Serikali imeanza mchakato
wa kumiliki Kampuni ya Mawasiliano Tanzania (TTCL) kwa asilimia 100 ikiwa ni
njia mojawapo ya kufanya mageuzi ya kibiashara na kuliendesha shirika hilo
kisayansi zaidi ya ilivyo sasa.
Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Mh. Januari Makamba aliyasema hayo mkoani
Dodoma mwanzoni mwa wiki hii wakati akielezea mikakati mbalimbali inayotaka
kuchukuliwa na serikali ili kuweza kulimiliki shirika hilo kwa asilimia 100
badala ya 65 za sasa.
Kwa sasa TTCL inamilikiwa
kwa ubia, serikali ikiwa na asilimia 65 wakati 35 zinamilikiwa na kampuni ya
simu za mikononi ya Airtel.
“Mazungumzo tayari
yameshaanza na dhamira yetu ni kununua aslimia 35 ya hisa zinazomilikiwa na
wenzetu ili serikali iweze kumiliki asilimia 100,” alisema Mh.
Makamba.
Alisema katika kufanya
mipango ya kwenda mbele kimaendeleo kupitia shirika hili ni lazima kufanya
mchakato wa kulimiliki kwa asilimia 100 ili serikali iweze kufanya mageuzi kwa
utashi wake kadiri inavyofaa.
Alifafanua kwamba hatua hii
ni Kutokana na changamoto zilizopo za kimuundo, kiungozi na ndio maana serikali
imechukua hatua za kinidhamu miongoni mwa baadhi ya watendaji waliobainika
kutumia madaraka yao vibaya ikiwa ni pamoja na kufanya ubadhirifu na hivyo
kulisababishia shirika hasara.
“Hii ni moja ya hatua
muhimu katika kuelekea kufanya mageuzi katika shirika hili kongwe hapa nchini,”
alisema.
Alizitaja changamoto
nyingine kuwa ni matatizo ya mtaji, na kusema kuwa ni lazima yashughulikiwe
ikiwa ni pamoja na kwenda na teknolojia mpya na kulifanya shirika lijiwekeze
kibiashara zaidi ya ilivyo sasa.
“Naamini katika kufanya
mageuzi makubwa bodi itachukua nafasi yake kwa maana ya uongozi wa shirika
katika kurekebisha mambo na mapungufu yaliyopo, kwa maana ya kuweka uongozi mpya
utakaoleta mabadiliko ili kulibadilisha liwe shirika kubwa la kisasa
linalotengeneza faida,” alisisitiza.
Alisema kutokana na
historia yake huko nyuma kampuni hii ilipaswa kuwa ndio kampuni inayoongoza
kimapato na pia kwa kutoa huduma nchi nzima kutokana na kuwa ipo kila wilaya
katika nchi, lakini kutokana na changamoto mbalimbali imekuwa ni tofauti na
matarajio yaliyowekwa wakati huo.
Alisisitiza kuwa wakati
sasa umefika kwa shirika kuwa katika mtazamo wa kuwekeza kibiashara zaidi na
ushindani.
“Shirika hili kongwe
limeendelea kubaki kama lilivyo na serikali imeliona hilo, kinachohitajika ni
kuwekeza katika rasilimali fedha na watu ili kukabiliana na ushindani wa
kibiashara uliopo sasa,” aliongeza.
Alisema mbali na changamoto
zote hizo lakini TTCL imefanikiwa kuunganisha Ofisi za Serikali, mashirika
mbalimbali, Taasisi za kifedha, utangazaji na Taasisi za elimu na hivyo
kuboresha matumizi ya huduma za mtandao wa mawasiliano kupitia Mkongo wa Taifa
wa Mawasiliano katika utoaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi.
“Kwa mfano huduma za video conferencing zinawezesha kuendesha mafunzo au mikutano kwa wahusika na hivyo kuongeza ushiriki, na kupunguza gharama,” alisema.
Akisikiliza
kero za wafanyakazi wa kampuni hiyo hivi karibuni, waziri Makamba aliiagiza bodi
ya Wakurugenzi ya TTCL kumtumia Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) kufanya ukaguzi
wa mahesabu ili kuthibitisha tuhuma za ubadhirifu wa fedha za kampuni hiyo ili
hatua za kisheria wakibainika.
Baadhi ya malalamiko
yaliyotolewa na wafanyakazi hao ni pamoja na uongozi na bodi dhaifu katika
ufuatiliaji mambo, ubadhirifu wa fedha za kampuni pamoja na uhamisho wa
wafanyakazi usofuata taratibu.
Post a Comment