UTAFITI wa Kitaifa wa Afya uliofanywa mwaka
2010 umeonyesha kuwa asilimia 72 ya wanawake na watoto wanaofanyiwa vitendo vya
ukatili wa kijinsia Mkoa wa Dar es Salaam ikiwa nafasi ya pili kwa kuwa na
asilimia 46 ambayo ni zaidi na kiwango cha ukatili huo nchi nzima ambacho ni
asilimia 44.
Kwa mujibu wa utafiti huo ambao ulifanywa na
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii umeonyesha kuwa Mkoa wa Tanga una idadi ndogo
ya vitendo hivyo ambapo ni sawa na asilimia 16.
Akizungumza jana Dar es Salaam katika mkutano
uliohusisha viongozi wa Mkoa na Wilaya Dar es Salaam kuhusu mwongozo wa kisera
na mwongozo wa kutoa huduma kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia, Mkuu wa Mkoa
huo, Said Meck Sadick alisema vitendo hivyo vimekuwa vikiongezeka kila siku na
kwamba vinatakiwa kukemewa.
Alisema kutokana na utafiti wa Kitaifa wa Afya
uliofanywa mwaka 2010, hali ya vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na
watoto inaonekana kuwa mbaya hasa katika Mkoa wa Dar es Salaam jambo ambalo
linatakiwa kuwekewa mikakati sahihi ili kutokomeza vitendo hivyo.
“Katika utafiti wa Kitaifa uliofanywa mwaka
2010, umeonyesha kuwa kiwango cha ukatili wa nyumbani kati ya wanawake wenye
umri wa miaka 15 hadi 49 ni asilimia 45 ambapo kwa Mkoa wa Dar es Salaam sababu
kubwa inaweza kuwa mwingiliano wa watu kitu ambacho ni vyema kikaangaliwa kwa
undani ili kuondoa vitendo hivyo,” alisema Sadick.
Alisema ukatili huo unajumuisha ukatili wa
kimwili asilimia 25, kingono asilimia saba na asilimia 14 kwa aina zote mbili.
Ukatili wa wanawake wajawazito ni asilimia tisa na asilimia 60 inaonyesha kwamba
wanawake wajawazito hushurutishwa kufanya ngono na wapenzi wao bila ridhaa
yao.
“Matukio ya ukatili wa kijinsia yanatofautiana
kati ya mkoa na mkoa. Mkoa wa Dar es Salaam utafiti unaonyesha kuwa asilimia 46
ya wanawake na watoto wanafanyiwa vitendo hivyo na asilimia 74 katika Mkoa wa
Mara,” alisema Sadick.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la Usimamizi na
Maendeleo ya Afya (MDH), Dk Guerino Chalamilla alisema kila mtu anatakiwa kuwa
mstari wa mbele kukemea vitendo hivyo kwani havikubaliki katika jamii na kwamba
ni kinyume na sheria.
Alisema MDH kwa kushirikina na Serikali
wameweka mikakati sahihi ya kuhakikisha wanatoa elimu kwa watu wanaofanya
vitendo hivyo ili kupunguza ukatili wa kijinsia wanaofanyiwa wanawake na
watoto.
“Kwa kushirikina na Serikali tutahakikisha
tunapiga vita na kuweka mikakati sahihi ambayo inasaidia kutokomeza vitendo vya
ukatili wa kijinsia kwa wanawake,” alisema Dk Chalamilla.
Chanzo: Mwananchi
Post a Comment