Jukwaa la kiuchumi duniani limefunguliwa rasmi mjini Davos nchini Uswisi hii leo ambako takriban viongozi 45 duniani pamoja na wanaharakati 2500, waandishi habari, wakuu wa kibiashara na wanauchumi wanahudhuria.
Mkutano huo wa kila mwaka ambao unafanyika kwa siku tano umeanza kwa kujitokeza hisia za kuwepo matumaini kwamba hali mbaya ya kiuchumi huenda ikawa imefikia mwisho. 
Tofauti na ilivyokuwa katika mkutano wa mwaka jana, ambapo ulitawaliwa na mzozo wa kiuchumi barani Ulaya pamoja na hofu kwamba Ugiriki huenda ikatimuliwa katika kanda ya Euro.
 Katika ufunguzi muasisi wa jukwaa hilo na muandaaji Klaus Schwab mwenye umri wa miaka 74, ametoa wito kwa wajumbe kulishughulikia suala la mgogoro wa madeni katika kanda ya Euro, ambao umelisogeza eneo hilo katika mporomoko wa kiuchumi.