1. Jeshi la Polisi
Nchini, linawakumbusha wananchi wote kuwa, tunapoelekea kipindi hiki cha sikukuu
za Christmas na Mwaka Mpya itakayoadhimishwa kati ya tarehe 24-26 Disemba, 2012
na tarehe 01 Januari, 2013 wanatakiwa kusherehekea sikukuu hizo kwa amani na
utulivu pasipo vitendo ama viashiria vyovyote vya uvunjifu wa sheria. Wananchi
wote wachukue tahadhali kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kuhakikisha kuwa
vitendo vyote vya uhalifu na wahalifu kwenye maeneo mbalimbali
vinadhibitiwa.
2. Ikumbukwe kuwa, wananchi wenye imani ya Kikristo na hata madhehebu mengine hutumia muda huo kwenda kuabudu pamoja na muendelezo wa sherehe hizo kwenye maeneo mbalimbali ya starehe, uzoefu unaonyesha kuwa baadhi ya watu hutumia kipindi hicho cha sikukuu kufanya matukio ya uhalifu kutokana na mikusanyiko hiyo ya watu.
3. Jeshi la Polisi
limejipanga kikamilifu kuhakikisha kwamba wananchi kote nchini wanasherekea
sikukuu hizo kwa amani na utulivu, ulinzi umeimarishwa kwenye maeneo yote ya
kuabudia, fukwe za bahari, sehemu za starehe na maeneo mengine yote ambayo
yatakuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu.
4. Aidha,
tunawatahadharisha wale wote ambao watakuwa wakitumia barabara, kuwa makini kwa
kuzingatia sheria za usalama barabarani, madereva kuepuka kwenda mwendo kasi na
kutumia vilevi wawapo kazini.
5. Katika kuhakikisha usalama kwenye kumbi za starehe, wamiliki wa kumbi hizo wazingatie uhalali na matumizi ya kumbi zao katika uingizaji wa watu kulingana na uwezo wa kumbi hizo, badala ya kuendekeza tamaa ya fedha kwa kujaza watu kupita kiasi. Vilevile, wazazi wawe makini na watoto wao na hasa disko toto na kutokuwaacha kutembea peke yao, ili kuepuka ajali na matukio mengine yanayoweza kusababisha madhara juu ya watoto hao.
6. Wananchi wote wanakumbushwa kwamba, watokapo kwenye makazi yao wasiache nyumba wazi ama bila mtu na endapo kuna ulazima wa kufanya hivyo watoe taarifa kwa majirani zao, na pale wanapowatilia mashaka watu wasiowafahamu wasikae kimya bali watoe taarifa kwa Jeshi la Polisi ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa haraka kwa wahusika kupitia namba simu 0754 785557 ama namba za viongozi wa polisi zilizokwishatolewa hapo awali.
7. Jeshi la Polisi
linatoa wito kwa taasisi mbalimbali za serikali, madhehebu ya dini, asasi za
kiraia, vyama vya siasa, vyombo vya habari, makampuni binafsi ya ulinzi na
wananchi kwa ujumla, kuendelea kutoa ushirikiano na hasa katika kipindi cha
mwisho wa mwaka, ili kuhakikisha usalama wa nchi yetu unadumishwa na raia wote
wema wanaishi kwa amani na utulivu bila hofu ya uhalifu.
8. Mwisho,
nawahakikishia wananchi kwamba, Jeshi la Polisi linatekeleza majukumu yake kwa
kuzingatia sheria za nchi na hivyo halitawajibika kumwonea huruma ama upendeleo
mtu yeyote atakayeenda kinyume na sheria.
NAWATAKIENI WATANZANIA WOTE
KHERI YA CHRISTMAS NA MWAKA MPYA.
Advera Senso-ASP
Msemaji wa Jeshi la Polisi (T)
POLISI MAKAO MAKUU.
Msemaji wa Jeshi la Polisi (T)
POLISI MAKAO MAKUU.



Post a Comment