Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma
Kaskazini
Na Kambi Mbwana, Dar es
Salaam
BAADHI ya watu wanajidanganya kuwa rais mzuri
wa Watanzania atatokana na jina lake au umaarufu wake kisiasa katika Tanzania ya
leo yenye changamoto.
Edward Lowassa, Mbunge wa
Monduli
Si kweli. Wengi wenye uelewa wa mambo ya siasa
na umahiri wa kupambanua mambo, wanajua kuwa mtu huyo ambaye ndio tegemeo la
nchi, atatokana na ujuzi wake wa kubuni na kuchambua changamoto kwa ajili ya
maendeleo ya Taifa lake.
Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard
Membe
Katika kulisema hili, nashangaa kuona baadhi
ya watu wakitembea Mashariki na Magharibi kunadi majina ya watu wao wanaotajwa
kugombea urais mwaka 2015.
Professa Ibrahim Lipumba,
Mwenyekiti wa CUF
Sipingi nia ya watu hao kuwania urais katika
Taifa lao, ila nitashangaa kama wanasiasa hao watapitishwa kwa umaarufu wa
majina yao.
Tukifanya hivyo tutaumia. Ikulu ni mahali
patakatifu na kamwe hapatastahili kwenda kwa sababu tu ya umaarufu wake wa jina
linalopambwa na wafuasi wake.
Hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere aliwahi kulisema hili enzi za uhai wake. Alipinga wale walioanza kuingia
kwenye dhambi ya kutaja majina ya wanasiasa wao eti wanafaa kugombea
urais.
Sakata hili limezidi mno mara baada ya Rais
Jakaya Mrisho Kikwete kushinda awamu yake ya pili, mwaka 2010, ambapo wenye
malengo ya kugombea urais mwaka 2015 walianza kujipanga.
Mengi yalianza kusikika au kuonekana, pale
wanasiasa hao wanavyojipambanua katika kutilia mkazo hoja zao au mahitaji yao
siku za usoni.
Kwa bahati mbaya, ndani ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM), hakuna hata mwanasiasa mmoja aliyetangaza nia ya kurithi mikoba ya
Kikwete.
Ingawa
hawajatangaza hadharani, lakini wachambuzi wa mambo ya kisiasa, wamewabaini,
hasa kwa kuorodhesha kauli zao au vikao vyao vya siri.
Kwa mfano, Waziri Mkuu wa zamani, Edward
Lowassa, ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, ametajwa kuwa na nia ya kugombea urais
mwaka 2015.
Japo
Lowassa hajasema popote lengo hilo, lakini kila analofanya kwa sasa, linaingizwa
katika mlengo wake wa Uchaguzi Mkuu, ikiwamo chaguzi za ndani ambazo zilitajwa
kama silaha ya kwanza ya waziri huyo aliyejiuzulu.
Viongozi wengi walioshinda katika
chaguzi za ndani za CCM mwaka jana, walitajwa kuwa na uhusiano mzuri na Lowassa,
wakiwamo washindi kutoka Jumuiya ya Vijana (UVCCM) Taifa, ambapo Sadifa Khamis
Juma, alishinda nafasi ya Mwenyekiti, wakati Mboni Mhita alishinda nafasi ya
Makamu Mwenyekiti wa Umoja huo.
Ukiacha
Lowassa, bado wapo wanasiasa wengine kutoka CCM, akiwamo Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, anayetajwa kuwania nafasi hiyo ya
urais mwaka 2015 na wengineo.
Mbali
na CCM, lakini bado wapo wanasiasa kutoka vyama vingine ambavyo huko nako kuna
majina makubwa na yenye kutishia katika harakati hizo za urais.
Wapo
watu kama vile Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
Willbroad Slaa, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe pamoja na mwenyekiti
wao, Freeman Mbowe wanaotajwa kuwania urais.
Vita
vyao ndani ya chama watavimaliza wenyewe, kama itakavyokuwa ndani ya Chama cha
Wananchi (CUF), chini ya Profesa Ibrahim Lipumba, Maalim Seif Sharif Hamad na
wengineo kutoka NCCR-Mageuzi, TLP na vyama vingine vyenye kusimamisha wagombea
wa nafasi ya urais.
