TAIFA letu limekuwa lilikabiliwa na mdororo mkubwa
wa uchumi uliosababishwa na sera ambazo si rafiki kwa walalahoi. Suala la
kuanzisha vijiji vya ujamaa kuliwaondolea motisha wakulima na kuona kama kuna
ukiritimba kwani aliyekuwa akifanya kazi kwa bidii aliwekewa
vikwazo.
Katika mkutano wa Taasisi ya utafifiti katika
masuala ya kiuchumi na kupunguza umasikini (REPOA) uliofanyika Machi 28, mwaka
huu Jijini Dar es Salaam, Profesa Ibrahim Lipumba aliainisha baadhi ya masuala
muhimu ya uchumi huku akiishauri Serikali hatua za kuchukua.
Profesa Lipumba, ambaye ni bingwa wa uchumi duniani,
anasema wakati wa ujamaa wafanyabiashara wengi waliokuwa katika sekta binafsi
walikuwa wanajua namna ya kuitumia serikali na sekta ya umma kuweza kupata
masilahi ambapo kutokana na hali hiyo ndipo rushwa ikaanza kwenye ukiritimba wa
dola ndani ya uchumi.
Anasema, hadi kufikia mwaka 1985 Tanzania ilikuwa na
hali mbaya zaidi kutokana na madeni yaliyoshindwa kulipwa na Serikali hata
kufikia Mashirika ya umma kupata hasara na hayakuweza kuendeleza ajira wala
uzalishaji.
Anasema, wakati tukiingia katika urekebishaji wa
uchumi huku tukiwa hatuna dira thabiti kwa wale wanaouziwa mashirika,
tulishindwa kujua waliouziwa kama wanaweza kufanya kazi kama mikataba
inavyosema.
Akitolea mfano, Profesa Lipumba anasema, wakati
wakulima wa korosho wanaambiwa wasimuuzie yeyote zao hilo zaidi ya chama cha
ushirika, bado chama hicho kinawakopa na kusababisha kupungua kwa motisha kwa
mkulima.
“Miundombinu yetu ni mibovu kwani huwezi kuwa na
uchumi wa kisasa bila ya kuwa na umeme wa uhakika, uwekezaji wetu katika umeme
umekuwa mdogo”
“Ni wazi uwekezaji mwingi ulikuwa ukitegemea misaada
kutoka nje, lakini pamoja na misaada hiyo, bado tumeshindwa kukusanya mapato na
kuendeleza uwekezaji nchini” anasema Profesa Lipumba.
Mtaalamu huyo wa uchumi, anasema anasema madini
yamekuwa ni sababu kubwa kwa serikali kutegemea misaada ya wahisani katika
kupanga bajeti yake, kwani imekuwa haikusanyi mapato katika sekta ya
madini.
“Wawekezaji wamefanikiwa kututeka kwani kampuni zote
kubwa za wanasheria wetu maarufu ndio wanakuwa wanasheria wa Kampuni za migodi,
na Watanzania wengi maarufu wamepewa nafasi ya kuwa wenyeviti wa bodi au wajumbe
wa bodi.
“Kampuni zimekuwa bingwa wa kuchukua watu wakubwa
kuwa na vyeo vya juu, hivyo inahitaji kiongozi wa nchi uwe na nguvu ya umma au
jasiri kuhakikisha nchi nayo inapata fedha za kutosha.
“Tanzania tumegundua kuwepo kwa gesi maeneo ya
Mkuranga, Mtwara na Kilwa lakini tusipokuwa makini kwa kuangalia mikataba bado
haitawanufaisha Watanzania.
“Tunatakiwa katika madini tupate angalau mapato ya
asilimia 30 yaingie katika pato la serikali ili tuyaingize yasaidie katika sekta
za afya, miundombinu, elimu na kilimo,” anasema Profesa Lipumba
Anasema tofauti na hilo, inabidi kujifunza kwa
wengine huku akitolea mfano Botswana kwa kueleza kwamba katika madini yao ambayo
mengi ni almasi inayofikia asilimia 70, inatumiwa kwa kuwanufaisha wananchi moja
kwa moja au kuingia katika mapato ya serikali au mapato ya
umma.
Profesa Lipumba anasema nchi inapaswa kuwa na
mikataba ya aina hiyo ambayo ina tija kwa wananchi.



Post a Comment