Ndugu zangu,
Uchaguzi Mkuu wa Kenya
umefuatiliwa kwa karibu sana na sisi Watanzania, ni pamoja na wanasiasa wa vyama
vya siasa; Chama tawala, CCM na wapinzani.
Lakini, nahofia, kuwa hakuna
ambacho vyama hivi vyetu vya siasa vitajifunza kutoka Kenya.
Ndio, pamoja
na mapungufu ya hapa na pale, lakini Wakenya, kupitia Uchaguzi wao wametuachia
somo kubwa sana; kuwa hata Afrika tunaweza kuendesha siasa za kistaarabu ikiwemo
chaguzi Huru.
Ni kawaida kwa majirani sisi; Kenya na Tanzania, kuoneana
wivu kwenye kupiga hatua kimaendeleo. Hakika ni wivu wa kimaendeleo tunaopaswa
kuwa nao. Nikiri, safari hii, kama Mtanzania, nimejisikia kuwaonea wivu Wakenya
kwa jinsi walivyoionyesha Afrika na Dunia kuwa nao wanaweza kuwa Taifa Kubwa;
kisiasa na kiuchumi.
Mchakato ule wa mabadiliko ya Katiba yao na hata
kufanya uchaguzi ule kwa amani na uwazi ni USHINDI mkubwa wa kimfumo. Ni ushindi
wa Wakenya wote. Kwamba Wakenya wameujaribu mfumo mpya. Umeonyesha kuwa
unafaa.
Kwa mfano, kufuatilia matokeo ya uchaguzi ule kutoka kwenye Tume
yao Huru ilikuwa ni kama ‘ burudani’ ya kisiasa. Kila kitu kilikuwa kinawekwa
wazi na kisayansi.
Si ajabu Wakenya waliweza kusubiri matokeo kwa juma
moja bila kurushiana mawe. Na hata kama ingekuwa kusubiri kwa majuma mawili,
naamini kuwa Wakenya wale wangesubiri bila kupigana, maana, wamekuwa na imani
kubwa na Tume yao Huru ya Uchaguzi. Na hatukusia kule Kenya, habari ya watu ‘
kulinda kura’ wala kusimama hatua mia moja kutoka kituo cha kuhesabia kwa usiku
mzima. Hiyo kazi iliachiwa Tume Huru ya Uchaguzi walioiamini.
Ndio,
Wakenya wamejifunza kutokana na ujinga wa wanasiasa wao uliopelekea vurugu za
baada ya Uchaguzi wa mwaka 2007. Wengi walikufa na wengine kupoteza makazi na
mali zao. Wakaanza haraka mchakato wa kuifanyia marekebisho makubwa Katiba yao.
Wakapata Katiba Mpya 2010. Wakenya wale wametumia gharama kubwa kwa kuitafuta
amani yao. Kimsingi, tangu 2010, Wakenya wamekuwa ‘ wakiangushiwa mabomu ya
ujumbe wa amani’- Ni kila kukicha.
Serikali yao imetumia fedha nyingi
sana kufikisha ujumbe wa amani kwa Wakenya. Sasa wanavuna walichopanda; kuwa na
chaguzi huru za amani na utulivu. Na walichokitafuta Wakenya kwa gharama kubwa,
kwa maana ya amani, sisi Watanzania tulikuwa nayo, sasa tunaipoteza wenyewe ili
baadae tuanze kugharamia kuitafuta. Ni ulimbukeni.
Kwa kupitia Katiba yao
ya sasa Wakenya wameweza kupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la ukabila. Kwa
namna gani?
Ona kwenye kugombea Urais; mgombea lazima afikishe asilimia
50+1 ( Asilimia 50 na kura moja) ili aweze kutangazwa mshindi. Mgombea pia
lazima akubalike kwa asilimia 25 ya Counties zote ( Majimbo yote).
Sasa basi,
kwa Kenya, Wakikuyu ni asilimia 23 ya Wakenya. Wajaluo asilimia
11.
Nyingine zilizobaki ni za makabila mengine madogo madogo. Hivyo, ili
mgombea ushinde zaidi ya asilimia 50 una lazima ya kukubalika kwenye maeneo
mengine nje ya wigo wa kabila lako. Kwamba kula za Wakikuyu pekee kwa Uhuru
Kenyatta zisingetosha, vivyo hivyo kwa Odinga.
