Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Maofisa wa Jiji Dar kizimbani kwa tuhuma za wizi

MAOFISA watatu wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka 90 yakiwamo ya kula njama, wizi na kuisababishia Serikali hasara ya mamilioni ya fedha.
Akisoma hati ya mashtaka jana mbele ya Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa, Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Hellen Osujaki aliwataja maofisa hao kuwa ni Mhasibu Msaidizi na Ofisa Malipo Mkuu wa Halmashauri hiyo, Elida Mponda, Mhasibu na Mkusanya Mapato, Geofrey Kibasa na Ofisa wa Mapato, Ernest Maduhu.
Osajuki aliiambia Mahakama kuwa mbali na washtakiwa hao, mshtakiwa mwingine, Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Mahesabu wa Halmashauri hiyo, Fatiel Emmanuel bado hajakamatwa na aliiomba itoe hati ya kumkamata, ombi ambalo lilikubaliwa.
Akisoma hati ya mashtaka inayowakabili washtakiwa hao, Mwendesha Mashtaka huyo wa Takukuru alidai kuwa maofisa hao walifanya makosa hayo kinyume na Vifungu vya Sheria vya 306, 258, 270 na 284 A (1) vya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Alidai kuwa kati ya Januari, 2004 na Juni, 2007, Mponda aliisababishia Serikali hasara ya Sh379,868,665.04 kwa uzembe.
Aidha, alidai kuwa kati ya Januari 2005 na Juni 2007, Kibasa pia kwa uzembe, aliisababishia Serikali hasara ya Sh87,576,091.11.
Osajuki pia aliiambia Mahakama hiyo kuwa kati ya Januari 2004/ Septemba 2005 na Novemba 2005/ Januari 2007, Maduhu aliisababishia Serikali hasara ya Sh187,051,169.55 kwa uzembe.
Katika kesi hiyo, namba 13 ya 2013, Mponda anakabiliwa na jumla ya mashtaka 71 yakiwamo ya kula njama, wizi na kuisababishia hasara Serikali na anadaiwa kuwa kwa nyakati tofauti, kati ya Januari, 2004 na Juni, 2007 alikuwa akiiba fedha hizo.


Mshtakiwa huyo anadaiwa kufanya makusanyo mbalimbali katika Kituo cha Mabasi yaendayo Mikoani cha Ubungo, fedha ambazo zilikuwa ni mali ya mwajiri wake na kuzibadilisha kwa kuonyesha hundi zilizokuwa zilizolipwa na kampuni mbalimbali.
Kati ya kampuni hizo, zimo Superdoll, Scania, Gapco, Hoteli ya Temirnal, Sanya, Msae Investment, Scandnavia, Benki za NBC, NMB, CRDB, Azania, Baclays, Standard Chertered, Exim, Tanzania Investment Bank na Wizara ya Fedha.
Kibasa anakabiliwa na mashtaka 16 ya wizi na kuisababishia Serikali hasara na Maduhu anakabiliwa na shtaka la kuisababishia Serikali hasara.
Baada ya kusomewa mashtaka yanayowakabili, wote walikana na upande wa mashtaka ulisema upelelezi bado haujakamilika.
Mawakili wanaowatetea washtakiwa hao, Ademba Gomba, Alipo Mwamanenge na Jesro Tuliamwesiga waliiomba Mahakama iwapatie dhamana wateja wao.Akitoa masharti ya dhamana, Hakimu Nongwa alimtaka Mponda kuwasilisha fedha taslimu Sh190 milioni mahakamani hapo au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha.
Aidha, alimtaka Kibasa kuwasilisha fedha taslimu Sh44 milioni mahakamani hapo au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha na Maduhu alitakiwa kuwasilisha fedha taslimu Sh94milioni mahakamani hapo au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha.
Baada ya kutoa masharti hayo ya dhamana, Hakimu Nongwa alisema hati zote za mali hizo lazima zihakikiwe kama ni halali kabla ya kutoa dhamana na kuiahirisha kesi hiyo hadi Februari 5, mwaka huu.
MWANANCHI
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top