KAMPUNI TANO ZAOMBA KUFANYA UKARABATI HOSTELI ZA TFF
Kampuni tano zimewasilisha
tenda zao kuomba kupewa kazi ya kukarabati hosteli ya Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF). Januari 7 mwaka huu TFF ilitangaza tenda kwa ajili ya
ukarabati wa hosteli hiyo baada ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF)
kukubali ombi lake la kutoa fedha kwa ajili ya kazi
hiyo.
Ufunguzi wa tenda hizo
ulifanyika jana (Januari 28 mwaka huu) kupitia kwa Bodi ya Tenda ya TFF mbele ya
wazabuni wote watano waliowasilisha tenda zao na kushuhudiwa pia na Mkandarasi
mshauri. Wazabuni (kampuni) waliojitokeza awali walikuwa saba, lakini
waliorejesha zabuni zao ni watano.
Kampuni hizo ni Crescent
Concrete Limited, DGS Company Limited, Mart Builders Company Limited, Prince
General Investment Limited na Send Star Company Limited.
Bodi ya Tenda ya TFF
itakutana Januari 31 mwaka huu pamoja na mambo mengine kuchagua kampuni ambayo
itafanya ukarabati huo.
LALA SALAMA DARAJA LA
KWANZA KUANZA JUMAMOSI
Mzunguko wa pili wa Ligi
Daraja la Kwanza (FDL) ambayo itatoa timu tatu zitakazocheza Ligi Kuu ya Vodacom
(VPL) msimu ujao (2013/2014) unaanza Jumamosi (Februari 2 mwaka huu) katika
viwanja tisa tofauti.
Kundi A litakuwa na mechi
kati ya Mbeya City na Burkina Faso itakayochezwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya,
Majimaji na Kurugenzi katika Uwanja wa Majimaji mjini Songea, na Polisi Iringa
dhidi ya Mkamba Rangers kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora mjini
Iringa.
Mechi za Kundi B, Jumamosi
(Februari 2 mwaka huu) itakuwa Transit Camp na Ndanda itakayochezwa Uwanja wa
Mabatini mkoani Pwani, Moro United dhidi ya Villa Squad (Uwanja wa Karume, Dar
es Salaam). Jumapili (Februari 3 mwaka huu) ni Tessema na Green Warriors
(Mabatini, Pwani), Ashanti United na Polisi Dar (Uwanja wa Karume, Dar es
Salaam).
Kundi C Jumamosi (Februari
2 mwaka huu) ni Polisi Dodoma na Kanembwa JKT (Uwanja wa Jamhuri, Dodoma),
Morani dhidi ya Mwadui (Uwanja wa Kiteto, Manyara), Polisi Mara na Pamba (Uwanja
wa Karume, Musoma), Polisi Tabora na Rhino Rangers (Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi,
Tabora).
Ligi hiyo inatarajiwa
kumalizika mwishoni mwa Machi mwaka huu ambapo mshindi wa kila kundi atapanda
daraja kucheza Ligi Kuu msimu
ujao.
WAPAMBE WAPIGWA 'STOP' KWENYE PINGAMIZI, USAILI WA TFF
Kamati ya Uchaguzi ya
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imesema waliowekewa pingamizi na wa
walioweka pingamizi hawaruhusiwi kufika katika kikao cha kesho (Januari 30 mwaka
huu) wakiwa na vikundi vya ushangiliaji au wapambe.
Kikao cha kupitia pingamizi
kitafanyika saa 4 asubuhi na wapambe au washabiki wa waombaji uongozi pamoja na
waweka pingamizi hawakiwi kuwepo kwenye eneo la kikao
hicho.
Wote walioweka pingamizi na
waliowekewa pingamizi barua zao za mwito wa kuhudhuria kikao cha Kamati ya Uchaguzi ya
TFF zimeshatumwa kwenye anwani za barua-pepe zilizo kwenye taarifa za pingamizi
au kwenye fomu za maombi ya uongozi.
Leo waombaji uongozi
watatumiwa barua za mwito kwa barua-pepe wa kuhudhuria usaili utakaofanyika
tarehe 01-02 Februari 2013. Tarehe 01 Februari 2013 watasailiwa waombaji uongozi
wa TPL Board na waombaji ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF kupitia Kanda ya 1
hadi Kanda ya 8. Waombaji uongozi kupitia Kanda ya 9 hadi ya 13 na waombaji
uongozi wa Makamu wa Rais na Rais wa TFF watasailiwa tarehe 02 Februari 2013
kuanzia saa 4 asubuhi.
Vyombo vingi vya habari
vimeonyesha nia ya kuwepo mdahalo wa wagombea uongozi katika TPL Board na TFF.
Kanuni za Uchaguzi za TFF hazizuii jambo hilo kufanyika, bali tu lizingatie
Kanuni za Uchaguzi za TFF. Mojawapo ya mambo ya kuzingatiwa ni kwamba mdahalo
huo ufanyike wakati wa kipindi cha Kampeni na usiwe na taswira ya kuwapendelea
au kuwabagua baadhi ya wagombea. Kanuni hazimlazimishi mgombea kushiriki
mdahalo.
Pia ni vema mdahalo
ukaandaliwa na kuratibiwa na Taasisi
inayounganisha vyombo vya habari au waandishi wa habari kama TASWA. Kamati ya
Uchaguzi ya TFF lazima ijulishwe kwa maandishi nia hiyo ya kufanyika mdahalo na
utaratibu utakaotumika mapema kabla ya kufanyika mdahalo huo ili kujiridhisha
kuwa utaratibu utakaotumika kuandaa na kuendesha mdahalo haukiuki kanuni za
Uchaguzi za TFF.
Kamati ya Uchaguzi ya TFF
inavishukuru vyombo vya habari kwa kuzingatia Kanuni za Uchaguzi hadi sasa na
kuwaomba waendelee kufanya hivyo hadi mwisho wa mchakato wa
uchaguzi.
Post a Comment