KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, imeitaka serikali kutumia adhabu mbadala ili kupunguza msongamano wa wafungwa gerezani ambao wengi wao wana kesi za kubambikiziwa.
Mbali na hilo, kamati hiyo pia imeitaka Serikali kuweka utaratibu mzuri wa usikilizaji wa kesi za mahabusu ambazo zinakaa muda mrefu bila ya kusikilizwa, jambo ambalo limechangia kuongezeka kwa idadi ya mahabusu huku magereza zikizidiwa uwezo.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Edward Lowasa alisema kutokana na hali hiyo nchi nzima ina zaidi ya wafungwa 29,000, wakati mahabusu 36,552. Alisemakutokana na hali hiyo, idadi ya mahabusu inazidi wafungwa kwa asilimia 23, jambo ambalo linaonyesha wazi kuwa magereza yamezidiwa uwezo.
Alisemakati ya hao,asilimia 90 ni vijana ambao wana kesi mbalimbali ikiwemo, ulevi, uzinzi, wizi wa kuku, wizi wa baiskeli, kesi za ndoa, uzururaji na mambo mengineyo ambayo kwa kiasi zinaweza kumalizwa kwa muda mfupi au kupewa dhamana.
Alisema, kwa upande wa Segerea peke yake, gereza hilo lina wafungwa 98,wakati mahabusu 2,400.
Aliongeza kuwa mahabusu na wafungwa hao wametakiwa kutoa Sh200,000 kama rushwa ili waweze kupewa dhamana au kutolewa, jambo ambalo linaonyesha wazi kuwa idara husika haitendi haki.
Kwa mujibu wa Lowasa,kutokana na hali hiyo, vijana wengi wameonekana kukata tamaa ya maisha, jambo ambalo limewafanya wajiingize kwenye vtendo hivyo.
Alisema ili kutatua tatizo hilo,wizara husika zinapaswa kujipanga ili kuhakikisha kuwa wanatatua suala la ukosefu wa ajira kwa vijana, jambo ambalo linaweza kusaidia kupungua idadi ya wafungwa gerezani.
Alisema kutokana na hali hiyo, kamati hiyo imependekeza kuwepo kwa ushirikiano wa karibu kati ya jeshi la polisi, idara ya upelelezi na magereza ili kutatua kesi hizo kwa muda mfupi na kupunguza idadi hiyo magerezani.
Alisema mbali na hilo, kamati hiyo pia imewataka kuwepo kwa uhuru wa kupata habari ili wafungwa na mahabusu hao waweze kuwasiliana na ndugu na jamaa zao.
Post a Comment