MOTO uliowashwa na wananchi wa mkoa wa Mtwara kupinga gesi asilia kupelekwa Dar es
Salaam inazidi kuchochewa siku hadi siku baada ya juzi Mbatia kufanyiwa vurugu,
sasa msafara wa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene unadaiwa
kuzuiwa kwa magogo na mawe alipojaribu kutembelea kijiji cha Msimbati ambako
gesi asilia inavunwa.
Habari za
kuaminika zilizolifikia blog hii mjini Mtwara leo zinadai kuwa tukio hilo
lilitokea saa 8 mchana mbapo waziri huyo alilazimika kugeuza msafara wake katika
kijiji cha Ziwani na kurejea mjini Mtwara baada ya kutaarifiwa kuwa hali si
shwari.
Habari
zinadai kuwa waziri huyo aliwasili mjini Mtwara kwa ndege ya asubuhi na
kupokelewa na viongozi wa mkoa ambapo inadaiwa kimyakimya alianza safari ya
kwenda Msimbati kabla ya kupewa taarifa ya hali tete ya usalama.
Mashuhuda
wa tukio la kufungwa kwa barabara wamesema kuwa baada ya wananchi kupata habari
za ujio wa waziri huyo, walionekana wazi kutokubalina, hivyo walijikusanya na
kuamua kuifunga barabara kwa kukata magogo na kuyalaza barabarani kwa lengo la
kumzuia asiingie katika kijiji hicho.
Gari
lililokuwa limebeba waandishi wa habari ndiyo la kwanza kuwasili kwenye kizuizi
hicho hata hivyo hawakudhuriwa zaidi ya kuamriwa kugeuza gari na
kuondoka.
Kubwa
linalodaiwa kuwakasirisha wananchi hao ni kauli za kejeli za viongozi wa
serikali kuwa wananchi wa kijiji hicho wananufaika na gesi asilia kwa kutumia
umeme bure ili hali wanalipa ankara za umeme kila mwezi.
“Waziri wa
Nishati na Madini Sospeter Muhongo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora
George Mkuchika kupitia vyombo vya habari wamesema sisi tunatumia umeme
bure…hizi ni kejeli…ninazo bili za umeme tangu nilipounganishiwa” alisema mkazi
wakijiji hicho kwa sharti la kutotajwa jina.
Aliongeza
kuwa “Kana kwamba haitoshi leo wanataka waje kututukana waziwazi ili
wadhihirishe kuwa sisi ni wapuuzi, hatujasoma …tumesema baasi, hatutaki kuonana
na kiongozi yeyote yule”
Mwenyekiti
wa kijiji cha Msimbati Salum Athumani Tostao anathibitisha kuwapo kwa hali hiyo
na kuongeza kuwa polisi walikwenda kijijini hapo na kufyatua mabomu ya machozi
kuwatisha wananchi hao hata hivyo msimao wao uliendelea kuwa hawataki kuongea na
waziri huyo.
“Walikuja
polisi, kama kawaida yao wakafyatua mabomu ya machozi hewani…hakuna mwananchi
aliyekimbia, ilikuwa kama mchezo wa mpira wa miguu wao wanafyatua mabomu hewani
wananchi wanashangilia na kuzidi kuongezeka eneo la tukio” alisema Tostao
akiongea kwa simu.
Alifafanua
kuwa “ Waziri hakuwahi kufika huku, ilikuja gari moja iliyobeba waandishi,
walipoona hali ni tete wakampigia simu asije na ndipo polisi walipokuja badala
yake…polisi waliacha kupiga mabomu na
kuamua
kuongea na wananchi ambao hawakuonesha woga wowote, waliwaambia polisi hawataki
waziri akanyaje ardhi ya kijiji chao”.
Alibainisha
kuwa yeye kama kiongozi wa kijiji hakupewa taarifa juu ya ujio huo na kwamba
hilo halikumshangaza kwa madai ni kawaida ya viongozi hao kuipuuza serikali yake
kwa kuingia kijijini hapo na kutoka bila ya kutoa taarifa kwake.
“Wananchi
walipata taarifa kuwa waziri au naibu wake anakuja na ndipo walipofunga barabara
wakisema hawataki kumuona akikanyaga ardhi yao…kwa bahati nzuri gari ya kwanz
akufika ilikuwa ya waandishi wa habari, kwa huruma wananchi wakawaambia warudi”
alisema mwenyekiti huyo
Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Mtwara, Mary Nzuki akiri wananchi kufunga barabara ingawa
alikanusha madai ya Naibu Waziri Simbachawene kuwapo ziarani mkoani
hapa.
“Waandishi
wa habari waliokwenda katika ziara za kazi zao za kawaida ndiyo waliozuiliwa na
wananchi hao…Naibu waziri hajawahi kufika Mtwara kwa siku ya jana…wananchi
walidhani hilo gari ni la waziri lakini ukweli si yeye” alisema Kamanda
Nzuki
Akizungumzia hilo Simbachawene alisema “Hapana sio kweli, ningekuja
hapo mjini singeweza kujificha…tatizo la wananchi wetu hawajapata elimu sasa
nitaendaje huko kimyakimya ili iweje….jana nilikuwa ofisini na vikao kutwa
nzima…nenda ‘airport’ (uwanja wa ndege) kaulize…hata mimi nimeona kwenye jamii
forum, ile ni ‘open paper’ (kurasa wazi) mtu yeyote anaweza kuweka
chochote”
Aliongeza
kuwa “Inasikitisha, aheri wewe uliyenipigia simu kuliko magazeti yanayochukua
habari kwenye jamii forum…inaonekana kuna watu wamedhamiria hili jambo
hili”
Tukio hilo
limetokea siku moja tangu mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia afanyiwe
vurugu na baadhi ya watu katika mkutano wake wa adhara uliofanyika Uwanja wa
Mashujaa mjini hapa na badaye kutaka kumdhuru kwa madai ya kutoridhishwa na
hotuba yake hali iliyosababisha akatishe ziara yake.
Habari kwa Hisani ya Lindiyetu
blog.
Post a Comment