Naibu Waziri wa Nishati na Madini Mh.George.(Picha na Maktaba).
Na Mahmoud Ahmad, Arusha.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini Mh.George Simbachawene amesema Uchumi wa mafuta na gesi unatarajia kujibu matatizo ya wananchi hivyo amewataka wanasiasa,wadau na vyombo vya habari kushirikiana ili kuongoza matarajio ya wananchi katika sekta hiyo.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri huyo mara baada ya kumalizika kwa kongamano la sita 6 la Afrika Mashariki linalohusiana na masuala ya mafuta ya petroli na gesi lililofanyika mjini Arusha lengo ikiwa ni kujadili fursa za uwekezaji na maendeleo ya sekta ya gesi na mafuta katika ukanda wa Afrika Mashariki ambapo nishati hiyo imegundulika hivi karibuni.Simbachawene amesema kuwa maslahi yanayotokana na nishati hiyo yataweza kutatua matatizo ya wananchi.
Simbachawene ameeleza kuwa katika kongamano hilo wameitangazia dunia juu ya fursa za uwekezaji katika sekta ya gesi na mafuta na matarajio yake ni kuwa ukanda wa Afrika Mashariki utakuwa ni ukanda wa mafuta na gesi kama wataalamu wa Sayansi ya miamba wanavyoeleza,akitolea mfano ukanda wa Ruvuma mpaka Msumbiji.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ambapo gesi ya asili imegundulika katika siku za karibuni kiongozi wa mkoa huyo Ndugu, Joseph Simbakalia anaeleza kuwa anatarajia kuwa wananchi wake watanufaika na fursa za kiuchumi zinazotokana na kuwepo kwa rasilimali hiyo na pia ndoto yake ni kuona kuwa katika miaka 10 hadi 15 ijayo Mtwara iwe sehemu inayoongoza kwa viwanda nchini Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa masuala ya huduma na sekta ya uzalishaji katika umuiya ya Afrika Mashariki (EAC),Bwana Nyamagege Wegoro amesema kuwa ni vyema serikali za nchi mwanachama wa jumuiya zikaangalia ni kwa kiasi gani rasilimali za gesi na mafuta ambazo ni za asili zinaweza kusaidia kukua kwa sekta nyingine za kiuchumi na kuleta maendeleo.
‘vizuri kujua ni kitu gani tunacho na kitu gani tunategemea kutokana na kuwa na rasilimali ya gesi na mafuta katika nchi wanachama wa jumuiya na hayo ndo maarifa yatakayotujengea uwezo wa kujua tulivyonavyo na tunaweza kubadilishana kwa fedha na pia kuwa kitu kimoja na sauti moja ili kuepuka unyonyaji kutoka mataifa ya kigeni ” Nyamagege Wegoro
Kwa miaka ijayo ukanda wa Afrika Mashariki unatarajia kuwa ukanda wa mafuta na gesi na kuongoza katika uwekezaji na usambazaji wa gesi na mafuta ndani na nje ya jumuiya ,hii ni kutokana na ugunduzi uliofanyika hivi karibuni na pia kwa mujibu wa wataalamu wa sayansi ya miamba.Lengo la Kongamano la sita 6 la linalohusiana na masuala ya mafuta ya petroli na gesi lililofanyika mjini Arusha ni kuwa na sauti moja kama wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki,kutetea maslahi ya wananchi,nchi moja moja na jumuiya kwa ujumla.
Post a Comment