Na Fredy Azzah na Kelvin Matandiko
MATOKEO
mabaya ya mtihani wa kidato cha nne yamezidi kuibua mapya, baada ya
wamiliki wa shule na vyuo binafsi nchini kusema mitihani ilitungwa kwa
mfumo tofauti na uliozoeleka miaka yote, huku tume iliyounndwa na Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda ikipondwa na baadhi ya watu.Mwenyekiti wa Chama cha
Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi nchini (TAMONGSCO), Mahmoud Mringo
alisema kwamba maswali waliyoulizwa watahiniwa yalikuwa ya kujieleza
tofauti na miaka ya nyuma, ambapo
mfumo uliotumika uliwataka watahiniwa kutaja vitu tu bila ya kulazimika kuvielezea kwa undani.
Kauli
yake iliungwa mkono na Mkuu wa Taaluma katika Shule ya Sekondari ya
Wasichana ya Marian, Florence Mapunda ambaye alisema kuwa mtihani wa
mwaka jana ulitaka zaidi watoto kujieleza tofauti na miaka ya nyuma
wakati wanafunzi walipokuwa wanakariri.
Hata
hivyo, Msemaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), John Nchimbi
alisema mfumo wa mtihani haukubadilika kwa namna yoyote na kuwa upo kama
ule wa miaka yote.
Naibu
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo, kwa upande wake
alisema madai yanayotolewa hayana msingi, huku akihoji kwa nini yasitoke
tangu mitihani ilipokuwa ikifanyika na badala yake yanatoka baada ya
kutangazwa kwa matokeo.
Matokeo
ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika mwaka jana yanaonyesha kuwa
watahiniwa 240,903 sawa na asilimia 60.6 wamepata sifuri, huku wanafunzi
23,520 tu ambao ni sawa na asilimia 5.16 ndiyo waliofaulu na wengine
103,327 sawa na asilimia 26.02 wamepata daraja la nne.
Kutokana
na matokeo hayo, Waziri Mkuu Pinda, juzi alitangaza kuunda tume ya
kuchunguza chanzo cha matokeo hayo kuwa mabaya, hatua ambayo hata hivyo
imekosolewa na wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Tume
hiyo inayoundwa na wajumbe kutoka Taasisi za Elimu, Chama cha Waalimu,
Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii na Umoja wa Wakuu wa Shule za
Sekondari Tanzania (Tahossa) inatarajiwa kuanza kazi wiki hii.
Profesa
Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema kuunda tume
ni kupoteza muda kwa sababu matatizo na changamoto zote ndani ya sekta
hiyo yanajulikana, huku mwenzake, Profesa Chriss Maina pia wa UDSM
akisema kuunda tume hakutaisaidia kwa kuwa Serikali inaidharau sekta ya
elimu.
“Tatizo
ni kutowekeza kikamilifu katika sekta ya elimu, imekuwa na matumizi
makubwa katika mambo yasiyokuwa ya lazima,”alisema Profesa Mpangala.
Alisema
matatizo mengine ni mazingira magumu ya kufundisha na uhaba wa walimu.
“Kinachotakiwa wajipange kufanyia kazi changamoto hizi zilizopo badala
ya kuunda tume, wakati fedha nyingi tunasikia inapotea kwenye
ubadhirifu,”alisema Profesa Mpangala.
Naye
Profesa Maina alisema: “Hiyo tume ya kazi gani kwa sababu matatizo
yanafahamika wazi, umewahi kusikia taifa gani ambalo halina mtalaa wa
elimu. Hiyo ndiyo hali halisi kwa nchi yetu. ”
Post a Comment