Mdhibiti na Mkaguzi mkuu
wa Hesabu za Serikali Bw. Ludovick Utouh akiongea na waandishi wa habari leo
jijini Dar es salaam kuhusu kukamilika kwa mradi wa kuiunganisha ofisi hiyo
kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, mradi uliofanywa kwa ufanisi na Kampuni
ya Simu Tanzania (TTCL) kwa gharama ya shilingi milioni 477.
Mdhibiti na Mkaguzi mkuu
wa Hesabu za Serikali Bw. Ludovick Utouh akipokea cheti cha kukamilika kwa mradi
wa kuiunganisha ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali kwenye Mkongo wa
Taifa wa Mawasiliano kutoka kwa Bw. Kisamba Tambwe (kulia) Meneja wa njia za
Mawasiliano za nje kutoka Kampuni ya simu Tanzania.
Mdhibiti na Mkaguzi mkuu
wa Hesabu za Serikali Bw. Ludovick Utouh (katikati mbele) akiwa katika picha ya
pamoja na watendaji wa Ofisi hiyo na viongozi wa Kampuni ya Simu Tanzania TTCL
leo jijini Dar Es salaam.
Na. Aron Msigwa
-MAELEZO. Dar es salaam.
Ofisi yaTaifa ya Ukaguzi
wa Hesabu za Serikali imeingia katika mfumo mpya wa mawasiliano wa matumizi ya
barua pepe na intraneti utakaoiwezesha ofisi hiyo kutuma na kupokea taarifa za
utendaji kwa haraka kufuatia kukamilika kwa mradi wa kuunganishwa kwenye Mkongo
wa Taifa wa Mawasiliano.
Akizungumza na waandishi
wa habari leo jijini Dar es salaam wakati wa makabidhiano ya mradi huo
uliofanywa na kampuni ya Simu Tanzania, Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za
Serikali Bw. Ludovick Utouh amesema kuwa mradi huo utaiwezesha ofisi yake
kuimarisha mawasiliano ya ndani na nje ya ofisi kupitia mfumo wa
intaneti.
Amesema mradi huo ambao
kwa sasa umeanza kwa kuziunganisha ofisi 12 za mikoa mbalimbali utaleta
mabadiliko makubwa katika nyanja nzima ya upashanaji habari na utawawezesha
watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za serikali kupata mawasiliano
kwa kwa haraka na usalama zaidi kupitia makao makuu ya ofisi
hiyo.
Amesema mkongo wa taifa
utaiwezesha ofisi hiyo kumiliki na kudhibiti taarifa mbalimbali zinazotumwa kwa
kuwatumia wataalam wa Tehama wa ndani huku akibainisha kuwa mfumo huo mpya
utawazuia watumishi wa ofisi hiyo kutumia mifumo ya kawaida ya barua pepe na
mitandao hatarishi inayoweza kuleta madhara kwenye taarifa muhimu za
serkali.
" Mradi huu umekamilika
wakati muafaka kwa sababu utatuwezesha kupunguza gharama, kumiliki na kudhibiti
sisi wenyewe taarifa zetu za kiutendaji za kila siku kupitia wataalam wa Tehama
tulionao katika ofisi zetu na kuondoa kabisa mfumo uliokuwepo wa kubeba taarifa
mikononi kutoka eneo moja hadi jingine" amesema Utouh.
Amefafanua kuwa
kukamilika kwa mradi huo kutaiwezesha Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za
Serikali nchini kujenga uwezo wa uimarishaji wa miundombinu za shughuli za
Ukaguzi na utendaji na kurahisisha mawasiliano kwa kutumia mfumo wa kompyuta
huku akifafanua kuwa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali Tanzania
kwa kipindi cha miaka 6 ni wakaguzi wa Umoja wa mataifa ukaguzi unaofanywa
katika miji mbalimbali duniani.
Utouh amebainisha kuwa
ofisi yake sasa itaweza kufanya mikutano ya kiutawala moja kwa moja na ofisi za
mikoani kupitia mfumo mpya wa mawasiliano wa mtandao (video conference) na
kuwataka watumishi wa ofisi hiyo kuutumia ipasavyo mfumo huo kwa manufaa ya
taifa.
Kwa upande wake Meneja
wa njia za mawasiliano ya nje wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) Bw. Kisamba
Tambwe akikabidhi mradi huo amesema kuwa kampuni hiyo imetekeleza mradi huo kwa
ufanisi mkubwa ili uweze kukidhi malengo yaliyokusudiwa.
Amesema TTCL itaendelea
kuhakikisha kuwa ofisi 12 za mikoa iliyouganishwa kwenye Mkongo wa Mawasiliano
wa Taifa zinakuwa na usambazaji salama wa taarifa kutoka eneo moja hadi
jingine.
Post a Comment