Kama
nilivyosema hapo juu kuwa yeyote anaruhusiwa kuwania nafasi hiyo, lakini
aangaliwe umahiri wake, sifa zake zinavyoweza kulikomboa Taifa
letu.
Mtu
huyo asipewe nafasi hiyo nyeti eti kwa kuwa anapopita barabarani wapo wachache
wanaolala na yeye kupita juu yao, au kutandikiwa kanga za sandukuni kama ishara
ya kumlaki mwanasiasa huyo.
Tanzania yenye changamoto nyingi
kama vile ugumu wa maisha, magonjwa na elimu duni, haitapiga hatua kama rais
wake hatakuwa makini.
Tutaanguka zaidi, hivyo ni jukumu
la kila Mtanzania kuwa makini katika mchakato huo wa kupatikana mrithi wa
Kikwete, ambaye hapana shaka naye anaumiza kichwa jinsi gani ya kumuachia mrithi
wake.
Najua
wapo ambao majina na haiba zao ni kubwa, lakini suala la urais si jambo la
kitoto. Hivyo tuwahoji na kuwapima kama kweli wanaweza kuvaa kiatu
hicho.
Na kama
tunajua kuwa hawawezi basi uungwana ni kuwaambia na kuwaweka kando bila kuleta
chuki na uhasama katika siasa za Tanzania zinazozalisha matatizo kwa baadhi ya
wanasiasa wetu.
Huu
ndio ukweli. Kuusema wakati huu ambao watu wanapita na wapambe wao kusafisha
njia kunataka moyo wa chuma, hasa kwa kuangalia kuwa kila mtu anataka kuweka
mtandao wake kwa ajili ya kumpatia nafasi hiyo.
Rais wa
Tanzania ni yule atakayeinua uchumi wa Taifa lake kwa kuwasimamia vyema
watendaji wake pamoja na kuhakikisha kuwa rasilimali za Taifa zinawanufaisha
wazawa.
Kwa
mfano, licha ya kujengwa shule za kata kwa ajili ya kuwafanya watoto wa masikini
wapate elimu ya sekondari, lakini shule hizo hazina walimu wala vifaa vya
kufundishia.
Ukirudi
kwenye elimu ya msingi, nako kuna changamoto nyingi, wakiwapo walimu kugoma
kwenda katika maeneo yao ya kazi kwa sababu ya kukwepa maisha
magumu.
Shule
nyingi zilizokuwapo vijijini zimekumbwa na balaa hilo, hivyo tunahitaji rais
mwenye mipango na ambaye atahakikisha kila mtu anafanya kazi yake kama
inavyotakiwa.
Naamini
watu wa aina hiyo wapo, ingawa kwa bahati mbaya, wanaweza kufichwa na wale wenye
nyota zao au uwezo wa kipato wa kununua watu wa kupita nyumba hadi nyumba
kuwahamasisha wajumbe wawapigie kura siku ya kutafutwa nani anaweza kupitishwa
kuwania urais.
Ingawa
Kikwete amejitahidi katika kipindi cha uongozi wake, lakini bado hatuwezi kukaa
na kubweteka na badala yake tunahitaji mwingine mwenye ujasiri, mtu makini,
mbunifu na mwenye kuendeleza miradi inayowanufaisha Watanzania
wote.
Mwenye
kujua uwezo anao, basi asifikirie tu kuwa watu watamuingiza kutokana na jina
lake na atakayefanya hivyo, atakuwa amekosea na kuwasaliti
Watanzania.
Huu ndio ukweli wa mambo. Ndio maana Mgodi
Unaotembea umeona ulijadili suala hilo kwa kina, maana rais bora ndiye anayeweza
kuwakomboa Watanzania.
Mengi yapo yanastahili kujadiliwa kwa kina,
hivyo naamini kila mmoja atakaa na kujiangalia mara mbili, huku wale wanaomwaga
fedha kwa ajili ya kunufaisha majina yao, nikiwashangaa kwa kitendo hicho, huku
nikiamini kuwa malengo yao yana matege na wanadanganya nafsi
zao.
Mungu
ibariki Tanzania.
Post a Comment