|
|
WAKATI wadau wa tasnia ya habari wakihoji ubabe uliotumiwa na
serikali kulifungia gazeti la wiki la MwanaHalisi kwa madai ya
uchochezi, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Assa Mwambene,
amembebesha sakata hilo Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto.
Mwambene katika kuivua lawama serikali, alidai kuwa Zitto alikuwa mtu
wa kwanza baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo, aliyemtahadharisha
asiende ofisini kumchekea Mkurugenzi wa Kampuni ya Hali Halisi,
wachapishaji wa MwanaHalisi, Said Kubenea ili isije kumharibia kazi.
Serikali ililifungia gazeti la MwanaHalisi Julai 30 mwaka jana,
kutochapisha nakala yoyote kwa muda usiojulikana kwa madai ya kuandika
habari na makala ya uchochezi.
MwanaHalisi ndilo gazeti lililoandika kwa undani tukio zima la watu
wanaoshukiwa kumteka kumpiga, kumng’oa meno na kisha kumtelekeza
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madakatari nchini, Dk. Stephen Ulimboka.
Mwambene ambaye aliteuliwa kushika nafasi hiyo kutoka kwa Clement
Mshana aliyehamishiwa TBC, alijikuta akitoa siri hiyo Ijumaa iliyopita
wakati wa kongamano la kutimiza miaka 50 ya Redio ya Ujerumani
‘Deutsche Welle’ (DW) Idhaa ya Kiswahili lililofanyika kwenye Ukumbi wa
Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam.
Hatua hiyo ilikuja baada ya kubanwa kwa maswali yaliyokuwa
yanamshutumu yeye na serikali yake kubana uhuru wa vyombo vya habari,
huku baadhi ya washiriki wakiinyooshea kidole cha moja kwa moja
serikali katika suala zima la kulifungia MwanaHalisi ili lisizidi
kuwaumbua.
Katika utetezi wake, Mwambene alisema serikali haizuii uhuru huo, na
hata hatua ya kufungiwa kwa baadhi ya magazeti ni kwa sababu ya kulinda
hadhi ya nchi.
Alitolea mifano nchi za Magharibi zinazodaiwa kuwa na demokrasia kuwa
nazo zinafungia au kuvifuta vyombo vya habari vyenye mwelekeo wa
uchonganishi.
Alisema kwa mara ya kwanza akiwa mkurugenzi wa idara hiyo, alipofika
bungeni kujitambulisha kwa wabunge, aliitwa pembeni na Zitto, na
kutahadharishwa juu ya MwanaHalisi.
“Mnasema sisi tunaminya uhuru wa vyombo vya habari kwa kutolea mifano
nchi za Uingereza na Marekani…mnaweza kuniambia leo Assange, yule
mmiliki wa mtandao wa Wikileaks yuko wapi au gazeti la News of the
World lilipo? Haya mambo yanafanyika hata katika nchi mnazozisifia kuwa
na demokrasia.
“Na niseme kabisa nilipokwenda bungeni kama Mkurugenzi wa Idara ya
Habari - Maelezo, Zitto aliniita pembeni na kuniambia katika kazi yangu
mpya nisiende kumchekea Said Kubenea,” alisema Mwambene.
Kauli hiyo ilizua minong’ono kutoka kila kona ya ukumbi huo, huku
baadhi ya washiriki wakisema serikali inatafuta sehemu ya kufichia
udhaifu na ukandamizaji wa uhuru wa vyombo vya habari kwa kuwahusisha
baadhi ya watu na uamuzi wa kuminya uhuru huo.
Tanzania Daima lilimtafuta Zitto kujua msimamo wake kuhusu kauli hiyo
ya Mwambene katika suala zima la kufungiwa kwa gazeti la MwanaHalisi,
lakini akajibu kwa kifupi kuwa hausiki.
“Sasa mimi ni mwajiri wake? Hayo maneno ni ya kutuchonganisha tu
hayo, mimi nina nguvu gani ya kusema hivyo? Inaingia akilini kweli?”
alijibu Zitto kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu yake ya mkononi.
Hata hivyo, Mwambene aliwashangaza waliohudhuria kongamano hilo baada
ya kusema kuwa serikali imetoa uhuru mkubwa wa habari ambapo baadhi
huitukana serikali, lakini hawafanywi kitu.
Baadhi ya wageni wengine walioalikwa kama wazungumzaji wakuu na kutia
fora, ni nguli wa habari nchini, Jenerali Ulimwengu, mwanablog mahiri
Majjid Mjengwa, Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake
Tanzania (Tamwa), Valerie Msoka na Naibu Mkuu wa Idhaa DW, Mohamed
Abdulrahman.
Sakata la kufungiwa kwa gazeti hilo kwa sasa limezidi kuwa tata
kutokana na Rais Jakaya Kikwete kunukuliwa hivi karibuni akiwa mjini
Addis Ababa nchini Ethiopia kuwa hatalifungulia kamwe kutokana na kosa
la kuchochea.
Pamoja na kwamba hakulitaja kwa jina, lakini kwa sasa nchini gazeti
hilo ndilo limefungiwa kwa kosa hilo la kudaiwa kuchochea.
Kutokana na msimamo huo wa Rais Kikwete, Chama cha Wamiliki wa Vyombo
vya Habari nchini (MOAT) hivi karibuni kilikutana na kujadili sakata
hilo na kuteua kamati ya wajumbe wa kukutana na rais kumshauri.
Wajumbe hao wataongozwa na Mwenyekiti wa MOAT, Reginald Mengi ili
kukutana na Rais Kikwete ambaye wanaamini kwa sasa ndiye pekee anaweza
kutoa uamuzi wa kufunguliwa kwa gazeti hilo.
Tanzaniadaima
|
|
on Monday, February 25, 2013
Post a Comment