Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba.
*************
UONGOZI wa Wizara ya Uchukuzi, unajiandaa kukabiliana na kitimoto cha wabunge kuhusiana na uamuzi wake wa kushinikiza kuondolewa kwa watendaji 30 wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), wengi wakiwa ni watendaji muhimu, imefahamika.
Taarifa za ndani ya wizara hiyo, zimeeleza kwamba watendaji wake hawakupumzika siku ya Mapinduzi jana, na badala yake walikuwa ofisini kujiandaa kukabiliana na wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, chini ya Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba.
Tayari imethibitishwa kwamba suala la watendaji wa TPA waliosimamishwa kazi na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, sasa litajadiliwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu.
Hatua hiyo imekuja tayari kukiwa na sintofahamu ndani ya sekta ya bandari, na wabunge wanatarajiwa kutaka maelezo yenye ushahidi kuhusu athari na faida za kuondoa uongozi wote wa TPA.
Dk. Mwakyembe alitangaza kumsimamisha aliyekuwa Mkurugenzi wa TPA, Ephraim Mgawe na viongozi wengine watatu ili kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali dhidi yao na kuunda tume ambayo ilishakabidhi ripoti yake, na sasa maandalizi ya kuwafukuza yamekamilika.
Watendaji hao waliosimamishwa kazi Agosti 23, mwaka jana ni pamoja na Mgawe na wasaidizi wake wawili na aliyekuwa Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Cassian Ngamilo.
Mkurugenzi Msaidizi wa Habari wa Bunge, Deogratius Egdio alisema moja ya kazi itakayofanywa na Kamati ya Miundombinu ya Bunge, itakayoanza kazi kesho, itakuwa ni ya kupokea taarifa kwa TPA.
Mbali ya kuondoa watendaji 30, Dk. Mwakyembe Novemba 6, mwaka huu, alitangaza kuivunja Bodi ya TPA na kushindwa kumuondoa Mwenyekiti wake, Raphael Molel ambaye ni mteule wa rais na kuwa kiongozi pekee anayeng'oa uongozi wote wa sekta nyeti.
"Hata rais akiingia madarakani hawezi kuondoa watendaji wote serikalini bila kuathiri mfumo wake kama alivyofanya Mwakyembe, hata serikali ikija ya upinzani na tumeona hata nchi ambazo yametokea mapinduzi, hawajatimua watendaji katika sekta nyeti," alisema mdau mmoja wa bandari.
Tayari kampuni binafsi ya kuhudumia makontena ya TICTS imeanza kutumia mwanya wa udhaifu wa TPA kujiimarisha na hivyo kuinyima serikali mapato.
Kabla ya timua timua hiyo TPA kwa upande wa kuhudumia makontena walishafika asilimia 35-40 kitendo ambacho kiliweka ushindani mkubwa kwa upande wa TICTS ambako ufanisi wake kwa kiasi kikubwa ulilegalega kutokana na uongozi wa juu wa kampuni hiyo na hasa hasa aliyekuwa mtendaji mkuu, Neville Bisset raia wa Uingereza kuwa mbovu.
Kutokana na Bisset kuonekana ndiye tatizo la kuzorota kwa huduma kwenye kampuni hiyo yenye uzoefu mkubwa duniani katika kuendesha terminals za makontena, makao makuu yao yalimuondoa na kumleta raia wa China, Anacin Kum ambaye amekuwa akiendesha terminal yao huko kwenye bandari ya Shaghai kwa miaka 12 na ana uzoefu mkubwa.
Kwa kipindi cha mwezi mmoja alichokaa nchini, Kum ameshaanza kuboresha hali ya kiuendeshaji iliyokuwepo na ari ya wafanyakazi ndani ya TICTS imesharudi na wateja hasa wenye meli na ICD operators wameshaanza kuridhika na uongozi wake.
Chanzo: Tanzania Daima
Post a Comment