KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma
(POAC) imebaini ufisadi wa zaidi ya Sh milioni 590 zilizotolewa na Wizara ya
Maliasili na Utalii kwa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).
Hatua ya kubainika kwa ufisadi huo, hasa wa
matumizi yasiyoeleweka ya fedha hizo, iliifanya POAC kuagiza kwa kauli moja
kuhakikisha Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wsa Hesabu za Serikali (CAG) anaifanyia TTB
ukaguzi maalumu.
Katika taarifa za hesabu za mwaka wa fedha wa
2010/2011 iliyowasilishwa mbele ya POAC, ilionekana kuwa kuna fedha za bajeti
zilizobaki, huku TTB ikishindwa kuziwasilisha Hazina kwa mujibu wa sheria.
Aidha, Kamati hiyo pia ilihoji sababu ya Wizara
ya Maliasili na Utalii kupeleka bajeti iliyobaki TTB na kutoa agizo fedha hizo
zilipwe kwa watu ambao waliwataka wao bila kutaja sababu za watu hao kulipwa
fedha hio badala ya kuzipeleka Hazina, hali iliyoonyesha utata juu ya matumizi
ya fedha hizo.
Viongozi wa Bodi hiyo walikuwa katika wakati
mgumu baada ya kuulizwa sababu iliyowafanya kuwapelekea fedha na kumpa mtu mmoja
kuwalipa watu na si Wizara kuchukua jukumu la kuzipeleka Hazina.
Akihoji kwa kutaka kupata ufafanuzi zaidi,
Mwenyekiti wa Muda wa Kamati hiyo, Kangi Lugola, alisema zaidi ya Sh milioni 590
ni fedha za bajeti ambazo zilibaki mwaka wa fedha wa 2010/2011 na hazina maelezo
zimepelekwa TTB na kulipwa watu kwa shughuli gani badala ya kupelekwa
Hazina.
“Kila mwaka inatengwa bajeti kwa ajili ya
shughuli ya maonyesho na bajeti inayobaki inatakiwa ipelekwe Hazina, sasa katika
eneo hili hatuwezi kuendelea na hesabu zingine hadi tupate maelezo ya kina juu
ya matumizi halali ya hizo fedha,” alisema Lugola.
Akitoa ufanunuzi, Mwenyekiti wa TTB, Charles
Sanga, alisema Wizara ndio inayoandaa bajeti na wao wamekuwa wakifanya kazi kwa
kushirikiana nao, hivyo mfumo wa Serikali na mashirika ni tofauti, hivyo fedha
zinapotolewa zinakuwa na barua na si mkataba.
Naye, Mkurugenzi wa Utalii kutoka Wizara ya
Maliasili na Utalii, Ibrahimu Mussa, alisema wanapopeleka fedha katika maonyesho
huwa wana kamati ya pamoja, hivyo kosa lilifanyika kwa TTB na fedha zake
zinaendeshwa kwa ruzuku.
Hata hivyo, Mbunge wa Jimbo la Kigoma
Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), alisema haiwezekani mtumishi mmoja wa wizara
kuchukua fedha na kwenda kufanya malipo.
Chanzo:
Gazeti la Mtanzania
Post a Comment