Shukurani njema zote anastahiki
Allah Ambaye ametuwezesha kuwa hai tukiwa na afya njema. Tunamuomba Allah
atuwafikishe kufanya mema na aujaalie uhai wetu wote uwe kwa ajili ya kumtumikia
Yeye katika Dini hii ya Kiislamu. Rehema na amani ya Allah zimwendee kipenzi
chetu, mtukufu wa viumbe Mtume Muhammad (Sallallaahu ‘alayhi wasallam), masahaba
zake, jamaa zake na wale wote waliomfuata kwa wema mpaka Siku ya
Malipo.
Ama baada ya hayo,Jumuiya ya Maimamu Zanzibar (JUMAZA)
inachukua fursa hii kutoa taarifa rasmi kwa vyombo vya habari kufuatia tukio la
kupigwa risasi na kuuwawa kwa Padri Mushi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mjini
jana tarehe 17/2/2012 Beit – El – Ras.
JUMAZA kwa mshtuko mkubwa imepokea kwa masikitiko
taarifa ya kuuwawa kwa Padre Mushin na inalaani kwa nguvu zote kitendo hicho cha
kiharamia ambacho kinaashiria kuitia doa Zanzibar kisiwa cha amani na ukarimu
tokea enzi na enzi. Kufuatia kadhia hii JUMAZA inawataka Wanzanzibari wote wa
dini na madhehebu zote kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu na kuendelea
kutunza amani na mshikamano tulionao chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa na
kutotoa mwanya kwa watu au vikundi ambavyo vina nia mbaya ya kutaka kuleta
kutokuelewana kwa wananchi kwa malengo yao binafsi.
Aidha JUMAZA inaungana na kauli iliyotolewa na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuliagiza
Jeshi la Polisi nchini kufanya uchunguzi wa kina na waharaka ili kubaini nani
waliohusika na tukio hili na hatimaye sheria ichukue mkondo wake.
Aidha JUMAZA inaliomba Jeshi la Polisi kufanya
uchunguzi wa kiuadilifu na usioambatana na shindikizo la mtu au kikundi chochote
ili hatimae ukweli halisi ujulikane na bila ya kuwadhuru
wasiohusika.
JUMAZA inakemea vikali kauli za baadhi ya vyombo vya
habari vinavyonasibisha waislamu na tukio hili na kuvitahadharisha vyombo vya
habari ikwemo magazeti na redio hizo kutoanza kutoa taarifa ambazo kwa makusudi
zinaweza kupandikiza chuki na uhasama katika jamii na hatimae kuotesha mizizi ya
fitna na kupelekea Taifa kuingia kwenye machafuko bali viachiwe vyombo
vinavyohusika kufanya uchunguzi wake na kutoa taarifa sahihi. Aidha JUMAZA
inaziomba Serikali zote mbili kuwa waamgalifu sana katika kipindi hiki kwa
kujizuia kutoa maneno yanayoashiria kuhusisha tukio hili na upande fulani wakati
bado uchunguzi unaendelea.
Imesaniwa na:
KATIBU WA JUMAZA
MUHIDDIN ZUBEIR MUHIDDIN
Post a Comment