Utaratibu huo unaua
ukabila na kujenga vema misingi ya Utaifa. Hata kama itachukua muda kufika mbali
zaidi katika hilo lakini Wakenya wameanza kuondokana na ukabila kwenye siasa
zao, kwa kupitia Katiba.
Kwa mantiki hiyo hiyo, Watanzania tungeweza
kabisa kuondokana na siasa za udini kwa kuweka, kwenye Katiba yetu ijayo sharti
la mgombea Urais kushinda kwa asilimia 50+1 ( Asilimia 50 jumlisha kura 1). Hilo
lingewafanya wanasiasa wetu wenye kuwania Urais na vyama vyao pia ‘ Kutia
akili’.
Maana ingekuwa na tafsiri moja kuu; kuwa mgombea na chama chenye
kuendekeza udini kisingekuwa na nafasi ya kutoa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania wala nafasi ya kushika dola. Maana, hakuna dini hapa Tanzania yenye
idadi ya waumini wanaovuka asilimia 50 ya jumla ya Watanzania.
Kwa maana,
hiyo, muarobaini wa kumalizana na udini uko kwenye Katiba ijayo, kama tuna nia
ya dhati ya kutoka hapa tulipo. Vinginevyo, udini huu tunaosema kuwa ni tatizo
tutakuwa tunaulea wenyewe.
Hata tatizo la siasa za ukanda nalo litapotea,
maana, hakutakuwa na mgombea au chama kitakachoweza kushinda na kutoa Urais kwa
kuegemea kura za kikanda. Hakuna kanda itakayovuka peke yake asilimia 50 ya kura
zote. Chama na mgombea kitahitaji kuungwa mkono na wapiga kura wa kanda hata
zilizo nje ya anakotoka mgombea Urais.
Vinginevyo, kama alivyotamka Uhuru
Kenyatta kwenye hotuba yake nzuri iliyojaa utaifa hivi majuzi, kuwa katika
uchaguzi waliofanya, kila kura ilikuwa ina umuhimu. Hivyo, kila kabila lilikuwa
na umuhimu. Na Uhuru Kenyatta akaweka wazi anachotaka Serikali yake kwa
kushirikiana na Wakenya kufanya ili kuitoa Kenya hapo ilipo na kwenda
mbele.
Kenyatata alimalizia na maneno matatu; Forward, Foward. Foward!-
Kusonga mbele!
Ndio, Wakenya wameamua; KENYA KWANZA!
And really, The
Kenyans are coming, Big Time!
Ni ukweli, Wakenya wanakuja. Kisiasa na
kiuchumi. Sisi hatujajipanga na hatutaki kujipanga kwa dhati. CCM na wapinzani,
na hata media yetu, kama kawaida, tumerudi kwenye kucheza ‘ Kiduku’ chetu.
Hatuna cha kujifunza kutoka Kenya. Tumerudi kwenye mambo yetu ya hovyo hovyo; ni
Siasa za Mwembe Yanga na Viwanja Vya Jangwani. Siasa za kupigana vijembe. Siasa
za reja-reja- Retail politics.
CCM na wapinzani ni kama vile wapenzi wa
soka. Wanaangalia kila siku soka la majuu. Wataongea sana kuhusu soka la majuu
lilivyo bora.
Lakini, wakirudi kwenye soka lao, ni yale yale, hawana cha
kujifunza na hawataki kujifunza. Ni madudu kwenye kuendesha vilabu na hata
kufikia kununua mechi kwa kuhonga marefa, wachezaji na viongozi. Ukisema nini
hiki?
Utajibiwa; “Wewe Bongo mpira pesa bwana!” “Mpira fitna!” Ni kama
majibu ya wanasiasa, iwe wa CCM au vyama vya upinzani. Nao watakwambia; “Wewe,
Bongo siasa pesa bwana!” “ Siasa mizengwe na fitna!”
Naam, nahofia, kuwa
CCM na wapinzani hawana cha kujifunza kutoka Kenya!
Maggid
Mjengwa,
Iringa,
0788 111 765mjengwablog.co.tz
Loading...
Post a Comment