WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amesema Mlima Kilimanjaro unaweza kutumika vizuri zaidi
kwenye vita ya kupambana na ugonjwa wa malaria kwa wanamichezo na watu mashuhuri
kuupanda mlima huo na kuchangisha fedha za kusaidia kampeni ya kupambana na
ugonjwa huo.Alitoa kauli hiyo jana usiku (Jumamosi, Februari 9, 2013)
wakati akihojiwa na waandishi wa habari mara baada ya kushiriki mjadala kuhusu
juhudi za Serikali katika kupambana na ugonjwa wa malaria uliofanyika kwenye
kituo cha mikutano cha Sandton, kilichopo jijini Johannesburg, Afrika Kusini.
Alisema katika majadiliano
yake na baadhi ya wajumbe walioshiriki mjadala huo, wengi waliunga mkono wazo
alilolitoa la kutumia Mlima Kilimanjaro katika kampeni za kupambana na ugonjwa
huo.
“Nimeongea na baadhi ya
wajumbe katika hafla hii hapa Johannesburg, wengi wameliafiki wazo la kutumia
Mlima Kilimanjaro kutangaza mapambano haya… kila mwanamichezo atakayepanda mlima
huu atatangazwa kwamba ameshinda vita dhidi ya malaria na fedha atakayochangisha
itatumika katika kampeni ya kupambana na malaria barani Afrika,”
alisema.
Alipoulizwa ni kitu gani
cha tofauti alichojifunza katika mjadala huo, Waziri Mkuu alisema jambo kubwa
aliloliona ni jinsi ya kutumia mbinu mbadala za kupeleka ujumbe kuhusu mapambano
dhidi ya malaria. “Kila mtu ana dhamana ya kuchangia vita dhidi ya malaria. Hawa
wenzetu wameitisha viongozi wa makampuni makubwa kutoka Afrika Kusini na nje ya
nchi hiyo, wako wadau mbalimbali jioni ya leo walioshiriki mjadala huu,”
alisema.
Akitoa mfano wa Tanzania,
Waziri Mkuu alisema tangu mwaka 2000 idadi ya wagonjwa wa malaria imekuwa
ikishuka lakini vilevile idadi ya wafadhili wanaochangia jitihada za kupambana
na ugonjwa huo nayo pia imekuwa ikishuka. Ndiyo maana nimesema kuna haja ya
kutumia wadau wengine kama vile Bunge, NGOs na Serikali za Mitaa ili kuona
wanaweza kusaidia vipi katika vita hiyo,” alisema.
“Wenzetu hawa, (akimaanisha
– Muungano wa Mashirika ya Kimataifa yanayopambana dhidi ya Ugonjwa wa Malaria –
United Against Malaria (UAM) wametumia mashindano ya AFCON kupeleka ujumbe wa
kupambana na ugonjwa huu unaoua watu wengi Afrika sababu ni moja tu: watu wengi
wanapenda mpira wa soka iwe uwanjani au kuangalia kwenye luninga kwa hiyo
wanajua fika kuwa ujumbe ukitolewa pale utawafikia watu wengi sana na kwa haraka
zaidi. Sisi Tanzania tulishaanza na sasa tunaangalia uwezekano wa kutumia
basketball, netball na michezo mingine kufikisha ujumbe huu,”
alisema.
Mwenyekiti wa Umoja wa
Wabunge wanaopambana na Malaria (TAPAMA- Tanzania Parliamentarians Against
Malaria), Bi. Riziki Lulida ambaye alikuwa miongoni mwa wajumbe waliofuatana na
Waziri Mkuu Afrika Kusini, alisema Tanzania bila Malaria inawezekana na wao kama
Wabunge wanaweza kwenda vijijini kutoa elimu kwa wananchi jinsi ya kujikinga na
ugonjwa huo.
Naye Dk. Hamisi Kigwangalla
ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa TAPAMA alisema atatumia fursa ya kushiriki
mjadala huo kama njia ya kujifunza mbinu mbadala za kuishirikisha jamii kwenye
vita dhidi ya ugonjwa wa malaria. “Leo tumeona wenzetu wakiwatumia watu maarufu
kama Yvonne ChakaChaka, Mark Fish – mchezaji wa zamani wa BafanaBafana na pia
Drogba yuko kwenye matangazo yao kuhamasisha wananchi watumie vyandarua
kujikinga na malaria… sisi pia tunaweza kutumia wasanii na wanamichezo wetu
kuelimisha umma kuhusu mapambano dhidi ya malaria,”
alisema.
Naye Mbunge wa Chonga,
Pemba, Dk. Haroub Mohammed Shamisi ambaye pia ni mjumbe wa TAPAMA alisema
ushirikishwaji mkubwa wa jamii kwenye vita dhidi ya malaria umesaidia sana
kushusha viwango vya maambukizi ya malaria kule Zanzibar.
“Zanzibar imepiga kasi sana
katika vita hii na sababu kubwa iliyochangia ni ushirikishwaji wa karibu wa
wananchi kwenye kampeni dhidi ya malaria. Baadhi ya wabunge tuliamua kuungana
ili tupeleke ujumbe huu kwa wananchi kwa urahisi ili tuweze kufanikiwa kwa
haraka zaidi,” alisema.
Post a Comment