuwekeza, na kuelezea umuhimu
wa kuwaalika wawekezaji wengi zaidi kuja kuwekeza.
Nae
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ameishukuru
Serikali ya Oman kutokana na misaada yake kwa Zanzibar ambayo inasaidia harakati
za serikali za kukuza uchumi
wake.
Ameelezea
kufarajika kwake kutokana na uamuzi wa Sultan Qaboos wa Oman kuanzisha Mfuko wa
Elimu Zanzibar ambao utawasaidia wanataaluma wa Zanzibar kukuza ujuzi wao na
kuinua kiwango cha elimu nchini.
“Nimepata
moyo sana kwa Sultan Qaboos kuanzisha mfuko wa elimu Zanzibar ambao naamini
utawasaidia sana wanataaluma wetu, na hii inathibitisha kuwa Sultan
Qaboos anaipenda na kuithamini sana Zanzibar”, alifahamisha Maalim
Seif.
Maeneo
mengine ambayo Oman iko mstari wa mbele katika kushirikiana na Zanzibar ni
pamoja na masuala ya utamaduni, afya na utunzaji wa kumbukumbu.
Kwa
mujibu wa maelezo ya viongozi hao tayari Sultan Qaboos amekialika kikundi cha
taarab cha wanawake cha Zanzibar kwenda nchini Oman kwa ajili ya kuonyesha
umahiri wao wa kuimba na kucharaza ala za muziki wa Taarab.
Wamefahamisha
kuwa Oman na Zanzibar zina uhusiano wa muda mrefu wa kindugu, na
kwamba hata tamaduni zake zinashabihiyana kwa kiasi kikubwa.
Post a Comment