Bango la mahakama ya hakimu mkazi mjini Singida.(Picha na Nathaniel Limu).
 
Na Nathaniel Limu.
Jumla ya raia 12 wa nchini Ethiopia wamehukumiwa na mahakama ya wilaya ya Singida kulipa faini ya shilingi laki moja (100,000) kila mmoja, baada ya kukiri makosa mawili ya kuingia na kuishi ndani ya ardhi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila ya kuwa na kibali halali.
Pia mahakama hiyo, imeamuru basi la kampuni ya Mtei ya mjini Arusha T.797 CDZ lililokuwa limewabeba Waethiopia hao, likamatwe na kutaifishwa kuwa mali ya serikali.
Waethiopia hao wote bado ni vijana wadogo na wengine ni wanafunzi wa shule na vyuo.
Baada ya nwendesha mashitaka mwanasheria wa serikali Ahmed Seif kuwasomea makosa hayo mawili ya kuingia na kuishi nchini bila ya kuwa na kibali, washitakiwa wote kila mmoja kwa nafasi yake, walikiri kutenda makosa hayo.
Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, mwanasheria wa serikali Seif aliiomba mahakama hiyo kuwa iwape adhabu kali washitakiwa ikiwa ni njia moja wapo ya kukomesha vitendo vya wahamiaji haramu kuingia na kuishi nchini bila ya kuwa na kibali cho chote halali.
Akitoa hukumu hiyo hakimu mfawidhi kiongozi wa mahakama ya wilaya ya Singida Flora Ndale, amesema mahakama yake imezingatia yale yote yaliyoombwa na upande wa mashitaka na utetezi na kufikia uamuzi wa kutoa adhabu ya kulipa faini ya shilingi laki moja kwa kila mshitakiwa.
Hata hivyo, washitakiwa wote 12 kila mmoja wao alilipa faini hiyo ya shilingi laki moja na hivyo kuachiwa huru.
Kwa mujibu wa mwanasheria wa serikali Seif, washitakiwa hao walikamatwa Januari 17 mwaka huu alasiri katika eneo la kijiji cha Kititimo nje kidogo ya mji wa Singida, wakiwa wametokea mkoani Arusha wakielekea nchini Afrika kusini.